Wednesday 24 January 2018

Mwanafunzi auawa kikatili

Na Walter Mguluchuma
Katavi

JESHI la polisi mkoani Katavi linamsaka mtu asijejulikana kwa tuhuma za kumbaka,kumchoma kisu,kumuua na kisha kukata sehemu za siri za mwanafunzi(14) wa  darasa la sita shule ya msingi  Vikonge wilaya ya  Tanganyika na kukimbilia kusiko julikana.

Akitoa taarifa ya tukio hilo kamanda wa polisi Damas Nyanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1;30 za asubuhi wakati marehemu akiwa anakwenda shule akiwa ameongozana na mdogo wake ambaye wanasoma shule moja.

Alisema kuwa siku ya  tukio hilo marehemu  alitoka  nyumbani akiwa na mdogo wake wa kiume  mwenye  umri wa miaka 11  mwanafunzi wa   darasa  la  nne  ambaye waliongozana wakielekea  shule ya  msingi  vikonge ambayo wanasoma.
Kamanda Nyanda alisema wakiwa  njiani  alitokea  mwendesha  pikipiki maarufu kwa jina bodaboda  ambae walikuwa  hawamfahamu  na  kusimamisha  pikipiki yake  na  kuwaambia anataka  awape  lifti ili wafike haraka shuleni  kwao.

Alisema  baada ya  kuambiwa  hivyo  wanafunzi hao walikubali  hata  hivyo alimtaka apande kwenye bodaboda hiyo mtoto huyo wa kike peke yake na aliondoka na kumwacha mdogo wake wa kiume.

Baada ya kunyimwa lifti hiyo mdogo wake aliamua kutembea kufuata nyuma hata hivyo akiwa  njiani  aliona  pikipiki  kama  ile  iliyokuwa imembeba  dada yake ikiwa kwenye kichaka  pembeni ya  barabara  lakini hakwenda kuangalia badala yake aliendelea  na  safari yake ya  kwenda  shule.

Mdogo wake huyo na marehemu  kutokana  na umri  kuwa mdogo alipofika shuleni hakumtafuta  dada yake na   badala yake  aliingia  darasani na  kuendelea  na  masomo  kama    kawaida   na   baada ya muda wa  masomo  ulipofikia  majira ya  saa 8;30  alianza  safari ya  kurejea  nyumbani pasipo kumtafuta  dada yake.

Kamanda  Nyanda   alieleza kuwa  baada ya kufika  nyumbani kwao wazazi wake walishituka  kumwona  akiwa  peke  yake  ndipo  walipomuuliza  aliko  dada  yake  na   aliwaeleza  mazingira yote  ya jinsi  alivyo  achana  na  dada  yake wakati walipokuwa  njiani  na  jinsi alivyoiona   pikipiki  iliyombeba dada yake ilivyokuwa  kichakani.

Wazazi wa  marehemu  baada ya  kupata  maelezo  hayo walipatwa na mashaka   ambapo  walimtaka  mdogo wa marehemu  awapeleke  kwenye  eneo   aliloona  pikipiki ile.

Alisema  wazazi wa marehemu waliokuwa wameongozana  na majirani zao  baada ya kufika  kwenye  eneo  hilo walishitushwa  kuona  majani yakiwa  yamelala  na  ndipo walipokwenda  mbele kidogo wali ukuta  mwili wa marehemu  ukiwa  amechomwa  kifu  sehemu ya  ubabu wake wa kulia  na  sehemu za  siri  zikiwa  zimenyofolewa.

 Kwaupande wake kaimu   mwalimu   mkuu wa  shule ya msingi Vikonge   Gadinendi   Kaseka  alisema    mpaka   walipomaliza  masomo ya siku  hiyo  hawakuwa na  taarifa juu ya kifo cha mwanafunzi huyo ila walipata taarifa hiyo siku  hiyo  hiyo  majira ya saa kumi na  mbili jioni  baada ya mwili wa marehemu kuwa umepatikana.

Kamanda huyo wa  polisi alisema kuwa wazazi na majirani walikwenda polisi kutoa taarifa ambapo polisi walifika na kuuchukua mwili wa marehemu na msako wa mtu aliyefanya tukio hilo unaendelea.

