Monday 31 July 2017

madiwani wamtaka mkurugenzi kuto ogopa

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MADIWANI wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamemtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa hiyo kuto ogopa kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji hata kuwafikisha mahakamani kwamadai kuwa wakishinda kesi halmashauri hiyo itawalipa fidia. 
Akizungumza katika baraza maalumu la madiwani jana likiloketi kwa lengo la kujibu hoja za mkaguzi mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali CAG mmoja wa wajumbe wa baraza hilo Vitalis Ulaya alisema kuwa yapo baadhi ya mambo ambayo yanafanywa kwa makosa kwa makusudi kwakuwa wanajua kuwa hawawezi kufikishwa mahakamani. 
Alisema kuwa utakuta katika baadhi ya malipo yanafanyika bila stakabadhi ama kutumia mashine za EFDs huku watendaji hao wakijua kuwa ni makosa lakini katika hali ambayo ni yakustaajabisha wamekuwa wakifanya hivyo. 
Ulaya alisema kuwa kitendo hicho kamwe hakivumiliki kuona halmashauri hiyo inapata hati ya mashaka kwani kwa upande wa madiwani wamechoka na hawako tayari kuona watendaji wakiwaangusha.
Alisema kuwa baadhi ya vitendo vinaonesha wazi kuwa wapo watendaji ambao wapo kwaajili ya kuchuma fedha za wananchi na wamekuwa wakiishia kuonywa kwa barua bila kufikishwa katika vyombo vya sheria kitu ambacho sio sawa. 
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa alisema kuwa watendaji ambao wapo ndani ya uwezo wao wawachukulie hatua kwani hata wakihamishiwa sehemu nyingine watakwenda kufanya mambo ya hovyo kama hayo. 
"ndugu zangu hakuna cha kuhamisha mtumishi hapa, bali kwawale ambao wapo ndani ya uwezo wetu tuwawajibishe maana hakuna halmashauri ambayo ipo tayari kupokea mtumishi wa hovyo ambaye amesababisha matatizo katika halmashauri nyingine" alisema Malisawa.
Awali mkaguzi mkazi wa ndani John Nalambwa aliwasilisha hoja 60 zenye utata ambapo hoja tatu ndizo zilizosababisha halmashauri hiyo kupata hati ya mashaka. 
Alisema kuwa hoja hizo zimetokana na ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2015 hadi 2016 hivyo aliwataka madiwani pamoja na watendaji kuhakikisha kuwa suala hilo halijitojezi tena kwani si jambo jema kwa halmashauri Kupata hati yenye mashaka. 
Mwisho

Sikaungu bado walilia ardhi kwaajili ya mashamba na kujenga

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAKAZI wa kijiji cha Sikaungu wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamelalamikiwa kitendo cha askari magereza wa gereza la Moro wakiwa na wafungwa kuwavamia na kuwatishia kwa kupiga risasi hewani wakidai kuwa wameingia na kuchungia ng'ombe katika eneo la gereza hilo. 

Tukio hilo lilitokea julai 28 majira ya saa 8 mchana baada ya wachunga ng'ombe hao kuwa wanachunga katika maeneo ya kijiji chao ambacho kinapakana na eneo la gereza hilo. 

Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa kijiji hicho William Khamsini alisema kuwa baadhi ya vijana walikuwa wakichunga ng'ombe wa familia ndipo waliposhangaa kuona askari magereza wanne wakiwa na wafungwa wanane wakiwa wamewazunguka na kuanza kuswaga ng'ombe wakidai kuwa wanachungia katika eneo la gereza hilo. 

Baada ya kitendo hicho vijana waliokuwa wamachunga mifugo hiyo walipiga kelele za kuomba msaada ambapo wananchi wengine walikwenda kuwasaidia na kisha kuibuka mzozo mkubwa baina ya wananchi hao na askari magereza pamoja na wafungwa. 

Kutokana na hali hiyo askari magereza hao walilazimika kupiga risasi hewani lakini wananchi hao hawakuogopa mpaka walipofanikiwa kuondoka na ng'ombe wao na askari polisi hao pia wakiwa na wafungwa waliondoka zao. 

