Wednesday 6 June 2018

Basi laua lajeruhi

Na Israel  Mwaisaka
Nkasi

MTOTO mwenye umri wa miaka minne amefariki dunia papo hapo baada ya basi lenye Namba za usajili  T178 DHD lililokuwa likisafiri kutoka Kabwe wilayani Nkasi kuelekea mjini Sumbawanga mkoani Rukwa kuacha njia na kupindukaa huku abiria 25 wakijeruhi na tisa kati yao wakiwa ni majeruhi.

Akizungumzia tukio hilo afisa mtendaji wa kata ya Kabwe  Jofrey Kuzumbi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea mei 5 majira ya saa 12 asubuhi katika eneo la Malimba katika kata hiyo ya Kabwe.

Alisema kuwa  gari hilo lilikua limebeba  abiria 43 na waliojeruhiwa ni 25 na kati yao tisa ni mahututi na wamekimbizwa katika hospitali teule ya wilaya Nkasi huku wengine wakipelekwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha waliyoyapata.

Alisema kuwa baada ya ajali hiyo kutokea mtoto wa kike aliyefahamika kwa jina la Beatrice Nyansio (4) alifariki papo hapo huku mzazi wake akipata majeraha.

Afisa mtendaji huyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi hilo na baada ya ajali hiyo dereva wa gari hilo aliyefahamika kwa jina moja tu la Moses alikimbia na mpaka sasa haijulikani alipo.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa George Kyando alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa bado uchunguzi wa ajali hiyo  ikiwa ni pamoja na kuendelea kumsaka dereva wa gari hilo ambaye amekimbia ili aweze kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo mkabili.

mwisho

Kipindu pindu chaua 397

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
HALI ya ugonjwa wa kipindu pindu bado ni tete wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo idadi ya wagonjwa imeendelea kuongezeka ambapo hivi sasa imefikia vifo 15 na wagonjwa 397 waliougua ugonjwa huo tangu ulipolipuka tena  Mei 6 mwaka huu.
Mganga mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Fani Mussa akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema kuwa ugonjwa huo bado haujaisha na watu wamekuwa wakiendelea kuugua.
Alisema kuwa mpaka kufikia jana jumla ya watu 397 wameugua kufa na wengine kupona ambapo mpaka hivi sasa kuna wagonjwa  saba ambao bado wapo wodini wakitibiwa ugonjwa huo.
Mganga mkuu huyo alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni wananchi kutofuata kanuni bora za afya hasa kunywa maji yasiyosalama sambamba na kutojisaidia kwenye vyoo.
Alisema kuwa hivi sasa wakulima wanavuna mpunga na maji wanayotumia kwa kunywa ni ya kwenye majaruba ambayo si salama kiafya kwakuwa hayajachemshwa na baadhi yao wakijisaidia porini.
Dkt Mussa alisema kuwa idara ya afya inajitahidi kutoa elimu lakini bado wananchi hawafuati taratibu za kujikinga na ugonjwa huo licha ya kwamba sheria kali pia zinatumika lakini bado ugonjwa huo unaendelea.
Alisema katika kipindi cha November mwaka jana ugonjwa huo ulilipuka na ulidhibitiwa ilipofika mwezi March mwaka huu lakini bila matarajio ugonjwa huo ulilipuka tena mwezi mei mwaka huu na katika siku si nyingi umeua watu 15 tofauti na mwaka jana ambapo watu 7 ndiyo waliopoteza maisha.
Mwisho

Rukwa kujikita kwenye Alizeti

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

MKOA wa Rukwa umejipanga kwaajili ya kuzalisha zao la alizeti ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula unaotokea mara kwa mara hapa nchini.

Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alisema hayo hivi karibuni wakati anazungumza na balozi wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock ofisini kwake  wakati akiwasilisha ombi la ushirikiano baina ya mkoa wa Rukwa na nchi yake hali itakayo ongeza uzalishaji wa zao la alizeti mkoani humo na kupelekea kuinua kipato cha wakazi wa mkoa wa huo.

alisema kuwa Kwa mwaka 2016/2017 zililimwa hekta 47,862 za alizeti na kupatikana tani 53,470 ambayo ni chini ya kiwango kilichotakiwa kuzalishwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa kwa hekta 47,862 zikilimwa vizuri zinaweza kupatikana tani 119,655 ambayo ni ongezeko la asilimia 55.