Mwisho

Sunday 21 January 2018

Waandishi watakiwa kuandika bila hofu

Gurian Adolf
Kalambo

SERIKALI mkoani Rukwa imewataka waandishi wa habari mkoani humo kuyaandika na kuyatangaza mambo mazuri na changamoto zilizopo bila kuhofia mtu yeyote kwani maendeleo ya mkoa huo yatapatikana kwa kuyatangaza mambo yaliyomo katika mkoa huo bila hofu.
Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo aliwaambia waandishi wa habari wa mkoa huo jana wakati akizindua zoezi la upandaji miti milioni sita lililofanyika juzi katika mji wa Matai wilayani Kalambo.
Alisema kuwa waandishi wa habari ni wadau wakubwa wa maendeleo ya mkoa huo hiyo wanawajibu wa kuandika mambo mazuri na mabaya yaliyopo katika mkoa wa Rukwa kwani kushindwa na kufanikiwa kwa mkoa huo nao kunawahusu.
Wangabo alisema kuwa waandishi wa habari wanatumia kalamu katika kuchangia maendeleo hivyo wajue wanajukumu la kuandika mazuri na changamoto ili mkoa upige hatua kwani wakikaa kimya mkoa ukikosa maendeleo nao itawagharimu.
''waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa nawaagizeni andikine vitu vyote vinavyoendelea katika mkoa wa Rukwa,pigeni picha na tangazeni yote bila kumuogopa mtu na asiwepo mtendaji ambaye anakataa kuwapa ushirikiano" alisema.
Alisema kuwa yeye binafsi yupo tayari kuona mkoa wake ukitangazwa kwa mazuri pamoja na changamoto zake kwani ndiyo fursa ya kupiga hatua,na kazi hiyo waandishi wanapaswa kuifanya kwa kuzingatia misingi ya taaluma yao.
Mkuu huyo wa mkoa aliwataka waandishi wa habari kutembea vijijini kuandika habari za uharibifu wa mazingira pamoja na kuhamasisha wananchi wajitume katika kilimo cha kisasa na ufugaji wenye tija kwani mkoa huo unahitaji maendeleo.
Awali akimkaribisha mkuu huyo wa mkoa, mkuu wa wilaya ya Kalambo Juliath Binyura alisema kuwa wananchi wa wilaya ya Kalambo wamejipanga katika kutekeleza zoezi la upandaji miti kwani wanatambua kuwa miti ni uhai.
Alisema kuwa halmashauri ya wilaya hiyo ipo tayari kuwadhibiti watu watakao baininika kuharibu mazingira kwakuwa serikali inatumia fedha nyingi na muda hivyo ni lazima waone thamani ya miti.
Binyura alisema kuwa kwakuwa mkuu wa mkoa amekwisha zindua kampeni ya upandaji miti wananchi wameipokea na wanahakikisha watafikia lengo kwa asilimia mia moja kwani wao ni wakulima na wanahitaji mvua ambayo haiwezi kupatikana bila kuwepo misitu.
Mwisho

Halmashauri yaagizwa kujenga Mwalo

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

MKUU wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani humo kutafuta fedha ili ijenge mwalo wa Nankanga katika ziwa Rukwa utakao wasaidia wavuvi kufanya biashara ya samaki na utakuwa ni chanzo kizuri cha mapato kwa halmashauri hiyo.
Agizo hilo alilitoa jana wakati alipokuwa akifanya ziara ya kukagua makambi ya wavuvi wa samaki katika jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu uliotokea wilayani humo tangu mwezi Novemba mwaka jana ambapo usababisha vifo vya watu nane na 270 kuugua ugonjwa huo.
Alisema kuwa ufukwe uliopo katika makambi ya wavuvi ya Nankanga katika ziwa Rukwa  wilayani Sumbawanga linafaa kwaajili ya kujenga mwalo ambapo wavuvi watakuwa wanafanya biashara ya samaki na kisha halmashauri kupata fedha kwa kutoza ushuru.
''naagiza halmashauri ya wilaya ya Nkasi itafute fedha ili ijenge mwalo huu wa Nankanga kwani eneo hili ni zuri kwa wafanyabiashara kuuzia samaki ambapo pia itakuwa ni chanzo kizuri cha mapato kwakuwa mtakusanya ushuru na halmashauri yenu itapata fedha''
Alisema kuwa wilaya hiyo imejaliwa fursa nyingi ambazo kama zikitumika ipasavyo zitaongeza makusanyo na halmashauri itapata fedha nyingi na itaweza kuwahudumia wananchi ili waaweze kuondokana na changamoto mbalimbali zinazo wakabili.
Alisema kuwa nilazima  itafutwe namna fedha zipatikane haraka na mwalo huo ujengwe kwakuwa wananchi wanahitaji huduma nzuri kwani ni jukumu la watendaji kuzitambua fursa zilizopo na kuzitumia ipasavyo.
Awali akitoa taarifa ya ugonjwa wa kipindupindu katika halmashauri hiyo Kaimu mkurugenzi ambaye ni Mganga mkuu wa wilaya hiyo Fani Musa alisema kuwa kipindupindu kimedhibitiwa licha ya kuwa bado jitihada zinahitajika kutoa elimu ya afya kwa wavuvi.
Alisema kuwa changamoto iliyopo ni kutotumia maji safi na salama kwani baadhi ya wavuvi wanakataa kutumia maji yanayotibiwa kwa dawa aina ya waterguard kwamadai kuwa hayana radha.
Mwisho

Ahukumiwa viboko

Na Gurian Adolf
Nkasi

MAHAKAMA  ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemuhukumu  Paschal Kabagi (18)  kuchapwa viboko sita baada ya kupatikana na  hatia ya kumbaka  mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 anzyesoma Kidato cha Kwanza katika shule ya Sekondari Nkomolo wilayani humo.

