Thursday 31 August 2017

Jela miaka 20 kwa kumkata mkono albino

Na Gurian Adolf
Sumbawanga. 
Mahakama kuu kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela, kila mmoja washitakiwa sita waliokutwa na hatia ya makosa ya kula njama na kujaribu kumuua mtoto mmoja ambaye mlemavu wa ngozi (Albino).

Jaji wa Mahakama hiyo, Adam Mambi akisoma hukumu hiyo alisema  mahakama imeridhishwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka uliokuwa na mashahidi 12 wakiwemo daktari na mkemia ambako kiungo hicho kilipelekwa kuchunguzwa viini saba (DNA) ili kuthibitisha kwamba kilikuwa cha mtoto huyo.

Jaji Mambi alisema mahakamani hapo kwamba watuhumiwa hao walithibitika kutenda kosa hilo katika kijiji cha Msia, wilani Sumbawanga feb 15 mwaka 2013 kwa kumvamia mtoto Mwigulu Matomange akiwa na miaka sita ambapo akichunga ng'ombe na kukata kiungo cha mkono na kutoweka nacho.

Alisema baada ya watuhumiwa hao kutoweka na kiungo hicho, walikamatwa na polisi Aprili 20 mwaka 2013 mkoani tabora wakiwa katika harakati za kutafuta mnunuzi wa kiungo hicho.

 Washitakiwa sita kati ya kumi waliofikishwa mahakamani hapo, na kukutwa na hatia katika kesi hiyo ni Ignas Sungura, James Paschal, Ibrahimu Tela, Faraja Jailos, Weda Mashilingi na Nickson Ngalamila  huku walioachiwa huru katika kesi hiyo ni Kulwa Mashilingi, Peter Said, Hamis Rashidi na James Ngalamila ambao wote walikuwa wakitetewa na mawakili wanne ambao ni Bartazar Chambi, Charles Kasuku, Peter Kamyalile na Mathias Budodi.

Jaji Mambi alisema mahakama imejielekeza katika mambo kadhaa ya msingi ili kuthibitisha makosa hayo, ambapo iliangalia ushahidi wa mazingira, kitendo cha washitakiwa kukutwa na kiungo cha binadamu wakitafuta soko na nia ovu ya washitakiwa kutenda kosa na kusababisha maumivu makali au kifo.

Aliongeza kwamba baada ya kujiridhisha katika maeneo hayo na kusikiliza utetezi wa washitakiwa, mahakama imethibitisha pasipo kuacha mashaka kwamba washitakiwa wana hatia ya makosa mawili ya kula njama ya kuua na jaribio la kutaka kumuua.

 Alisema kosa la kula njama ya kuua adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela kwa kuzingatia kifungu cha sheria 215 kanuni ya adhabu sura 16, huku kosa la kufanya jaribio la kutaka kuua adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.

Awali, wakili wa Serikali Fadhiri Mwandoloma aliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotenda makosa kama hayo.

Nao, mawakili wa upande wa utetezi waliiomba mahakama kupunguza adhabu kwa wateja wao kwa kuwa tayari wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne kitu ambacho ni funzo tosha kwao hivyo hawawezi kurudia kutenda tena makosa hayo.

Jaji Mambi katika hukumu yake alisema mahakama kwa kuangalia mazingira ya kesi na hoja za upande wa utetezi imewapunguzia adhabu washitakiwa hao kutoka kifungo cha maisha kwa kosa la pili kifungo cha miaka 20 huku kosa la kwanza wakitumikia kifungo cha miaka 14 hivyo watatakiwa kutumikia vifungo vyo kwa pamoja jela.

Mwisho.

Magazeti ya leo