Friday 25 July 2014

Wazazi Sumbawanga mkoani Rukwa waomba kucharazwa mboko na walimu

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga.

Baadhi ya wazazi katika kata ya Lusaka wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamemuomba kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Chrispine Mrwanda kupeleka ombi lao kwenye baraza la madiwani ili lipitishe kuwa sheria ambayo itawapa uwezo walimu wa kuwacharaza viboko baadhi ya wazazi wasiowatimizia mahitaji ya elimu watoto wao.

Ombi hilo walilitoa jana katika viwanja vya serikali ya kijiji hicho ambapo Idara ya elimu halmashauri hiyo ilikuwa ikifanya ziara yenye lengo kuboresha ufaulu katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni utekelezaji wa sera ya matokeo makubwa sasa (BRN) katika halmashauri hiyo.

Mmoja wa wazazi hao Datus Seleman alimuomba kaimu mkurugenzi huyo kupokea ombi kutoka kwa wazazi wa kata hiyo kuliomba baraza la madiwani kuanziasha sheria ndogo itakayo waruhusu walimu kuanza kuwachapa viboko wazazi wote ambao hawawatimizii watoto wao mahitaji ya elimu.

Alisema kuwa wapo baadhi ya wazazi wamekuwa hawajali kuhusu watoto wao kama wanakwenda hata shuleni ikiwa ni pamoja na kuwanunulia sare za shule, madaftari na michango mbalimbali kitu ambacho kinapaswa kuwa ni kosa la kisheria.

Naye bi Maria Maivune alisema kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakitumia pesa zao kwa kunywa pombe na kuoa wanawake wengi na hivyo kushindwa kuwahudumia watoto wao.

"nadhani kama wazazi hao wangekuwa wanacharazwa viboko na walimu labda wanaweza kubadirika kutokana na aibu ya kuchapwa huenda wakaanza kuwajali watoto wao".....alisema.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi Mlwanda alisema kuwa halmashauri itakachopaswa kufanya ni kuwabana wazazi hao ili waweze kutimiza wajibu wao wakuwapa mahitaji wanafunzui hao ili malengo ya BRN yaweze kutekelezeka katika Halmashauri hiyo.

Mwisho.

Mvuta bangi anusurika kwenda jela miaka miwili

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

MUUZA JI wa dawa  za kulevya  aina ya bangi , Ferdinand Makundi (40)
amenusurika  kwenda jela miaka  miwili jela  baada kulipa
faini  ya Sh 100,000- kwa kosa la kukutwa  na  kilo mbili  za bangi.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama  ya Wilaya  ya Nkasi , mkoani Rukwa ,
Ramadhani Rugemalira  alimuhukumu  mshtakiwa huyo  ambaye ni mkazi wa
kijiji cha Mkole  wilayani  humo  kutumikia miaka miwili jela  au
kulipa  faini ya Sh 100,000-  baada ya kukiri kosa lake  mbele ya
mahakama hiyo .

Hata  hivyo mahakama  hiyo ilimwachia  mshtakiwa  huyo  baada ya
kulipa faini  hiyo  mahamani hapo .

Mshtakiwa  huyo  alikiri  kosa lake  hilo  baada ya Mwendesha Mashtaka
, Mkaguzi Msaidizi , Hamimu Gwelo  kumsomea  jana makosa  yake  ya
awali .

Kwa mujibu  wa Gwelo , mshtakiwa huyo  ni mzoefu  kwa  sababu aliwahi
awali  kutiwa  hatiani  na mahakama  hiyo  kwa kosa  la  kukutwa na
dawa  ya kulevya aina ya bangi  pia aliweza  kulipa faini na kuachiwa
hivyo aliiomba  mahakama impatie  adhabu kali  kwa kuwa bado
hajajifunza .

Hati  za mashtaka  mahakamani hapo  zinaonesha kuwa mshtakiwa huyo
alitenda  kosa hilo Mei , 14 mwaka  huu saa saba mchana  akiwa
nyumbani kwake  kijijini Mkole .
Alipotakiwa  kujitetea , mshtakiwa  aliiomba mahakama  hiyo impunguzie
adhabu  kwa kuwa  ana watoto  kumi na  mke  wanaomtegemea .
Mwisho