Akisoma hukumu  hiyo mwishoni mwa wiki jana,hakimu wa mahakama hiyo,Ramadhani  Rugemalira  alisema  kuwa kwa kuwa mshtakiwa alitenda kosa  hilo akiwa na umri wa miaka  17 ataadhibiwa kwa kucharazwa viboko sita ili iwe  fundisho kwa wengine wenye tabia kama yake.

Awali  mwendesha mashtaka mkaguzi wa Polisi , Hamimu Gwelo alidai mahakamni hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo  Januari 12 , 2016 majira  ya saa  mbili asubuhi katika kitongoji cha Uwanja wa Ndege kilichopo mjini Namanyere wilayani Nkasi.

AlidaI mahakamani hapo kuwa  wakati akitenda kosa hilo mshitakiwa  alikuwa akisoma Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Nkasi.
Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo alimvizia mwanafunzi huyo wa kike kwenye mahindi wakati akienda shule ndipo alipo mshika kwa nguvu na kisha kumuangusha chini na kumbaka.

Mshtakiwa alijitetea kwa kuiomba mahakama  imsamehe kwa kuwa  hakujua kuwa alichokifanya kilikuwa kosa kisheria utetezi uliopingwa na mwendesha masthaka na kisha mahakama hiyo ikaamua kutoa hukumu hiyo .

Mwisho

Friday 19 January 2018

Wakware Nkasi waonywa

Na Gurian Adolf,
Nkasi

KATIKA kukabiliana na tatizo la mimba kwa wanafunzi wanaume wilayani Nkasi  wameonywa  kuacha mara moja tabia ya kuwaita watoto hao wa kike majina ya mahaba kwani yanawapelekea kujiona wamekua na kuanza kushiriki vitendo vya ngono

Wito huo umetolewa jana na afisa elimu Sekondari wilayani Nkasi Abel Ntupwa  kwenye kikao kazi kilichowajumuisha Wakuu wa shule 23 za sekondari wilayani Nkasi  kilichomshirikisha na afisa elimu wa mkoa Nestory Mloka kilicholenga kupeana mikakati namna ya kuboresha taaluma baada ya wilaya Nkasi kuporomoka sana kwenye mitihani ya kitaifa.

Alisema hivi sasa watu wazima wamekua na tabia ya kuwaita watoto hao wa kike ambao ni Wanafunzi majina ya kimahaba kama  Baby kama mzaha na mwisho wa siku ujikuta Watoto hao wanajiingiza kwenye mtego huo mbaya na hivyo kuanza kushiriki vitendo vya mapenzi.

Hivyo  kufuatia hari hiyo amedai kuwa ni marufuku kwa mtu yeyote  kumwita mtoto wa kike ambaye ni Mwanafunzi majina hayo ya Baby ili kuwaweka Watoto hao katika hari ya usalama.

Lakini pia alikemea tabia ya baadhi ya Walimu wenye tabia ya kujihusisha kimapenzi na Wanafunzi au hata kuwatamani kuwa hakuna dhambi kubwa kwa Mwalimu kama hiyo na kuwa hakuna atakaebaki salama kwa kujihusisha na tabia hizo pindi itakapobainika.

Lakini pia aliwataka Wakuu wa shule kuhakikisha kuwa wao ndiyo wakaguzi wa kwanza katika shule zao kwa kuhakikisha kuwa Walimu wao wanafundisha sawasawa na kuleta tija ya kitaaluma katika masomo wanayoyafundisha.

Alisema shule yoyote inayofanya vizuri ni matokeo ya uongozi bora wa shule ambapo Walimu wakuu wameamua kuzisimamia shule zao na kuwa sasa wameamua kuboresha elimu wilayani Nkasi nas kutaka Wakuu wa shule kusiomama imara na kama kuna ambaye atakwenda kinyume na kasi hiyo  watamshughulikia mara moja.