Khamsini alisema kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo Kutoelewana baina ya wananchi hao na watumishi wa gareza hilo ambapo wananchi wamekuwa wakituhumiwa kuvamia eneo la gereza hilo na kuchungia mifugo yao kutokana na kijiji hicho kukosa ardhi ya kutosha kwakua eneo kubwa la kijiji hicho lipo katika shamba la Malonje linalomilikiwa na taasisi na gereza hilo pamoja na taasisi ya EFATA Ministry ambapo analimiliki kama mwekezaji. 

Kutokana na hali hiyo wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakikutana na changamoto ya kupigwa na kujeruhiwa pindi wanapoingia kuchunga ama kupita katika upande wa mwekezaji huyo ama upande wa eneo la magereza hali ambayo mwenyekiti wa kijiji hicho aliiomba serikali ya awamu ya tano kushughurikia suala hilo kwani limekuwa likisababisha kero kubwa kwa wananchi hao kwakua hawana eneo maeneo ya kulima, kuchungia mifugo pamoja kujenga nyumba za kuishi. 

Alisema kuwa wameamua kumuandikia barua mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelote Steven ili awasaidie na kama suala hilo ataona liko nje ya uwezo wake alifikishe kwa raisi aweze kuwatatulia kero zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ardhi ya kulima na kujenga kwani imekuwa niyamuda mrefu. 

Hata hivyo kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa hawezi kuzungumzia chochote kwakuwa tukio hilo halijaripotiwa polisi,na alitoa wito kwa wananchi kuwa na tabia ya kutoa taarifa ya matukio yoyote yanayotokea. 

Mwisho

Manyanya aagiza wanafunzi wenye ulemavu wajengewe vyoo kwenye mabweni

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Naibu Waziri wa Elimu Mhandisi Stella Manyanya amemuagiza msimamizi wa ukarabati wa shule ya Sekondari Kantalamba kuhakikisha kuwa walemavu wanajengewa vyoo vyao ndani ya mabweni wanamolala ili kuepuka kuwaamsha wenzao usiku pindi wanapotaka kwenda kujisaidia. 
Ametoa agizo hilo jana muda mfupi baada ya kufanya ukaguzi wa ukarabati wa shule hiyo iliyopo Wilayani Sumbawanga iliyopewa Shilingi Bilioni 1.1 ikiwa ni mpango wa serikali wa kuzirudishia hadhi shule kongwe nchini huku shule hiyo ikiwa imejengwa tangu 1964 na haijawahi kufanyiwa ukarabati. 
“Lazima muhakikishe kwamba Mnakuwa na vyumba maalum kwaajili ya wanafunzi wenye ulemavu na kuwawekea miundombinu hasa kwa wale wenye  ulemavu ambao mazingira yao ni magumu Zaidi, kwa mfano mwanafunzi ana ulemavu wa miguu na anatakiwa kwenda kujisaidia hapaswi kutambaa kwenye mikojo ya wanafunzi wenziwe hii inawapelea wao kuwa katika mazingira hatarishi zaidi,” Alisema.
Mbali na agizo hilo pia Mhandisi Manyanya ametoa wiki tatu ukarabati wa shule hiyo uwe umekamilika  kwani muda waliopangiwa ulikwishamalizika huku kipaumebele kikiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo yao katika hali ya utulivu.
“Sijaridhishwa na kasi ya ukarabati huu hivyo tumewaongezea wiki tatu mhakikishe mnamaliza ili wanafunzi waendelee na masomo maana yake kama mngekuwa hamwezi kumaliza kwa wakati kwanini msingesema mapema,” Alihoji
Aidha alipokuwa anakagua bwalo la kulia chakula wanafunzi aliagiza kutanuliwa kwa bwalo hilo baada ya kuona kuwa bwalo hilo ni dogo na wanafunzi ni wengi kiasi ambacho ingewabidi wanafunzi hao kula kwa zamu ili wote waweze kulitumia bwalo hilo na kuongeza kuwa ukarabati unaofanyika ni pamoja na utanuzi wa majengo kwani ukubwa wa jengo lililopo ni wa tangu 1964 na sasa ni 2017 hivyo haliendani na mahitaji na wakati. 
Kabla ya kumaliza ziara yake shuleni hapo aliwasisitizia wanafunzi kuwa nia ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kuwa hakuna tofauti kati ya shule za serikali na shule binafsi kuanzia huduma za majengo, elimu na vifaa vya kusomea. 
Mwisho

