Saturday 21 December 2013

MAHAKAMA YAMWACHIA HURU ALIYEMPACHIKA MIMBA MWANAFUNZI WA DARASA LA SABA.



MAHAKAMA ya  Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi  imemuachia  huru  Gelald  Gabriel  (18)  mkazi wa mtaa wa Kawajense  aliyekuwa  mshitakiwa wa kesi ya kubaka na kumpa mimba mwanafunzi  wa  darasa la saba wa shule ya Msingi Msakila  (15)  kwa madai ya kutenda kosa  hilo akiwa na umri mdogo.



Akisoma hukumu hiyo  Hakimu  Chiganga aliieleza mahakama kuwa wakati mshitakiwa anatenda kosa hilo desemba 17 mwaka jana alikuwa na umri wa miaka 17  na kutokana na sheria namba 119  inakataza kumuhukumu kifungo  cha kwenda jela  mtu ambaye hajatimiza umri wa miaka 18.



Hakimu Chiganga alisema kuwa Mshitakiwa  kutenda kosa hilo la kumbaka na kumpa mimba  mwanafunzi huyo  nyakati za saa tatu asubuhi  nyumbani kwa mjomba wake ambapo wazazi wa msichana walikuwa wamepanga kwenye nyumba hiyo.



Mshitakiwa alidaiwa kumbaka msichana huyo baada ya kuona  kuwa  watu wote waliokuwa wanaishi kwenye nyumba hiyo  wameondoka kuelekea  kwenye  shughuli zao za kila siku.



Awali kabla ya kusoma hukumu hakimu hiyo, Hakimu Chiganga alimpa mshitakiwa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba mahakama  imwachie huru kutokana  na umri wake  kuwa mdogo wakati akitenda kosa hilo, pia  alidai kuwa  msichana huyo alikuwa akiishi na mjomba wake  ambaye alikuwa hana mke   hivyo hata huo ujauzito msichana huyo anaweza akawa alipewa na huyo mjomba wake waliokuwa wakiishi naye.



Mwendesha mashitaka mkaguzi wa Polisi,  Ally Mbwijo,  baada ya utetezi huo aliiomba mahakama  itoe adhabu kali kwa mshitakiwa kwani  umri sio kigezo cha kumfanya mshitakiwa atende kosa hilo kwa makusudi.



 Hata hivyo Hakimu huyo akisoma hukumu hiyo kwa kueleza hivyo  mshitakiwa Gelald  amenufaika na sheria hiyo hivyo  mahakama inamwachia huru na asirudie tena kutenda kosa hilo  baada ya kuachiwa huru.

CARITAS NA MAENDELEO SUMBAWANGA YATOA MSAADA



MFUKO wa Calitasi na maendeleo wa jimbo katoliki Sumbawanga  lililopo mkoani Rukwa umetoa msaada wa  mabati  40  yenye thamani ya shilingi 500,000 kwa wahanga  wa mvua kubwa ya mawe iliyonyesha katika  kijiji cha Kasense  kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani humo.

Akikabidhi msaada huo kwa serikali ya kijiji  mkurugenzi wa mfuko huo Padre  Demetrius  Kazonde alisema kuwa lengo la msaada huo ni kuwasaidia baadhi ya watu ambao nyumba zao ziliezuliwa  kabisa paa ili wazikarabati upesi na warejee katika nyumba zao waondokane na usumbufu wanaoupata.

Alisema kuwa kutokana na kuwa tukio lenye ni dharula mfuko huo ulitafuta fedha hizo kidogo na kuanza kutoa huku akiwaomba watu wenye mapenzi mema wajitolee ili kuwasaidia watanzania wenzao wali katika wakati mgumu kuliko kusubilia serikali ndiyo iwasaidie watu hao.

Katika msaada huo padre huyo alikabidhi pia fedha taslimu kiasi cha shilingi 300,000 ambazo alisema alitumwa na askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga  Damian  Kyaruzi  ambapo alisema askofu huyo alitoa fedha hizo ili ziwasaidie wahanga hao katika wakati huo mgumu walio nao.

Naye Ofisa mtendaji  wa  kijiji hicho Joseph  Nandi  alisema kuwa wameupokea msaada huo kwa mikono miwili hasa katika kipindi hiki ambacho wakazi wa kijiji hicho wapo katika wakati mgumu kutokana na wengine kubomoka kwa nyumba zao na hivyo hawana kwa kuishi.

