Thursday 31 December 2015

Waganga wajadi wachangia ujangili

Na Gurian  Adolf

KUTOKANA na kuongezeka kasi ya waganga wa jadi kutumia viungo vya wanyama pori katika kutoa tiba kumechangia kuongezeka kwa ujangili katika hifadhi ya taifa ya Katavi iliyopo mkoani Katavi.

Baadhi ya wakazi wa mkoa huo wamesema kuwa kitendo cha waganga wa jadi kutumia viungo vya wanyama hao kumesababisha watu wanaopewa masharti ya kutafuta viungo hivyo ili watibiwe kuwinda wanyama hao ili kupata vitu wanavyoagizwa na waganga hao.

Mmoja wa wakazi Hao Fransis Kashamakula akizungumza na nipashe alisema kuwa wakati mwingine wanapokwenda kutibiwa kwa waganga hao wamekuwa wakiambiwa ili wapone ni sharti wapeleke ngozi ya simba ama kwato za swala na hivyo wao kulazimika kutafuta vitu hivyo.

Alisema kuwa niwazi hakuna namna nyingine isipokuwa kuwinda mnyama huyo ili kupata mahitaji hayo ambapo kitendo hicho kinachangia kuua wanyama kutokana na kuagizwa na waganga hao wa jadi.

Alisema watu wengine ni wakulima wa tumbaku mkoani humo ambao wanaamini kuwa waganga wa jadi hutumia viungo vya wanyama hao kama kucha ngozi na vinginevyo kufanya zindiko katika mashamba yao ili wakulima wenzao wasiwaibie mazao yao shambani kwa njia za kishirikina.

Aidha imani nyingine iliyopo ni kuwa waganga hao hutumia vitu hivyo kuzuia mvua ya mawe isinyeshe kwani mvua hivyo inaponyesha shambani mawe huangukia majani ya tumbaku na kuchanika chanika na hivyo kuto faa tena hivyo waganga wamekuwa wakitumia viungo vya wanyama hao ili kufanya zindiko mvua hiyo isiharibu majani hayo ya tumbaku.

Naye Maria Kaswaya mkazi wa mkoa huo alisema kuwa pia kunabaadhi ya magonjwa ya watoto yanatibiwa na waganga hao kwa kutumia ngozi na manyoya ya wanyama hivyo hulazimika kutafuta vitu ambavyo vinaagizwa na waganga hao na hivyo kusababisha kuuawa kwa wanyama katika hifadhi hiyo.

Desemba 27 mwaka jana, mganga wa jadi aliyefahamika kwa jina la Vitus Chomba(42) mkazi wa Sumbawanga mjini mkoani Rukwa alishikiliwa na polisi wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi baada ya kukutwa na nyara za serikali ambazo alieleze kuwa huwa anazitumia wakati wa kutibu na kuroga pindi wateja wake wanapohitaji huduma hizo.

Mwisho

Majangili wanaswa, waua tembo wanne


Na Gurian  Adolf

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia watu  watatu kwa tuhuma
za kuwakamata na meno ya Tembo yenye thamani ya shilingi milioni 120
ambayo  ni sawa na Tembo wazima wanne .

Watuhumiwa hao watatu waliokamatwa na meno hayo ya Tembo  wametajwa
kuwa ni  Bathromeo Agustino(26) Geofrey Exavery(40)  na  Elias
Mwelela( 40) wakazi wa Mtaa  wa  Aitel Kata ya Uwanja wa Ndege
Manispaa ya Mpanda.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari aliwaambia
waandishi wa Habari  kuwa watuhumiwa hao walikamatwa  Desemba 29
majira ya saa 4 usiku katika Mtaa huo wa Airtel waliko kuwa wakiishi.

Alisema    Askari Polisi  na Askari wa (TANAPA)  wa  HIFADHI  ya Taifa
ya mbuga ya Katavi walipatataarifa za siri kutoka kwa Raia wema  kuwa
katika Mtaa huo kuna  watu wanamiliki  nyara za Serikali.

Kamanda Kidavashari alieleza   kuwa baada ya taarifa hizo kuwa
zimepokelewa  na ufuatiliaji  ulifanyika   katika makazi waliokuwa
wakiishi watuhumiwa hao watatu.

