Thursday 29 June 2017

Marufuku kuchungia mifugo ndani ya hifadhi

Na Gurian Adolf
Katavi
Wizara ya  Maliasili na  Utalii imewaonya wafugaji hapa nchini kuacha tabia yakwenda kuchungia mifugo yao katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na watambue kuwa hawataepuka mkono wa sheria iwapo watabainika wakiingiza mifugo yao humo.
Amewataka  Wahifadhi wote  kushirikiana  na  Mamlaka za  Mikoa  na  Wilaya  ili kuweza  kukabiliana  na  tatizo  la uvamizi  wa maeneo  ya  hifadhi  yanayofanywa  kwa ajili ya shughuli za kibinadamu  hususani  uvamizi wa mifugo  kwenye  maeneo ya hifadhi .
Onyo hilo limetolewa jana na  Katibu  Mkuu  wa   Wizara ya   Maliasili na  Utalii  Meja Generali  Gaudence  Milanzi alipokua  akifunga   mafunzo  ya uongozi  kwa maafisa   Wanyama  pori   yenye  lengo  la kuwafanya wafanye  kazi  kutoka  mfumo wa kiraia   na kuwa mfumo wa kijeshi yaani Jeshi usu, yaliofanyika  katika kituo cha  mafunzo   Mlele  Mkoani  Katavi .
Alisema kuwa hivi sasa  uhifadhi unakabiliwa  na tatizo  la uvamizi  unaonywa kwa shughuli za kibinadamu  hususani  uchungaji wa mifugo  kwenye  maeneo ya hifadhi baadhi ya maeneo hata binadamu kujenga na kuishi ndani ya maeneo ya uhifadhi kitendo ambacho ni kosa kisheria na kamwe hakita vumiliwa.
 Meja Jenerali huyo alisema kuwa Wizara  inatoa wito  kwa   Wahifadhi wote  na kwa kushirikiana  na  Mamlaka  za  Mikoa  na  Wilaya  husika  kulimaliza kabisa  tatizo  hilo.
  Aliwaagiza wahitimu wa  mafunzo  hayo  washirikiane na wakuu  wao  kupanga mipango  itakayo  washirikisha  wananchi  katika  kumaliza  tatizo  la uvamizi  wa mifugo  kwenye  maeneo  ya  hifadhi  na  migogoro ya mipaka   kati ya  maeneo  ya  hifadhi  na  Vijiji kwani nalo zimekuwa ni changamoto kubwa.
Milanzi  aliwaomba  wananchi  wote kuendelea  kuheshimu   sheria  za  nchi  na kuacha  kufanya  shughuli  za  kibinadamu  kwenye  maeneo ya  hifadhi  kwani watambue kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Alisema  kwa  kipindi  cha  miaka  ya  hivi  karibuni wizara ya   Maliasili na   Utalii  imeshuhudia  baadhi ya  matukio  ya mmomonyoko  mkubwa wa  maadili  hasa   kwa watumishi  wa  kada  ya   Askari  wao  wenyewe kujihusisha  na vitendo  vya  ujangili  na  mengine  mambo yasiyo faa  katika utumishi wa umma.
 Alieleza kuwa  mafunzo waliopatiwa    wahitimu  hao   anaamini kuwa  kwa  kuwa wao ndio  viongozi wakuu wa  askari  watakwenda  kusaidia  kurudisha  nidhamu kwa  askari  na watumishi  wa chini yao kwa kuwaelekeza   mambo mazuri  ya kujenga  wanayotakiwa  kuyafanya  ili kuhakikisha  kunakuwepo na uhifadhi endelevu wa maliasili  za  nchi.
Kaimu   kwaupande wake Mkurugenzi  Mkuu wa  Mamlaka ya  Wanyama  pori Tanzania   Martin  Loibooki  alisema  ulinzi wa  rasilimali  za  Wanyama  pori  umeendelea  kuimarika ndani  na  nje  ya  mapori ya  akiba na   tengefu  sambamba  na kuimarisha  ukaguzi wa  nyara  katika  maeneo  ya  mipakani  kwa kushirikiana   na wadau wengine.
  Chini  ya uongozi wa  Wizara  TAWA   imeshirikiana  na idara  ya Wanyama pori ,TANAPA  na  mamlaka  ya  hifadhi  Ngorongoro NCCA  katika  kutekeleza  kazi  mbalimbali.
Mafunzo  hayo ya  wiki sita  yaliwashirikisha  wahitimu 97 wakiwemo   Maafisa  wandamizi  20 na    maafisa wa  kati 77 wa  kutoka Mamlaka  ya  Wanyama  pori   Tanzania   TAWA.
Mwisho

