Sunday 7 January 2018

Nkasi washauriwa kuanzisha shule mpya

Na Gurian Adolf
Nkasi
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa  Joachim Wangabo ameishauri Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi  kuanzisha shule mpya za Sekondari ambazo zitapokea wanafunzi wa kuanzia kidato cha Kwanza mpaka cha nne kuliko kuendelea kuwapangia wanafunzi waliofaulu katika shule zilizo jaa na ambazo zinawanafunzi kuanzia kidato cha Kwanza mpaka cha sita.
Ushauri huo ameutoa Jana wakati akishiriki songambele ya ujenzi wa madarasa nane ya Shule ya Sekondari Kirando yanayotarajiwa kutumiwa na wanafunzi 422 waliofaulu kuanza kidato cha kwanza kwa mwaka 2018 katika shule hiyo inayobeba wanafunzi kutoka katika kata mbili zilizopo wilayani humo.
Alisema ili kuleta uwiano wa waalimu katika shule hizo unaoendana na idadi ya wanafunzi ambao wanatarajiwa kuongezeka kila mwaka mpya wa masomo nivizuri  halmashauri hiyo ikaanzisha shule mpya kwani hivi sasa wanafunzi wanafaulu kwa wingi na wanapangiwa katika Shule zile zile kongwe zenye vyumba vile vile vya madarasa na idadi ile ile ya walimu. 
“tunapoangalia kutatua changamoto ya shule hii ya Kirando Sekondari tuangalie ufumbuzi wa kudumu , nawashauri muangalie uwezekano wa kujenga shule nyingine, huo ndio utakuwa ufumbuzi, shule hii ina O – level na A – level, sasa kama kutakuwa na shule nyingine ya O – level peke yake, ili shule hii muipunguzie mzigo wa kuchukua wanafunzi wengi na walimu wengi katika shule moja kwani hivi sasa imeelemewa”
Aidha alisema  kuwa kwa eneo la ekari 60 linalomilikiwa na shule hiyo ya Sekondari ya Kirando lingetengwa walau ekari 20 kwaajili ya ujenzi wa shule  mpya jambo litakalopelekea kupewa walimu wapya kwaajili ya shule mpya na kuleta uwiano wa walimu kuliko hali ilivyo sasa wote kujazana katika Shule moja. 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Said Mtanda alisema ameupokea ushauri huo wa mkuu wa mkoa hayo na kuahidi kuufanyia kazi kuanzia ngazi ya Kijiji hadi halmashauri ya Wilaya na kuongeza kuwa suala hilo litawekwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019 na kuongeza kuwa wananfunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza lazima wapate nafasi ya kusoma.
“wanafunzi waliofaulu kuanza kidato cha kwanza katika shule hii ya Kirando ni 422 na tumekubaliana kuwa hadi kufungua shule wananfunzi wote wanatakiwa wawe madarasani, lakini tumekubaliana pia na wazazi kuwa kama serikali tutanunua meza zote 422, na tumewahamasisha kuchangia walau mchango wa kiti ili mwanafunzi anapokuja akute meza na kiti ili tulimalize jambo hilo,”
Awali mkuu wa Shule ya Sekondari kirando Erneo Mgina akitoa taarifa  ya shule hiyo alisema kuwa shule ina wanafunzi 677 na kutaraji kupokea wanafunzi 422 na inakabiliwa na upungufu wa madara vyumba vinne ambayo vitatu tayari na vingine vipo katika hatua ya msingi na wanatarajia kurekebisha vyumba vingine vitatu vya maabara ili wanafunzi wavitumie Kama madarasa kwa muda.
Hayo yote yanafanika  ikiwa ni utekelezaji wa agizo la waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa, TAMISEMI kuitaka mikoa iliyokuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2018 ukiwemo mkoa wa Rukwa kuhakikisha  wanafunzi wote wanapata madarasa ya kusomea, madawati na vyoo pale shule zitakapofunguliwa januari 8.
Mwisho

No comments:

Post a Comment