Magazeti ya leo


Sunday 30 July 2017

Waonywa kutofanya ujangiri

Na Gurian Adolf
Katavi
ASKARI wa hifadhi za Taifa (TANAPA)  wameonywa kutojihusisha na vitendo vya ujangili kwani wakibainika kufanya hivyo hatua kari zitachukuliwa dhidi yao kwakua wao ndio wanandhamana kubwa ya kulinda hifadhi hizo. 
Mwenyekiti wa  bodi ya Wadhamini  ya  TANAPA  Mkuu wa  Majeshi  mstaafu   Meja jenerali    George   Waitara  alitoa onyo hilo jana  kwa askari wa   Hifadhi za Taifa  wakati  alipokuwa  akifunga  mafunzo ya   askari hao wapatao 153 wa kutoka   Tanapa  na   Hifadhi ya  Ngorongoro yaliofanyika  katika  kituo  cha   mafunzo   Mlele   Mkoani   Katavi  yenye   lengo la kuwaandaa    ki  utendaji  kazi wa kutoka  mfumo wa  sasa wa kiraia na  kuwa  mfumo wa  Jeshi usu.
Alisema  zipo taarifa  za kuwepo  baadhi ya  askari wa   hifadhi za  Taifa  na wa   mapori ya   akiba  wamekuwa   sio  waaminifu  na  wamekuwa wakifanya   shughuli za  ujangili  kwenye  mapori ya   akiba  na   kwenye  hifadhi za   Taifa kitu ambacho ni makosa makubwa. 
 Aliwataka  wale  wote  wenye  tabia  hiyo  waache  mara  moja  na watakao  bainika  wajue kuwa watachukuliwa  hatua  za  kinidhamu  na  kufikishwa   Mahakamani bila kujali cheo wala wadhifa wa mtu kwani jukumu walilonalo ni kulinda hifadhi hizo. 
Mwenyekiti  huyo wa  bodi ya Tanapa   alifafanua  kuwa   kamwe huwezi kuwa   wewe  ni   askari  unae  linda  maliasili  za   nchi  na  huku  ukiwa  ni   mhalifu  wa   maliasili   za  nchi  yetu na hautavumiliwa. 
 Alisema Tanzania  ilikuwa  imekubwa  na changamoto kubwa  ya  ujangili  wa kutumia  silaha za  moto  na  hasa  za  kivita  ila kutokana  na  mafunzo waliopata   askari  kwenye  kituo cha  Mlele ya mfumo wa  jeshi usu yamesaidia  sana kupunguza ujangili wa kuua   wanyama  kama  Tembo  na   Faru  hata  hivyo  sio  kwamba    ujangili  umeisha   kabisa.
  Pia   alisema   Hifadhi za   Taifa   na  mapori ya  akiba  pia   yanakabiliwa na   changamoto  ya uingizwaji  wa  mifugo ndani ya hifadhi hivyo ni  imani  yake kuwa kupitia  mafunzo   yanayotolewa  kwenye kituo cha  Mlele   askari wa   hifadhi za   Taifa  na   wa  mapori ya   akiba wahakikishe   hifadhi  zinakuwa  salama kabisa .
  Alieleza  kuwa  kazi  kubwa   iliyombele ya  Wizara ya  Maliasili na   Utalii ni kulinda  maliasili za   nchi  ili   vizazi   vijavyo  vikute   wanyama   kama   Tembo na   Faru ambao wako hatarini kutoweka kutokana na ujangili. 
Kaimu   Mkurugenzi  Mkuu  wa hifadhi za   Taifa   Mtango  Mtahiko  alisema   mafunzo  hayo  yatawasaidia  kuwaandaa  wahitimu  kwa kuwajengea   utimamu wa  mwili  na kuwapa mbinu  za kupambana  na  ujangili.
Pia  alisema mafunzo hayo yatawaongezea   ujasiri ,kujiamini  na  hari zaidi  katika  kulinda   rasilimali za   wanyama  pori  na   maliasili kwa   ujumla  na   mpaka   sasa  askari   830 wa   Tanapa  wameisha   patiwa  mafunzo kama    hayo   katika   kituo cha   Mlele  kati ya  askari   837 walipangiwa huhudhuria  mafunzo  hayo ya  mfumo wa  jeshi usu.
Mwakilishi wa   Muhifadhi   Mkuu wa  mamlaka  ya   Ngorongoro  Izraeli   Lamon   alisema  Hifadhi ya   Ngorongoro  inakabiliwa na   changamoto ya   wanyama  kuishi na   watu  ndani ya   hifadhi.
Mkuu wa    Hifadhi wa   kituo cha  Sanane    Abeli  Mtui  alisema   mafunzo  hayo   yatawafanya  wahitimu wafanye  kazi  kwa  uadilifu   mkubwa tofauti na awali. 
Mafunzo  hayo yanafanyika kwa mara ya 14 katika  kituo cha   Mlele   tokea   Wizara ya   Maliasili na   Utalii ilipotangaza  kubadili  mfumo  wake  wa  utendaji  kazi  kwa  watumishi waliochini ya   Wizara hiyo kwa kutoka  mfumo wa sasa   wa  utendaji kazi wa kiraia  na kuwa jeshi usu   PARAMILITARY  TRANSFORMATION
Mwisho