Amuua rafiki yake akimdai mbao mbili

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga
MTU mmoja anayefahamika kwa jina la Fokas Pera(48)  mkazi wa kitongoji cha Ilemba B, kata ya Nankanga tarafa ya Laela wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ameuawa na rafiki yake kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni panga kichwani kwa madai kuwa alimdhurumu mbao mbili.
Tukio la  mauaji hayo kilitokea Juni 28 majira ya saa  3:00 asubuhi katika kitongoji hicho baada ya kumhadaa marehemu na kwenda naye porini ambako  yalifanyika mauaji hayo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alisema kuwa marehemu alikuwa akidaiwa mbao  mbili na rafiki yake aitwaye Paul Kayuni (50) mkazi wa kitongoji hicho ambazo anadaiwa alimpa rafiki yake huyo.
Baada ya kumdai  kwa muda mrefu Pera  alikuwa akisumbua kulipa hali iliyomkasilisha mtuhumiwa na kupanga kumpiga  kutokana na usumbufu aliokuwa  akiufanya.
Siku hiyo mtuhumiwa alimtumia rafiki zake marehemu kuwa waende porini wakamuuzie mbao naye alikubali na alipofika kule polini alimkuta mtu  anayemdai ambapo alianza kumshushia kipigo.
Akiwa anampiga marehemu naye aliamua  aanze kupigana  hali ambayo ilimfanya mtuhumiwa kuchukua panga  aliyokuwa ameficha porini na kumkata  nayo  kichwani ambapo alimsababishia jeraha kubwa lililoanza kuvuja damu nyingi.
Baada ya kuvuja damu nyingi katika jeraha hilo alianguka chini  na kupoteza fahamu ambapo walimchukua na kumkimbiza katika zahanati ya kijiji kwaajili ya matibabu.
Alipofikishwa katika zahanati ya kijiji hicho mganga wa zamu alipompokea na kumfanyia uchunguzi aliwaambia amekwisha  fariki kutokana na kuvuja damu nyingi kutokana na jeraha alilopata.
Polisi inamshikilia mtuhumiwa wa mauaji hayo na atafikishwa mahakamani pindi upelelezi wa awali utakapokuwa umekamilika.