Kwa upande wake afisa elimu wa mkoa wa Rukwa Nestory Mloka alisema kuwa yeyebinafsi kamwe hawezi kusita kuwavua madaraka Walimu wakuu ambao wataonyesha kushindwa kuzisimamia shule zao ili zitoe matokeo chanya na kuwa haoni sababu kwa wilaya Nkasi iliyokuwa inaongoza katika mkoa Rukwa sasa imeanza kushika mkia.

Alisema kwa kuanza wameanza na mabadiliko madogo ambapo wameteua baadhi ya waratibu wa elimu kata kutoka katika shule za Sekondari na msingi na kuwataka washirikiane nao vizuri na kuwa wanataka kuona mwaka huu mabadiliko yanatokea lakini kinyume cha hapo alisema kuwa hatamuelewa mtu.

Mwisho

Watoto 400 wakosa elimu

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

JUMLA ya watoto wa wavuvi wapatao 400 waliopo katika kambi ya wavuvi ya Nankanga wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ambao wamefikia umri wa kuanza darasa la kwanza wameshindwa kupata haki yao ya elimu kutokana na kutokuwa shule.
Diwani wa kata ya Nankanga wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, Anyisile Kayuni alimwambia hayo mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo wakati akiwa katika ziara ya kukagua makambi ya wavuvi katika suala la kukabiliana na ugonjwa wa kipindu pindu.
Alisema kuwa watoto hao wanaishi na wazazi wao katika kambi hiyo ya Nankanga iliyopo katika kijiji cha Nankanga,kata ya Nankanga na wamefikia umri wa kuanza shule ya msingi lakini wameshindwa kutokana na kuwa katika eneo walilopo hakuna shule.
Diwani huyo alisema kuwa shule ya msingi ipo umbali wa kilomita tisa kutoka yalipo makambi hayo umbali ambao ni mkubwa huku ukikabiliwa na changamoto ya barabara kitendo kinachosababisha washindwe kwenda shule.
alisema kuwa kwa kuliona hilo yeye kupitia uongizi wa makambi hayo walikubaliana kujenga shule ambapo mbapa sasa wamejenga vyumba viwili vya madarasa na kufikisha usawa wa lenta ambapo wanaiomba serikali ya mkoa iwasaidie bati 100 wapaue vyumba hivyo na kuwapelekea walimu ili watoto hao waanze kusoma.
Alisema kuwa katika kambi hiyo wavuvi waliopo wanajitahidi kuzingatia huduma za afya bora ikiwamo ni pamoja na kuchimba vyoo, pia wanapata huduma za dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ambapo wapo watu 270 wanaotumia dawa hizo na wameweka mkakati kuhakikisha kuwa hawaachi kutumia ili waishi maisha yenye afya na marefu.
Kwaupande wake mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alifurahishwa na hatua ya wananchi hao kuanzisha suala la ujenzi wa shule ili watoto hao wapate elimu ambapo aliahidi ofisi yake itatoa bati 50 na aliigiza halmashauri ya wilaya hiyo kutoa bati nyingine 50 ili vyumba hivyo vya madarasa vipauliwe na watoto hao waanze  shule mara moja.
Mwisho

Rukwa kupanda miti milioni sita

Na Gurian Adolf
Kalambo

MKOA wa  Rukwa umezindua kampeni ya upandaji miche ya miti kwa lengo la kuhifadhi mazingira ambapo katika kipindi cha mwaka huu unatarajia kupanda jumla ya  miche milioni sita katika halmashauri zote nne za mkoa huo.

Akizundua kampeni katika halmashauri ya wilaya ya Kalambo, katika mji wa Matai mkuu wa mkoa huo Joachim Wamgabo alisema kuwa kila halmashauri italazimika kupanda miche isiyopungua milioni 1.5 ambapo mpaka sasa tayari mkoa mzima umeotesha miche milioni 2,173,649 sawa na asilimia 36 ya miche itakayo pandwa.

Alisema kuwa yeye  amezindua kampeni hiyo kinachofuata ni watendaji wa serikali kuhakikisha kuwa wanasimamia na kutekeleza na itakapofikia mwishoni mwa mwaka halmashauri ambayo haitafikia lengo itatozwa faini ya shilingi milioni moja na fedha hizo itakabidhiwa halmashauri ambayo imetekeleza kampeni hiyo kwa asilimia mia moja.

Awali kabla ya kuzindua kampeni hiyo Wangabo alimuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kalambo Simon Ngagani amwajibishe Afisa mtendaji wa kiji cha Matai Ester Mwashambwa kwa kitendo cha kushindwa kuwahamasisha wananchi wananchi wajitokeze katika uzinduzi wa kampeni hiyo kwani waliofika walikuwa ni wanafunzi wa shule ya sekondari Matai na watumishi wa serikali.