Waacha vyandarua kuhofia kunguni

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
BAADHI ya wananchi wa naoishi katika bonde la ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wameacha kutumia vyandarua vilivyokuwa vikitolewa na serikali kupitia mradi wa hati punguzo wakidai kuwa vimesababisha kuwepo kwa kunguni katika nyumba zao. 
Wananchi hao walidai kuwa tangu kuanza kugawiwa kwa vyandarua hivyo kumekuwa na kunguni wengi tofauti na miaka ya nyuma hali iliyosababisha kuacha kutumia vyandarua hivyo. 
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Muze wilayani Sumbawanga Francis Kakole akizungumza na gazeti hili alisema kuwa wameacha kabisa kutumia vyandarua hivyo kwani tangu wameanza kuvitumia kumeibuka kunguni wengi na hivyo kusababisha kero kubwa kwa wananchi hao. 
Naye Peter Kalanda mkazi wa kambi ya wavuvi ya Kipa katika mwambao mwa ziwa Rukwa alidai kuwa hivi sasa kumekuwa na kunguni wengi katika maeneo yao na walipofanya utafiti waligundua kuwa chanzo cha kunguni hao kilikuwa baada ya kuanza kutumia vyandarua vilivyokuwa vikigawiwa bure  na serikali kwa wanawake wajawazito. 
"kabla ya kugawiwa vyandarua hivyo bonde letu lilikuwa halina kunguni lakini baada ya kugawiwa na kuanza kutumia vyandarua hivi kumeibuka kunguni hadi wamesababisha kero,ndio maana tumeamua kuacha kuvitumia kabisa."..alisema. 
Hii ilibainika baada ya mwandishi wa habari hizi kufika katika kambi ya uvuvi ya Kipa na kukuta wananchi wakiwa wanaishi bila kutumia vyandarua na wakati bonde hilo la ziwa rukwa lina mbu hali ambayo ni hatari kwa kupata ugonjwa wa malaria. 
Wananchi hao walimueleza sababu hiyo ambayo imesababisha wao waache kutumia vyandarua licha ya kuwa wapo wachache ambao wanatumia vyandarua ambavyo wamekuwa wakinunua madukani na si vile vya hati punguzo ambavyo vikigawiwa na serikali. 
Hata hivyo gazeti hili lilizungumza na Dkt Emmauel Mtika wa  hospitali ya mkoa wa Sumbawanga alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na kuongeza kuwa vyandarua hivyo vimewekewa dawa ambayo inafukuza kunguni na mbu na hivyo wanapo waona kunguni wanajua wamesababishwa na dawa hiyo. 
Alisema kuwa pia baadhi yao wamekuwa hawaumwi na mbu pindi wanapotumia vyandarua hivyo kwakua vinadawa ya kufukuza mbu na wanajikuta wamelala usingizi fofofo bila kushiriki tendo la ndoa na hivyo kusingizia kuwa vyandarua hivyo vinasababisha upungufu wa nguvu za kiume hali ambayo si kweli ni wao wanapitiwa na usingizi na wala si suala la vyandarua. 
Mwisho

Magazeti ya leo