Alisema kuwa wananchi hao wamekuwa wakisaidiana kwani baadhi waliwachukua watu ambao nyumba zao zimeharibika na kuwapa hifadhi hali iliyosababisha kugawana chakula kidogo walicho nacho na hivyo kuhitaji msaada mkubwa ili waweze kuishi katika mazingira bora zaidi.

Akishukuru wa niaba ya watu ambao nyumba zao zilibomoka kufuatia mvua hiyo  Peter  Mwanisawa alisema kuwa msaada huo umetolewa katika wakati muafaka kwani wengi wa watu ambao nyumba zao ziliboka wanahitaji msaada wa vifaa vya ujenzi kwani ukarabati wa nyumba hizo unahitaji fedha nyingi na bahati mbaya hawana fedha za kuweka kufanya ukarabati huo.
Baadhi  ya  wakazi  wa  kijiji  cha  Kasense  wakiangalia  msaada  wa  mabati  uliotolewa  na  mfuko  wa  Caritas  na  maendeleo  jimbo  Katoliki  Sumbawanga  na  kiasi  cha  fedha taslimu shilingi  300,000
zilitolewa  na  Askofu  Damian  Kyaruzi  wa  kanisa  Katoliki  jimbo la  Sumbawanga kwa  wahanga  hao  msaada  wote  huo  ulikabidhiwa  kwa  serikali ya  kijiji.

JELA MIAKA 60 KWA UNYANG'ANYI WA SILAHA.



WAKAZI wawili  wa kijiji cha Kakese  John Mwakalebene  (24)  na Kamili Lugoye  (30)  wametiwa  hatiani   na kuhukumiwa na makakama  ya wilaya ya  Mpanda mkoani Katavi   kutumikia  kifungo cha miaka 60 jela kwa pamoja  baada ya kupatikana na hatia  ya unyang’anyi wa kutumia silaha.


Hukumu hiyo ilitolewa  na Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda  baada ya mahakama kutokuwa na shaka na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na pande  mbili za mashitaka na utetezi ambapo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.



Washitakiwa hao  walidaiwa kutenda kosa hilo  la unyang’anyi hapo Julai  7 mwaka huu saa mbili  na nusu usiku kijijini hapo ambapo  walimshambulia kwa mapanga Tija Sailasi  na kisha kumpora fedha tasilimu  Tsh 430,000.



Katika tukio hilo pia walipola simu mbili zenye thamani ya shilingi laki moja vitenge  vya wax  bunda za sigara aina ya SM  na  vocha  na kufanya vitu thamani ya vitu na pesa  walivyopola  kuwa na jumla ya  Tsh  760,000


Akisoma hukumu  hiyo  Hakimu,  Chiganga  Ntengwa  baada ya kusikiliza mwenendo mzima  wa kesi mahakama  yake imewaona  washitakiwa  wamepatikana   na kosa  kwa mujibu  wa sheria  namba 287(A) ya sura ya 16 ya marekebisho ya mwaka 2009

Washitakiwa wakijitetea waliiomba mahakama hiyo iwapunguzie adhabu  kutokana na umri wao kuwa mdogo na wameoa hivi karibuni na wazazi wao wanawategemea lakini  baada ya maombi hayo, mwendesha mashitaka Mkaguzi msaidizi wa Polisi, Ally Mbwijo  alipinga vikali  na kuiomba  mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo kwani vitendo hivyo vimeshamiri sana Mkoa wa Katavi.

Friday 20 December 2013

MVUA YALETA MADHARA KIJIJI CHA KASENSE


Baadhi ya Nyumba  zilizo  bomoka  na kuezuliwa  paa  katika  kijiji  cha  Kasense  kufuatia  mvua  kubwa  ya  mawe  iliyonyesha  kwa  muda  wa  masaa  mawili.

KING'AMUZI CHA TING CHAZINDULIWA RUKWA.



KAMPUNI ya AGAPE  televisheni  imezindua na kuanza kuuza kisimbusi  chake cha aina ya  TING mkoani Rukwa ili kutoa fursa kwa wakazi wa mkoa huo kuanza kutumia teknolojia ya digitali ambapo wataweza kuona channel nyingi tofauti na kutumia teknolojia ya Analojia  ambayo haitoi fursa ya kupata chaneli nyingi kama ilivyo kwenye Digitali.

Akizindua kisimbusi  hicho kwa niaba ya mkuu wa mkoa  huo ,makamu  mwenyekiti wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga  Emmanuel  Malisawa  alisema kuwa hii ni fursa kwa wakazi wa mkoa huo kuingia katika mfumo wa digital mapema zaidi kuliko kusubiri mpaka serikali itakapo zima mitambo ya Analojia ndipo waanze kutumia visimbusi vitakavyo wawezesha kupata matangazo ya televisheni.

