Sunday 7 January 2018

Mbolea bado changamoto

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
KUNA kila dalili huenda mkoa wa Rukwa ukakabiliwa na baa la njaa mwaka huu baada ya  mawakala wa pembejeo kuweka mgomo baada ya serikali kupanga bei elekezi kwamadai kuwa bei iliyopangwa haiwapi faida.

Hayo yamebainika katika kikao cha kutafuta suluhu la upatikanaji wa mbolea mkoani humo baada ya kuwepo taarifa zakuwa Kuna uhaba wa upatikanaji wa mbolea  hasa katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo ambapo asilimia 80 ya wananchi wa mkoa wa huo wanategemea kilimo kujipatia kipato
Katika kikao hicho kilichoongozwa na mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo ilibainika kuwa baadhi ya mawakala wamesusia kuleta mbolea wakidai kuwa bei elekezi ya shilingi 55,000 kwa mfuko wa kilogram 50 hawapati faida kwani gharama za usafirishaji zako juu. 
Katika kikao hicho mkuu wamkoa alisema  kuwa Serikali kupitia Wizara ya kilimo ilichukua hatua za makusudi kubadili mfumo wa ruzuku uliokuwa ukiwafaidisha wakulima wachache kupitia vocha za pembejeo na kuamua kupitia mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) iliweka mfumo wa uuzaji na usambazaji wa mbolea kwa uagizaji wa pamoja na kutoa bei elekezi kwa kila Halmashauri.
Alisema kuwa hali ya upatikanaji wa mbolea mkoani Rukwa si ya kurudhisha na alibainisha kuwa hadi kufikia tarehe januari 3 mkoa ulikuwa umepokea mbolea ya kupandia (DAP) tani 3,746.6 kati ya tani 47,869 zinazohitajika na upungufu ukiwa ni tani 44,122.9 na mbolea ya kukuzia (UREA) tani 2,599.6 kati ya mahitaji ya tani 49,669 na  upungufu ukiwa ni tani 47,069.4.

Katika kikao hicho mkuu huyo wa mkoa aliwataka mawakala wa mbolea kuhakikisha wanaagiza mbolea ya kutosha kutoka nje ya mkoa ili wawasambazie wauzaji wadogowadogo waweze kukuuza mbolea hiyo katika vijiji vya halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa ili wakulima wapate mbolea.
Mmoja wa mawakala wa usambazaji wa mbolea mkoani humo na mmiliki wa Kampuni ya usambazaji ya Ikuwo General Enterprises Sadrick Malila alisema kuwa upungufu mkubwa uliopo ni katika upatikanaji wa mbolea ya kukuzia (UREA) na si mbolea ya kupandia (DAP) ambayo mpaka sasa katika ghala lake yeye binafsi ana tani 200 hivyo aliiomba serikali ya mkoa kuongeza shilingi 1000 katika bei elekezi ili kufidia gharama za usafirishaji wa mbolea hizo.
Naye mmoja wa wakulima aliyehudhuria kikao hicho Godfrey John aliiomba serikali ya mkoa huo kwa kushirikiana na mawakala hao kuongeza kasi ya upatikanaji wa mbolea ili kunusuru maisha ya wanarukwa wanaotegemea kilimo kujikimu kimaisha.
Katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2016/2017 mkoa huo ulilima hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602 na  Kwa msimu huu wa Kilimo wa mwaka 2017/18 mkoa  umelenga kulima jumla ya hekta 554,310.6 na unatarajia kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula iwapo changamoto hizo zitatatuliwa.

Mwisho


No comments:

Post a Comment