Alisema ndipo siku hiyo ya tukio upekuzi ulipofanyika kwenye makazi ya
watuhumiwa  na katika upekuzi huo watuhumiwa hao walikutwa na meno ya
Tembo vipande 12 vyenye thamani ya shilingi milioni 120  ambayo ni
sawa na tembo wanne hai yakiwa kwenye makazi yao.

Kidavashari aliendelea kueleza  kuwa watuhumiwa mbali ya kukamatwa na
meno hayo ya Tembo pia walikutwa na   mzani mmoja  na Pikipiki aina ya
  Sanya  yenye  Namba za usajiriT.552 CZE.

 Alisema  watuhumiwa  wanaendelea  kushikiliwa na  Jeshi la Polisi
kwa hatua za  upelelezi na watafikishwa Mahakamani  baada ya upelelezi
 utakapo kuwa umekamilika .

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi ametowa onyo kwa Wananchi kuacha
mara moja kujihusisha na biashara  za nyara za Serikali  na biashara
haramu .

Mwisho

Tuesday 29 December 2015

Apigwa radi akienda shambani

Na Gurian  Adolf

MWANAMKE  aliyefahamika kwa jina la Grace Nobert (36) mkazi wa kijiji cha Kipundukala katika mamlaka ya mji mdogo wa Namanyere  wilayani Nkasi mkoani Rukwa  amekufa papo hapo baada ya kupigwa radi.

Akizungumza na Nipashe  mume wa marehemu Anord Kaunda alisema kuwa mauti hayo yalimkuta mkewe Desemba 27 majira ya saa 9 alasiri akiwa njiani akielekea shambani.


Alisema tukio la kupigwa radi mkewe huyo  kilitokea muda mfupi baada ya kuagana na mke wake huyo aliyemuaga kuwa anakwenda shambani kupalilia maharage naye mumewe alimuaga kuwa alielekea kanisani katika ibada ya jioni.

Kabla hajafika kanisani alipigiwa simu na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho na kupewa taarifa kuwa  mkewe kafariki taarifa ambazo zilimsababishia mstuko mkubwa.

Baada ya taarifa hizo alielekea eneo la tukio na kushirikiana na majirani zake kisha walimkimbiza hospitali na walipofika madaktari waliwaeleza kuwa mwanamke huyo alifariki dunia palepale alipopigwa na radi.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho Kiliani tinga alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwa marehemu huyo alikutwa na majeraha kifuani na katika eneo la chini ya tumbo na nguo zake zilichanwachanwa na mwili wake ulikuwa mweusi kupita kiasi.

Alisema kuwa polisi walifika eneo la tukio kwalengo la  kujiridhisha kuwa kifo hicho kweli kilitokana na kupigwa  radi na si vinginevyo.

Diwani wa kata hiyo Philipo Kapembwa alisema kuwa katika maeneo hayo kumekuwepo na radi za mara kwa mara ambapo katika siku za hivi karibuni mbuzi kadhaa walikufa baada ya kupigwa na radi.

Alisema kumekuwepo na minong’ono kwa majirani  wa familia hiyo ya kuwapo kwa imani za kishirikina kufuatia tukio hilo lakini wana familia wa marehemu huyo walikataa na kuongeza kuwa kifo hicho kimetokana na mapenzi ya Mungu.

mwisho

Sangoma anaswa na Nyara za serikali

Na Gurian  Adolf

MGANGA  wa Jadi aliyefahamika kwa jina la Vitus Chomba(42) mkazi wa Sumbawanga mjini mkoani Rukwa anashikiliwa na polisi wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi baada ya kukutwa na nyara za serikali ambazo alieleze kuwa huwa anazitumia wakati wa kutibu na kuroga pindi wateja wake wanapohitaji huduma hizo.

Tukio la kukamatwa kwa tabibu huyo wa tiba mbadala lilitokea Desemba 27 majira ya saa 1;00 za jioni baada ya wakazi wa eneo alilokuwa akiishi kumtilia shaka kutokana na kukutana na watu kwa siri wakati yeye ni mgeni katika eneo hilo.

Akizungumzia tukio hilo afisa mtendaji wa kata ya Nsekwa wilayani Mlele mkoani Katavi Amos Ngozi alisema kuwa alipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa kata hiyo wakieleza kuwa kunamtu ambaye amekuwa akikutana kwa siri kubwa na baadhi ya wakazi wa kata hiyo hali iliyosababisha hofu kwa baadhi ya wananchi.