Alisema kuwa wananchi ni wadau wakubwa katika suala la uhifadhi mazingira na ndiyo wakataji miti wakubwa kwa lengo la kupata nishati ya mkaa na kuni lakini kitu cha ajabu hawakuwepo katika uzinduzi huo hali iliyomkera mkuu huyo wa mkoa.

‘’nakuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kalambo kumwajibisha afisa mtendaji wa kijiji kwani ameshindwa kuwahamasisha wananchi wajitokeze,kitendo hiki sijakipenda inaonekana huu ni utendaji mbovu,serikali haiwezi kuwavumilia watendaji wa aina hii’’ alisema

Naye mwakilishi wa wakara wa misitu Tanzania TFS wilaya ya Kalambo, Herman Ndanzi alisema kuwa wakara huo unajumla ya hekta 1192 ambazo unazihudumia licha ya kuwa bado jitihadazinzfanyika za kupanda miti ili kuongeza misitu.

Alisema kuwa wakara huo umewapatia wananchi kilogramu 6 za mbegu za miti ya aina tofauti ili wakaipande ambapo itasaidia kuhifadhi mazingira na kuwa inaendelea na suala kuwaelimisha wananchi waache kuharibu misitu.

Mwisho

Tuesday 9 January 2018

Dc apiga marufuku kuwapeleka wagonjwa wa kipindu pindu kwa waganga wa jadi

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa,  Dk. Halfan Haule amewataka wakazi wa bonde ziwa Rukwa, kuacha tabia ya kuwapeleka wagonjwa wa kipindupindu kwa waganga wa kienyeji badala yake wawapeleke vituo vinavyotoa huduma za afya ili kupata tiba za kitaalamu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Mtowisa wilayani Sumbawanga mkoani humo.

Alisema tabia ya baadhi ya wananchi kuendekeza imani za kushirikina na kuwapeleka wagonjwa wa kipindupindu kwa waganga wa kienyeji kunahatarisha maisha ya wagonjwa hao na wakati mwingine kusababisha vifo.

Alisema jamii ya watu wa bonde la ziwa Rukwa ambako ugonjwa huo umeenea ipo haja sasa kubadilika na kuachana na tabia hiyo, kwani ugonjwa huo unatokana na uchafu na si  kulogwa hivyo wanapaswa  kuwapeleka wagonjwa  katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ili wapate tiba sahihi ambazo zitaokoa maisha yao. 

Dk. Haule alipiga marufuku tabia ya kaya moja kutumia choo kimoja badala yake alitaka kila kaya kuwa na choo chake na kaya isiyokuwa na choo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Awali,mganga mkuu wa wilaya hiyo,Fani Mussa alisema kuwa tangu ugonjwa wa kipindupindu uingie katika halmashauri hiyo siku 53 zilizopita jumla ya wagonjwa 165 wameugua kulazwa katika vituo vinavyotoa huduma ya afya  ambapo nane kati yao wamefariki dunia.

Alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa pamoja na kuchukuliwa kwa sampuli 15 ambazo zilithibitisha kuwa na ugonjwa huo hivyo kusambaza dawa na vifaa tiba katika kambi mbalimbali zilizofunguliwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hao.

Alisema kuwa elimu ya afya inayolenga kuwahamasisha wananchi kuzingatia kanuni za afya, ikiwa pamoja na kuchemsha maji kabla kunywa na kunawa mikono baada kutoka chooni imetolewa kwa wakazi wa bonde la ziwa Rukwa ambalo vijiji vyake vingi vimeathirika na malazi hayo. 

Dk. Mussa alisema watu 14 kati ya 58 Waliokamatwa kwa kukiuka kanuni za afya ikiwa pamoja na kaya zao kutokuwa na vyoo wamehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela.

Mwisho.

Rc apiga marufuku kupakia mizigo katika mwalo wa Kirando

Na Gurian Adolf
Nkasi
SERIKALI mkuu mkoani  Rukwa imepiga marufuku  kuutumia mwalo uliopo katika  Kijiji cha Kirando ziwa Tanganyika kwaajili ya kupakia na kushia mizigo kwani mwalo huo umetengwa kwaajili ya shughuli za kuuzia samaki.

Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alisema hayo jana wakati akiwa katika ziara ya kikai wilayani Nkasi na kukuta katika mwalo wa Kirando unatumika kama bandari ambapo malori yalikuwa yakipakua na kupakia mizigo kwa lengo la kusafisirisha  kuipeleka kwenye visiwa vilivyopo ziwa Tanganyika.

Alisema kuwa wananchi wasipotoshe lengo la kutebnwa kwa  mwalo huo ambayo ni kwaajili ya kuuza na kununua samaki wavuliwao kwenye ziwa Tanganyika na si  kwaajili ya magari kupakilia mizigo.

