Monday 1 January 2018

Washauriwa kuwekeza kwenye afya

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

WAKAZI mjini Sumbawanga mkoani Rukwa wameshauriwa kuacha kupeleka fedha kwa waganga wa jadi ili wawatengenezee mazindikiko wasiugue,badala yake wajiunge katika mfuko wa bima ya afya ya taifa pamoja na mfuko wa afya ya jamii CHF kwani watapata uhakika wa matibabu tofauti na mazindiko ambayo yamejaa ubabaidhaji na autapeli mkubwa.

Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa alitoa ushauri huo juzi wakati akizungumza na wakazi wa Manispaa hiyo alipokuwa akiwatakia heri ya mwaka mpya wa 2018 na kuuaga Mwaka 2017.

Alisema kuwa wapo baadhi ya wananchi wanaimani kubwa na waganga wa jadi kiasi kwamba anauwezo wa kupeleka fedha kiasi cha shilingi 200,000 ili atengenezewe zindiko asiugue lakini anaona hakuna umuhimu wa kujiunga na mfuko wa bima ya afya ambao gharama yake ni shilingi 70,800 kwa mtu mmoja kwa mwaka na mfuko wa CHF ambao ni shilingi 10,000 kwa kaya kwa mwaka atapata uhakika wa matibabu.

Malisawa alisema kuwa bado jitihada kubwa za pamoja zinahitajika kuondoa dhana hii potofu kwani asilimia kubwa ya magonjwa yanatokana na uchafu na iwapo elimu ikitolewa na kufuatwa itakua zindiko tosha na wala sio kupeleka fedha kwa waganga wajadi ambao baadhi yao ni matapeli.  

Alisema kuwa wananchi wengi hawaja jiunga na mifuko ya huduma za afya kutokana na kutopata elimu kwani uwezo wanao kwakua wanafuga kuku na wana miliki simu ambazo wanaweka salio mwaka mzima fedha ambazo ni nyingi kuliko za kulipia huduma za afya mwaka mzima.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri Aliwataka watu wenye uwelewa wawasaidie wengine ili nao waweze kunufaika na mipango mbalimbali ya serikali ambayo inaanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kukabiliana na changamoto zinazowakabili. 

Hata hivyo Malisawa aliwataka wakazi wa mji wa Sumbawanga kuyasafisha mazingira wanayoishi ilikukabiliana na magonjwa mbalimbali kwakua tabia ya kutokuwa wasafi ndiyo imekuwa chanzo kikubwa magonjwa kwa wananchi wengi.

Mmoja wa wananchi wa mji Sumbawanga Peter Kalemya Aliiomba halmashauri hiyo kuongeza  magari yakuzoa taka kwani kumekuwa na c changamoto ambapo wananchi wanakusanya taka lakini magari ya kuzoa hayatoshi. 

Mwisho

No comments:

Post a Comment