Alisema baada ya taarifa hizo alitoa taarifa polisi ambapo kwa kushirikiana na polsi hao walivamia katika nyumba anayoishi mganga huyo na kuanza kuifanyia upekuzi na katika beji lake la nguo walikuta kuna Ngozi ya simba, maini ya Swala pamoja na ngozi ya paka pori.

Mtendaji huyo wa kata alisema kuwa vitu vingine walivyomkutanavyo ni nyama ya Sungura, kwato za pundamilia pamoja na mkia wa nyati ambapo alieleza kuwa yeye ni mganga wa jadi na huwa anatumia vitu hivyo wakati wa kutibu ama kuroga kutokana na huduma anayohitaji mteja wake.

Alisema mganga huyo alifika katika kijiji cha Inyonga wilayani humo kwalengo la kufuata wateja wake ambao walikuwa wamemuita awatibu na kuwafanyia zindiko pia kutafuta vitu ambavyo atavitumia katika kutengeneza dawa ambazo anatumia kutibia wateja wake.

Hata hivyo mtendaji Ngozi alisema mganga huyo alichukuliwa na polisi na kushikiliwa katika kituo cha polisi kutokana na kukutwa akiwa na nyara za serikali, kosa la kufanya tiba za jadi wakati hana kibali cha kufanya kazi hiyo.

mwisho.

Saturday 26 December 2015

Noah yauwa watatu mtoni

Na Gurian  Adolf

WATU watatu  wamekufa maji  wakiwa wanatoka katika mahemezi ya sikukuu ya Krismasi baada ya gari aina ya NOA walilokuwa wamepanda  kutumbukia katika mto Kilambo wakati likiwa safarini kutoka katika kijiji cha Muze wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa likielekea katika kijiji cha  Majimoto wilayani  Mlele mkoani Katavi.

Kwamujibu wa taarifa kutoka kwa Diwani wa kata ya Muze Kalolo Joseph Ntila alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba  24 majira ya saa 4;20 usiku ambapo gari hilo likiwa na abiria saba lilipoacha njia na kutumbukia katika mto huo.

Alisema kuwa baada ya gari hilo kutumbukia mtoni baadhi ya abiria walifanya jitihada za kujiokoa ambapo walifanikiwa kutoka huku wanawake wawili na mtoto mdogo mmoja walishindwa kutoka ndani ya gari hilo na kufa maji wakiwa ndani ya gari hilo.

Diwani Ntila alisema kuwa baada ya abiria hao kutoka walijitahidi kutoa msaada kwa watu waliokuwa wamebaki ndani ya gari hilo lakini hawakufanikiwa kutokana na maji mengi na walipofanikiwa waliwatoa wakiwa wameshafariki dunia.

Alisema kuwa watu hao bado hawajafahamika majina yao lakini miili ya marehemu hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Muze kwaajili ya kusubiri kutambuliwa ili ndugu zao wakafanye maziko ya watu hao.

Aidha diwani huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga alisema kuwa barabara katika eneo hilo si nzuri hasa nyakati hizi za masika pindi mvua zinaponyesha kumekuwa na utelezi hali iliyosababisha gari hilo kuteleza na kutumbukia mtoni.

Alitoa wito kwa madereva wanaofanya safari kupitia barabara hiyo kuwa waangalifu katika nyakati hizi za masika kwani tahadhari isipochukuliwa huenda watu wakaendelea kupoteza maisha kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Mwisho.

Thursday 24 December 2015

wananchi wajutia kuipa ardhi Serikali.

Na Gurian  Adolf

SERIKALI ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi imesema kuwa  imeamua kufunga safari na kwenda kumuona waziri wa Afya ili waweze kupewa uhakika wizara yake itatoa fedha lini za kuwalipa fidia wananchi waliotoa ardhi yao ili iweze kujengwa hospitali ya wilaya hiyo kwani imekuwa ni muda mrefu hivi sasa.
Mkuu wa wilaya hiyo Issa Njiku aliwaambia wananchi wa wilaya hiyo wawe wavumilivu kwani baada ya muda mfupi watapewa majibu ambayo yatamaliza tatizo la muda mrefu la wao kudai fedha zao za fidia kutokana na kutoa ardhi ili ijengwe hospitali hiyo.