,“Lengo la Mwalo huu ni kuuzia samaki na dagaa lakini naona mizigo hii, imegeuzwa kuwa bandari, narudia nimarufuku kupakilia mizigo katika mwalo huu kwani hapa ni  sehemu ya kuuzia mazao yatokanayo na ziwa na si vinginevyo" alisema

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa sehemu iliyotengwa ikitumika kama bandari haiko vizuri basi waone namna ya kuboresha ili sehemu hiyo ilirudi kama ilivyokuwa na sio kuikimbia na kuiacha kama ilivyo jwani kukimbia tatizo sio suluhisho bali kupambana na changamoto zilizopo na kuboresha.

Awali kabla ya Kukaribishwa Mkuu wa Mkoa, Mbunge wa Nkasi Kaskazini Ali Kessy alikemea vitendo vya wananchi wa Kirando kutumia mwalo huo kama bandari jambo ambalo ni kinyume na sheria na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.

“Nawaomba ndugu zangu kuanzia sasa hii  sio bandari na haipo chini ya TPA, bandari ni ile ya zamani na iendelee kutumika ile ile na hapa tuwaachie wavuvi"alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Said Mtanda aliwaasa wananchi wanaotumia vyombo usafiri ziwani kuzingatia kuvaa maboya na kuonya kutozidisha mizigo na abiria na kuwasisitiza wasafiri wa majini kuwa watumiaji wawe wantoa taarifa endapo wataona taratibu zinakiukwa kwakuwa wasafirishaji hao huangalia faida kuliko usalama wa maisha ya abiria wao. 

Mwisho

Sunday 7 January 2018

Nkasi washauriwa kuanzisha shule mpya

Na Gurian Adolf
Nkasi
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Joachim Wangabo ameishauri Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi  kuanzisha shule mpya za Sekondari ambazo zitapokea wanafunzi wa kuanzia kidato cha Kwanza mpaka cha nne kuliko kuendelea kuwapangia wanafunzi waliofaulu katika shule zilizo jaa na ambazo zinawanafunzi kuanzia kidato cha Kwanza mpaka cha sita.
Ushauri huo ameutoa Jana wakati akishiriki songambele ya ujenzi wa madarasa nane ya Shule ya Sekondari Kirando yanayotarajiwa kutumiwa na wanafunzi 422 waliofaulu kuanza kidato cha kwanza kwa mwaka 2018 katika shule hiyo inayobeba wanafunzi kutoka katika kata mbili zilizopo wilayani humo.
Alisema ili kuleta uwiano wa waalimu katika shule hizo unaoendana na idadi ya wanafunzi ambao wanatarajiwa kuongezeka kila mwaka mpya wa masomo nivizuri  halmashauri hiyo ikaanzisha shule mpya kwani hivi sasa wanafunzi wanafaulu kwa wingi na wanapangiwa katika Shule zile zile kongwe zenye vyumba vile vile vya madarasa na idadi ile ile ya walimu. 
“tunapoangalia kutatua changamoto ya shule hii ya Kirando Sekondari tuangalie ufumbuzi wa kudumu , nawashauri muangalie uwezekano wa kujenga shule nyingine, huo ndio utakuwa ufumbuzi, shule hii ina O – level na A – level, sasa kama kutakuwa na shule nyingine ya O – level peke yake, ili shule hii muipunguzie mzigo wa kuchukua wanafunzi wengi na walimu wengi katika shule moja kwani hivi sasa imeelemewa”
Aidha alisema  kuwa kwa eneo la ekari 60 linalomilikiwa na shule hiyo ya Sekondari ya Kirando lingetengwa walau ekari 20 kwaajili ya ujenzi wa shule  mpya jambo litakalopelekea kupewa walimu wapya kwaajili ya shule mpya na kuleta uwiano wa walimu kuliko hali ilivyo sasa wote kujazana katika Shule moja. 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Said Mtanda alisema ameupokea ushauri huo wa mkuu wa mkoa hayo na kuahidi kuufanyia kazi kuanzia ngazi ya Kijiji hadi halmashauri ya Wilaya na kuongeza kuwa suala hilo litawekwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019 na kuongeza kuwa wananfunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza lazima wapate nafasi ya kusoma.
“wanafunzi waliofaulu kuanza kidato cha kwanza katika shule hii ya Kirando ni 422 na tumekubaliana kuwa hadi kufungua shule wananfunzi wote wanatakiwa wawe madarasani, lakini tumekubaliana pia na wazazi kuwa kama serikali tutanunua meza zote 422, na tumewahamasisha kuchangia walau mchango wa kiti ili mwanafunzi anapokuja akute meza na kiti ili tulimalize jambo hilo,”
Awali mkuu wa Shule ya Sekondari kirando Erneo Mgina akitoa taarifa  ya shule hiyo alisema kuwa shule ina wanafunzi 677 na kutaraji kupokea wanafunzi 422 na inakabiliwa na upungufu wa madara vyumba vinne ambayo vitatu tayari na vingine vipo katika hatua ya msingi na wanatarajia kurekebisha vyumba vingine vitatu vya maabara ili wanafunzi wavitumie Kama madarasa kwa muda.
Hayo yote yanafanika  ikiwa ni utekelezaji wa agizo la waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa, TAMISEMI kuitaka mikoa iliyokuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2018 ukiwemo mkoa wa Rukwa kuhakikisha  wanafunzi wote wanapata madarasa ya kusomea, madawati na vyoo pale shule zitakapofunguliwa januari 8.
Mwisho

