Saturday 30 December 2017

Madaktari lawamani

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Justine Malisawa amewalaumu madaktari na kuwataka kuacha tabia ya kuwaandikia magonjwa wasiyokuwa nayo watumishi wa umma iliwaweze kuhama vituo vya kazi kwani hali hiyo imekuwa ikichangia kutokuwa na mgawanyo mzuri wa watumishi.

Aliyabainisha hayo Jana wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2018 na kuuaga mwaka 2017 kupitia kituo  kimoja cha redio mjini Sumbawanga.

Alisema kuwa baadhi ya madaktari ambao si waaminifu wamekuwa wakishawishiwa na watumishi ili waandikie kuwa wanasumbuliwa na magonjwa ambayo haya ruhusu kuishi katika mazingira fulani,kwani hali hiyo imekuwa ikichangia kutokuwa na mgawanyo mzuri wa watumishi. 

Malisawa alisema kuwa halmashauri inapowapangia maeneo ya kazi watumishi wake baadhi yao wanakimbilia kwa madaktari na kupewa vyeti vinavyoelekeza kuwa maeneo hayo ni hayafai kwa afya ya mtumishi hivyo kulazimika kumuondoa kwakuzingatia Ushauri wa daktari ambao pengine si wakweli. 

"ninamuomba sana Mungu awajalie magonjwa yale wanayo yatamani kutokana na kwenda kwa madaktari kughushi vyeti vikionesha kuwa wanasumbuliwa na magonjwa hayo ili wasikae katika vituo walivyopangiwa" alisema

Alisema watumishi wa sekata ya afya hasa madaktari wanapaswa kutambua kuwa watoto wa vijijini pia wanahitaji watumishi bora ili waweze kupata huduma bora kwani daima watumishi wengi wamekuwa na visingizio wanapopangiwa maeneo ya pembeni ya mji ama vijijini. 

Malisawa alisema kuwa watumishi wa serikali wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuisaidia serikali ya awamu ya tano katika kuwapelekea wananchi huduma sawa bila kujali wapo vijijini ama mijini kwakua wote ni wa Tanzania.

Hata hivyo Meya huyo aliwasihi wananchi kujituma katika kazi iliwaweze kujiongezea mapato halali kwani katika serikali ya awamu hii hakuna kufanikiwa bila kufanya kazi na watambue kuwa kazi ndio kipimo cha maendeleo. 

Mwisho

Magazeti ya leo