Alisema kuwa  mabadiliko hayo ya kiteknolojia ni fursa nzuri kwa wakazi wa mkoa huo ambao ulikuwa haupati vyombo vya habari vingi katika mfumo wa analojia lakini kwa mfumo huu mpya wakazi wake watakuwa na uamuzi wa kuchagua kuangalia televisheni wanayotaka.

Naibu meya alisema kuwa kutokana na madiliko hayo wakazi wa Rukwa wanafursa ya kujua mambo mengi ikiwemo na masuala ya kibiashara ambapo kupitia ongezeko la vyombo vya habari wataweza pia kujua bei ya vitu mbalimbali ikiwemo soko la zao la mahindi ambalo imekuwa ni tatizo kwa wakulima waliopo mkoani humo.

Kwaupande wake mkurugenzi wa  Kampuni ya Agape  Televisheni  Vennon  Fernandos wanaomiliki kisimbusi cha TING  alisema kuwa wameamua kuja mkoani Rukwa kwa nia mbili kwanza ikiwa ni kutoa fursa kwa wakazi wa mkoa huo kuingia katika mfumo wa digitali mapema zaidi ambapo watapata nafasi ya kusikia na kujifunza mambo ya watu wengine sambamba na wao kutangaza yakwao.

Alisema kuwa sababu nyingine ni kuhubiri neno la mungu kupitia chaneli za kidini zinazopatika katika kisimbusi hicho ambapo kinaongeza wigo wa kusikia neno la Mungu hata ukiwa nyumbani kwako injili itakufikia hapo ulipo.

POKEA KING'AMUZI HIKI UKATUMIE NYUMBANI KWAKO.


 
Mkurugenzi wa ATN  Televisheni  Nabii na  Askofu Veron  Fernandos  akimkabidhi kisimbusi  cha  TING mmoja wa wachungaji mkoani Rukwa wakati akizindua kisimbuzi hicho ambacho kinanasa matangazo ya Digitali mkoani Rukwa.

Thursday 19 December 2013

VIBAKA WATEMBEZA KIPIGO KATIKA BAA MBALIMBALI SUMBAWANGA



BAADHI ya wakazi wa mji wa Sumbawanga mkoani Rukwa wamelelamikia kuwepo kwa  kundi la vibaka wanaoendesha vitendo vya uvamizi katika maeneo tofauti ya kuuzia vilevi na kisha kuwatembezea kipigo watu wanaowakuta katika maeneo hayo na  kuwapora vitu mbalimbali ikiwemo fedha taslimu.

Kikundi hicho kimekuwa kikivamia katika baa zilizopo uchochoroni na kisha kuwalazimisha wateja wanao wakuta kutoa simu na fedha walizonazo na kisha kumvamia muhudumu na kuchukua fedha zote za mauzo na kuondoka nazo kuelekea kusikojulikana.

Peter  Joachim ni mmoja wa watu walivamiwa katika baa  ijulikanayo kwa jina la Lusaka Pub iliyopo mjini humo alisema kuwa wakiwa wanaendelea na burudan zao majira wa saa 5;15 za usiku lilitokea kundi la watu sita wakiwa na nondo na mapanga na kuingia ghafla ndani ya baa hiyo na kuwataka walale chini na kwa yeyote atakaye kataa kutii amri hiyo atauawa.
Alisema kutokana na silaha hizo walizokuwa nazo watu wote walilala chini na kisha vibaka hao waliwataka watoe fedha zote walizokuwa nazo pamoja na simu na kisha kuanza kuwakagua na waliporidhika kuwa hawanakitu waliondoka zao.
Katika tukio jingine lililotokea katika eneo la Wajanja Pub kundi la watu waliokuwa na mapanga, marungu na nondo walivamia katika baa hiyo ambapo walimkuta mtunza hazina wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Rukwa  na kisha kumpora fedha zaidi ya shilingi 200,000 na kuondoka nazo.
Mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Lingatsova alivamiwa akiwa mlangoni kwake na kundi la watu wasiojulikana  na kisha kumpiga nondo katika maeneo mbalimbali ya mwili wake na kisha kumpora fedha taslimu kiasi cha shilingi 250,000 pamoja na simu aina ya Sumsung Galaxy na kisha kuondoka nazo.
Baada ya kumpora  mtunza hazina huyo  vibaka hayo walivamia  katika nyumba ya mwanamke mmoja ili nako wafanye uporaji huo lakini mwanamke huyo aliwaona na kupiga kelele  ambapo vibaka hao walitimua mbio na kuelekea kusikojulikana.