Cwt yampongeza rais Magufuli

Na Gurian Adolf
Kalambo

CHAMA cha Walimu CWT wilayani Kalambo mkoani Rukwa kimepongeza hatau ya rais John Magufuli kutangaza kutoa fedha kiasi cha bilioni 200 kwaajili ya kulipa madeni mbalimbali ya ndani yakiwemo ya walimu.

Pongezi hizo zilitolewa jana na katibu wa chama hicho Peter Simwanza alipokuwa akizungumza na gazeti hili lililotaka kujua wanachama wa chama hicho wamepokeaje ahadi hiyo ya rais.

Alisema kuwa hatua ya serikali kuamua kulipa madeni yaliyokwisha hakikiwa ikiwemo ya walimu italeta moyo wakuongeza juhudi katika utendaji kazi kwani kilikuwa ni kilio cha muda mrefu cha Walimu wa wilaya hiyo. 

Simwanza alisema kuwa tangu walimu walipomsikia raisi akitangaza ahadi hiyo kupitia vyombo vya habari wamekuwa na morali wa kufanya kazi kwakua wanaamini serikali itawalipa fedha hizo ambazo walikuwa wakizisubiri kwamuda mrefu.

Aidha katibu huyo wa CWT wilaya ya Kalambo aliwataka walimu kuendelea kufanya kazi kwa weledi ili kuongeza ufaulu na kuleta tija katika wilaya ya Kalambo na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla. 

 Mwaka jana  walimu nchini walitishia kuitisha kugoma kwa kile walichodai kuwa ni njia ya kuishinikiza serikali ili ilipe madeni yao kwani yamekuwa ni ya muda mrefu na yanasababisha walimu kuvunjika moyo katika kufanya kazi.

Hata hivyo walimu wilayani humo walitumia fursa hiyo kumuomba raisi John Magufuli afanye uamuzi wa kuwapandisha madaraja watumishi wa umma sambamba na kuwaongeza mishahara. 

Mwisho
 

Mbolea bado changamoto

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
KUNA kila dalili huenda mkoa wa Rukwa ukakabiliwa na baa la njaa mwaka huu baada ya  mawakala wa pembejeo kuweka mgomo baada ya serikali kupanga bei elekezi kwamadai kuwa bei iliyopangwa haiwapi faida.

Hayo yamebainika katika kikao cha kutafuta suluhu la upatikanaji wa mbolea mkoani humo baada ya kuwepo taarifa zakuwa Kuna uhaba wa upatikanaji wa mbolea  hasa katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo ambapo asilimia 80 ya wananchi wa mkoa wa huo wanategemea kilimo kujipatia kipato
Katika kikao hicho kilichoongozwa na mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo ilibainika kuwa baadhi ya mawakala wamesusia kuleta mbolea wakidai kuwa bei elekezi ya shilingi 55,000 kwa mfuko wa kilogram 50 hawapati faida kwani gharama za usafirishaji zako juu. 
Katika kikao hicho mkuu wamkoa alisema  kuwa Serikali kupitia Wizara ya kilimo ilichukua hatua za makusudi kubadili mfumo wa ruzuku uliokuwa ukiwafaidisha wakulima wachache kupitia vocha za pembejeo na kuamua kupitia mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) iliweka mfumo wa uuzaji na usambazaji wa mbolea kwa uagizaji wa pamoja na kutoa bei elekezi kwa kila Halmashauri.
Alisema kuwa hali ya upatikanaji wa mbolea mkoani Rukwa si ya kurudhisha na alibainisha kuwa hadi kufikia tarehe januari 3 mkoa ulikuwa umepokea mbolea ya kupandia (DAP) tani 3,746.6 kati ya tani 47,869 zinazohitajika na upungufu ukiwa ni tani 44,122.9 na mbolea ya kukuzia (UREA) tani 2,599.6 kati ya mahitaji ya tani 49,669 na  upungufu ukiwa ni tani 47,069.4.

