Thursday 12 June 2014

WATUMISHI WA AFYA WATAKIWA KUHESHIMU MAADILI YA KAZI.

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

Serikali mkoani Rukwa imewaagiza watumishi wa idara ya afya mkoani humo kuzingatia maadili ya kazi hasa kwa kutovujisha siri za wateja wao pindi wanapofika kupata huduma.

Agizo hilo limetolewa na mwakilishi wa mkuu wa mkoa huo Iddy Kimanta ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Nkasi wakati akizindua kampeni za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto.

Alisema kuwa kitendo cha baadhi ya watendaji wa afya kutokuwa na siri hususani kwa watu wanaopima virusi vya ukimwi kumekuwa kukisababisha watu wengi kuacha kujitokeza kupima.

"baadhi yenu mmekuwa mkitoa siri za wateja wenu maana mtu anapima asubuhi kufikia jioni taarifa zote za vipimo vyako unavikuta mtaani" alisema.

Alisema kuwa kitendo hicho ni ukoseefu wa maadili ya kazi na kinadhoofisha kampeni mbalimbali zinazohusu masuala ya kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi.

Kwaupande wake mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa John Gurisha alisema kuwa kasi ya maambukizi mapya ya VVU inazidi kuongezeka ambapo hivi sasa imefikia kiwango cha asilimia 6.2 huku kiwango cha kitaifa ni asilimia 4.5

mwisho