Sunday 24 September 2017

CWT yamuunga mkono raisi Magufuli

Na Gurian Adolf
Kalambo
CHAMA cha walimu( CWT) wilayani Kalambo mkoani Rukwa kimeunga mkono hoja ya raisi John Magufuli kukataa wanafunzi wanaopata ujauzito shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua. 

Katibu wa chama cha walimu CWT wilayani Kalambo Peter Simwanza aliyasema hayo jana wakati akihutubia katika sherehe ya kuwaaga wanachama wa Tanzania Christian Youth Service(TYCS) wanaotarajiwa kuhitimu kidato cha nne hivi karibuni. 

Alisema Kuwa siyo busara hata kidogo kuacha wanafunzi wanaopata ujauzito mashuleni kuendelea na masomo kwani watasababisha wanafunzi wengine waone ni suala la kawaida na watakuwa wakiendekeza mapenzi shuleni na kubeba ujauzito kwakuwa wataona sio kosa.

Simwanza alisema Kuwa kitendo cha mwanafunzi kubeba ujauzito kinamuathiri kisaikolojia na hawezi kusoma vizuri katika kipindi hicho na hawezi kufanya vizuri hivyo kuchangia kuwa na maisha mabaya kwakua hawezi Kuwa muhitimu aliye elimika vizuri.

Alisema wazazi ambao wanataka mafanikio kwa watoto wao hawana budi kumuunga mkono raisi kwani hakuna lelemama Katika elimu jukumu la mwanafunzi ni kusoma na sikujihusisha na mapenzi awapo shuleni. 
 
"nitashangaa sana kama kuna mzazi atakaye mlaumu raisi Katika hilo na yupo tayari kufurahia mtoto wake akipata ujauzito, labda awe na matatizo yake binafsi lakini si kwa mzazi mwenye nia njema na maisha ya mtoto wake, na wanaojiita watetezi wahaki hizo waruhusu watoto wao wakapate ujauzito lakini sio ninyi" alisema

Cwt wilayani humo imekuwa tofauti na wanaharakati wengine wa masuala ya kielimu ambao wanapingana na msimamo huo wa raisi Magufuli wakitaka wanafunzi wanaopata ujauzito warudi kuendelea na masomo baada ya kujifungua. 

Mmoja wa waagwa hao Rea Funga alisema Kuwa wapo baadhi ya wanafunzi walioshindwa kufika kidato cha nne kwasababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito hivyo kuchezea elimu katika maisha yao. 

Kwaupande wake kaimu mkuu wa shule hiyo Audifas Mwanakulya alisema Kuwa amefarijika sana kwa hatua waliyofikia wanafunzi wake na anawatakia fanaka katika mitihani yao watakayo fanya siku chache zijazo na safari yao ya maisha watakapo hitimu kidato cha nne katika shule hiyo ya Matai Sekondari. 

Mwisho

No comments:

Post a Comment