Alisema wananchi wamekuwa wakidai fedha zao ili waweze kulipwa na wanunue ardhi katika maeneo mengine ambapo wataweza kuendelea na shughuli za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na ujenzi wa nyumba bora na  za kisasa.

Njiku alisema kuwa mara kadhaa serikali ya wilaya hiyo wamekuwa wakiwasiliana na watendaji wa wizara ya afya na kupewa majibu ambayo hayawaridhishi wananchi hivyo yeye, mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na mganga mkuu wa hospitali hiyo watafunga safari kwenda wiazara ili wakaelezwe ni lini fedha hizo zitakuwa tayari.

Alisema imefika wakati wananchi wameanza kupoteza imani na viongozi hao wa wilaya inaonekana kama hawalipi uzito suala lao na wao ndiyo wanaoishi na wananchi hao na hivyo lawama zote wanazibeba wao hivyo wanajisikia vibaya.

Mmoja wa wananchi wanaodai fidia Fransis  Mikidadi alisema kuwa wamechoka kuvumilia na hawaamini kuwa viongozi wao wanalifuatilia suala lao kwa umakini kwani lingekuwa limekwisha malizika kwani serikali haiwezi ikakosa fedha za kuwalipa deni lao.

Alisema wananchi hao wanaendelea kuchangishana fedha kwaajili ya naauri ili baada ya sikukuu ya mwaka mpya wafunge safari kwenda kuonana raisi John Magufuli ili aweze kuwasaidi wapatiwe fedha hizo ama ikibidi akiisoma habari hii katika gazeti la Nipashe awasaidie kwani wanateseka na wanazidi kuwa masikini kwa ujinga wa kutoa ardhi yao na kuipa serikali inayowasumbua.

mwisho

wananchi watakiwa kutoa taarifa za polisi waharifu

Na Gurian  Adolf                                                              
                                                                
JESHI la polisi mkoani Rukwa limetoa wito kwa wakazi wa mkoa huo
kutowafichia siri watendaji wa jeshi hilo pindi wanapokuwa wakifanya
vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya kazi yao ili waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo ni pamoja na kutimuliwa kazi.

Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoani humo Allan Bukumbi
akizungumza na gazeti hili alisema kuwa huu ni wakati ambao si
wakulaumiana ila ni wakila mtu kuwajibika na hivyo kuwataka wananchi
kuacha kulalamika kuhusiana na mwenendo wa watendaji wa jeshi hilo ila
kutoa taarifa hatua ziweze kuchukuliwa.

Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika bila kutoa taarifa
kwa viongozi wa jeshi hilo na kama wanaona kunaudhaifu kwa baadhi ya
askari polisi wanachopaswa kufanya ni kutoa taarifa ili hatua
zichukuliwe.

''tunaomba wananchi wasiogope watoe taarifa kwa viongozi wa polisi
kuhusiana na tabia mbaya za askari, wanaochukua rushwa na walevi ili
tuwawajibishe kwani sisi ndiyo tunapaswa kuwa mfano wa kuigwa lazima
tuwe waadilifu''  alisema Bukumbi.

Mkuu huyo wa upelelezi wa makosa ya jinai alisema jeshi la polisi
halipo tayari kuchafuliwa na watendaji wake wasiokuwa na maadili ni
bora wakatimuliwa kwani hawafai kuwa sehemu yao kwani sifa za kuwa
mtendaji wa jeshi hilo uadilifu na utii ni sifa za msingi za jeshi
hilo.

Aidha alitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kuwa makini katika sikukuu
hizi za Krismas na Mwaka mpya kwa kuwaangalia watoto ambao wamekuwa ni
waathirika wa vitendo vibaya kutokana na wazazi wao kuendekeza starehe
na kuwaacha watoto bila uangalizi wa kutosha.

Alisema nyakati hizi za sikukuu kumekuwa na matumizi ya vilevi kupita
kiasi hali ambayo inasababisha madereva na watembea kwa miguu kupoteza
utashi wawapo barabarani na hivyo kusababisha ajali ambazo zingeweza
kuepukika.

Mwisho