Katika kikao hicho mkuu huyo wa mkoa aliwataka mawakala wa mbolea kuhakikisha wanaagiza mbolea ya kutosha kutoka nje ya mkoa ili wawasambazie wauzaji wadogowadogo waweze kukuuza mbolea hiyo katika vijiji vya halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa ili wakulima wapate mbolea.
Mmoja wa mawakala wa usambazaji wa mbolea mkoani humo na mmiliki wa Kampuni ya usambazaji ya Ikuwo General Enterprises Sadrick Malila alisema kuwa upungufu mkubwa uliopo ni katika upatikanaji wa mbolea ya kukuzia (UREA) na si mbolea ya kupandia (DAP) ambayo mpaka sasa katika ghala lake yeye binafsi ana tani 200 hivyo aliiomba serikali ya mkoa kuongeza shilingi 1000 katika bei elekezi ili kufidia gharama za usafirishaji wa mbolea hizo.
Naye mmoja wa wakulima aliyehudhuria kikao hicho Godfrey John aliiomba serikali ya mkoa huo kwa kushirikiana na mawakala hao kuongeza kasi ya upatikanaji wa mbolea ili kunusuru maisha ya wanarukwa wanaotegemea kilimo kujikimu kimaisha.
Katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2016/2017 mkoa huo ulilima hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602 na  Kwa msimu huu wa Kilimo wa mwaka 2017/18 mkoa  umelenga kulima jumla ya hekta 554,310.6 na unatarajia kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula iwapo changamoto hizo zitatatuliwa.

Mwisho


Mkaguzi wa ndani apewa jukumu

Na Gurian Adolf
Nkasi
SERIKALI wilayani Nkasi mkoani Rukwa imemuagiza mkaguzi wa hesabu za ndani afanye ukaguzi katika michango ya maendeleo  ya wananchi ili kujiridhisha Kama michango yote inatumika Kama ilivyokusudiwa. 

Mkuu wa wilaya ya Nkasi Said Mtanda aliyasema  hayo jana wakati akiongoza Songambele ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika sekondari ya Kirando iliyomo wilayani humo.

Alisema kuwa hivi sasa serikali haina mzaha katika suala la fedha za wananchi na nilazima ijue kila shilingi iliyotolewa kwaajili ya maendeleo inatumika Kama ilivyo kusudiwa.


"nimemuaziza mkaguzi wa hesabu za ndani akague fedha zilizokusanywa kutoka kwa wananchi kwaajili ya shughuli za maendeleo Kama tulivyokubaliana ili tujiridhishe kama ni sahihi, na iwapo kuna yoyote atakuwa amekwenda tofauti lazima sheria ichukue mkondo wake, tunataka kila mwananchi fedha yake ionekane imefanya shughuli gani ya maendeleo" alisema

Alisema kuwa kwa watendaji wenye tamaa na michango ya wananchi waondoke wilayani mimesema hayo leo mkuu wa wilayani Nkasi kwani hakuwafai wakatafute sehemu nyingine watakapovumiliwa.

Mkuu huyo wa wilaya aliwasihi wananchi wawilaya hiyo kujitoa Kwa hali na mali na wanapaswa kutambua kuwa maendeleo ya wilaya hiyo yatatokana na juhudi zao wasisubiri mgeni kutoka nje ndio awafanyie maendeleo kwani wilaya hiyo imejaliwa kila kitu. 

Alisema ili iweze kupiga hatua nilazima wawekeze kwenye elimu kwani duniani pote maendeleo yanaletwa nawatu wenye elimu hivyo sualala la elimu lazima liwe kipaumbele chao namba moja ndipo watafanikiwa.

Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwasihi wananchi kutunza mazingira kwakua maendeleo na mazingira ni vitu pacha wajitahidi kufuga kwa Kuzingatia eneo la malisho sambamba na kufanya Kilimo endelevu ili ardhi itumike muda mrefu kwani wasipo zingatia hayo watajuta siku zijazo.

Naye mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo aliyeshiriki songambele hiyo aliwasihi wananchi kufanya kazi wasitegemee wahisani kutoka nje ya wilaya hiyo kwani zama hizo zimepitwa na wakati. 

Nao wananchi wa wilaya hiyo waliwaomba viongozi wa serikali kuwa nao bega kwa bega kwani wanachohitaji ni maendeleo kutokanana na wilaya yao kuwa nafursa nyingi hivyo nijukumu lao kuwaongoza vizuri. 

Mwisho