Mwisho

Wanawake washauriwa kupata tiba za kitaalamu

Na Gurian Adolf
Sumbawanga. 
Wanaume mkoani Rukwa wametakiwa kuweka kando mifumo kandamizi ya dhidi ya wanawake hivyo waruhusu kwa wake zao wenye kusumbuliwa na maradhi mbalimbali kujitokeza na kupata tiba hospitalini pindi madaktari bingwa watakapowasili mkoani hapa.
Mkazi wa kitongoji cha Jangwani, Pendoeva Kapola alisema hayo jana wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, kuhusu ujio wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali wanaoletwa na mfuko wa bima ya afya (NHIF).
Madaktari hao wanaotibu maradhi mbalimbali wanatarajiwa kuwasili na kuanza kutoa tiba mapema juma lijalo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa iliyopo mjini Sumbawanga.
Kapola alisema kuwa wapo baadhi ya wanaume wamekuwa wakiendekeza mifumo kandamizi dhidi ya wanawake, kiasi cha kushindwa kuwapata hata ruhusu ya kutoka nyumbani kwao ili waende hospitali kupata tiba hivyo kutibiwa kienyeji hali ambayo imesababisha baadhi ya wanawake kutopata ufumbuzi wa kudumu wa maradhi yao na wakati mwingine kupoteza maisha. 
Alisema mifumo dume na mingine iliyotawala katika jamii inapaswa kuachwa mara moja ili wanawake waweze kujitokeza hospitali na kutumia fursa ya uwepo wa madaktari bingwa kupata tiba ya uhakika ya magonjwa sugu na mengineyo yanayowasumbua.
Aidha, Meneja wa NHIF, Simon Mbaga alisema ujio wa madaktari bingwa ni sehemu ya utekelezaji mpango wa mfuko huo kuyafikia maeneo ya pembezoni ili wagonjwa waweze kupata tiba kutoka kwa wataalamu hao wa afya pasipo kutembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kuwafuata.
Mbaga alisema kwamba madaktari bingwa watakaokuwepo ni wale wa magonjwa sugu ya ndani pamoja na magonjwa ya moyo, watoto, mfumo wa mkojo, pua, koo, na masikio sambamba na madaktari bingwa wa afya ya uzazi na magonjwa ya wakina mama.
Alisema kwamba wanachama wa Mfuko wa bima ya afya watatibiwa kwa kutumia kadi zao, lakini wale wasio na kadi watalazimika kulipia gharama za kawaida za hospitali.
Mwisho.

Magazeti ya leo



























Wednesday 28 June 2017

Amuua mdogo wake kwa kumpiga mpini wa jembe

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Jeshi la Polisi mkoa wa Rukwa, linamshikilia mkazi wa kijiji cha Kilida kona wilayani Sumbawanga, Japhet Kigula kwa tuhuma ya kumuua mdogo wake kwa kumpiga mpini wa jembe kichwani wakati
akimuadhibu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juni 26 nyakati za saa 12 jioni katika kijiji hicho, ambapo aliyeuawa ni Makumbi Kigula.
Taarifa zinaeleza kuwa siku mbili kabla tukio mtuhumiwa ambaye alikuwa amesafiri kutoka mkoani Mwanza alimwita mdogo wake nyumbani kwake ili waweze kufanya mazungumzo ambayo hayakuwekwa bayana lakini kijana huyo hakuweza kwenda hali ambayo ilimkera Japhet.
Inasemekana kwamba juzi nyakati za jioni saa 11 kijana huyo alikwenda nyumbani kwa kaka yake na kuanza kuongea nae ambapo mtuhumiwa
alionekana kutofurahisha na kitendo cha mdogo wake kuchelewa kuitika wito wake.
Kutokana na hali hiyo, Japhet akisaidia na mmoja wa watumishi wake wa ndani walimkamata kijana huyo na kumfunga kamba mikono na miguu kisha
kaka mtu kuanza kumuadhibu kwa kutumia mpini wa jembe ambao alimpiga nao sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani huku damu
zikimtoka puani ndipo majirani walipoingilia kati.
Baada ya majirani kuingilia kati walimkimbiza katika zahanati ya kijiji iliyopo kijijini hapo lakini ilipofika jana mchana alifariki dunia.
Polisi walifika kijijini hapo na kumkamata mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye bado anashikiliwa kwa mahojiano kabla ya kufikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Katika hatua nyingine, Polisi inamshikilia dereva Josephat Salya mkazi wa Sumbawanga mjini kwa tuhuma za kumgonga kwa gari mtoto Eliud
Steven(5) mkazi wa kijiji cha Kipundu Kala tarafa ya Namanyere wilayani Nkasi.
Tukio la  kumgonga mtoto huyo lilitokea juni 27 saa 10:05 katika kijiji hicho wakati mtoto huyo akiwa anatembea barabarani.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa George Kyando alisema kuwa dereva huyo alikuwa akiendesha  gari lenye namba za usajili T 790 DEM T aina ya Tata Truck mali ya Assif Ashraf ambapo lilimgonga mtoto huyo na kufa papo hapo.
Alisema kuwa chanzo cha ajalia ni uzembe wa dereva kushindwa kujali watumiaji wengine wa barabara na hivyo kukosa umakini awapo
barabarani.

Mwisho.

Magazeti ya leo