Wangabo alisema kuwa nia ya kujikita katika kuzalisha alizeti kwa wingi ni kuzalisha mafuta ya alizeti kwa wingi, kutengeneza ajira na kuongeza viwanda ili kufikia nia ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda.

Alisema kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Tanzania inatumia Shilingi bilioni 189.6 kila mwaka kununua mafuta ya kula nje ya nchi huku ikizalisha tani 91,000 ambayo ni sawa na asilimia 40 za mafuta hayo tofauti na makadirio ya tani 200,000 hadi 300,000 ya uhitaji wa bidhaa hiyo kwa mwaka kitu ambacho mkoa wa Rukwa umeiona fursa hiyo na hivyo umejipanga kujikita katika kilimo cha alizeti vizuri.

Mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alisema kuwa mkoa unatarajia kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Faida mali ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kukuza zao la alizeti katika Mkoa wa Singida ili kuhamishia ujuzi huo katika Mkoa wa Rukwa.

Kwa upande wake balozi wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock alisema kuwa amefurahishwa sana na mikakati hiyo ya mkoa wa Rukwa kwa kuona umuhimu wa kutafuta zao mbadala la biashara katika Mkoa wa Rukwa ikiwa ni pamoja na kuinua kilimo cha mkoa na kuinua kipato cha wakulima wadogo na hatimae kuwatafutia namna ya kuongeza viwanda vidogo na kuongeza ajira.

Alisema kuwa serikali ya nchi yake ipo tayari kutoa msaada wa hali na mali ili mkoa huo uweze kufikia malengo hayo kitu cha muhimu ni kuendelea na ushirikiano ili mikakati hiyo iweze kufanikiwa na kuleta tija kwa wakulima pamoja na serikali kwa ujumla.
 
Mwisho

Saturday 2 June 2018

Wanafunzi Nkasi sasa wapeana mimba

Na Gurian Adolf
Nkasi

IMEELEZWA vitendo vya kupeana mimba baina ya wanafunzi kwa wanafunzi vimeshika kasi katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa hali inayochangia kukwamisha jitihada za kukabiliana na mimba za utotoni wilayani humo.

Hayo yalielezwa jana na hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya hiyo Ramadhan Rugemalila wakati akitoa mada katika mkutano wa siku moja wa kupitia utekelezaji wa mpango kazi wa kuanzia mradi wa kuzuia mimba za utotoni unaofadhiriwa na shirika la kimataifa la Plan International  wa mwezi Januari hadi Juni na kuandaa mpango kazi wa mwezi Julai hadi mwezi Desemba mwaka huu.

Alisema kuwa kutokana na elimu inayotolewa kwa wananchi pamoja na adhabu kali za kisheria zinazotolewa hivi sasa vitendo vya watu wazima kuwapa mimba watoto wa kike vimepungua badala yake vimeibuka vitendo vya kupeana mimba wanafunzi kwa wananfunzi.

Rugemalila alisema kuwa hivi sasa mahakani zimejaa kesi za mimba kwa wanafunzi ambazo idadi kubwa ni wanafunzi wamekuwa wakipeana mimba hali ambayo inalazimu sasa mashirika ya kutoa elimu yaelekeze nguvu mashuleni huenda mashirika yaliyopo yalijikita kutoa elimu kwa watu wazima na wakawasahau wanafunzi.

Hakimu huyo mfawidhi alisema kuwa pia changamoto nyingine iliyopo ni sheria inayotoa adhabu kwa mwanafunzi anayempa mwanafunzi wa kike ujauzito kwani haitoi adhabu kali  isipokuwa inaelekeza kupelekwa katika magereza maalumu ya watoto ambako anakwenda kuendelea na masomo hivyo kitendo hicho kinasababisha baadhi yao kuto ogopa wakati mwanafunzi wa kike anapoteza fursa ya masomo.

Alisema kuwa pia ipo chanagamoto kwa baadhi ya kesi kukosa ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani watuhumiwa ama baadhi ya mashahidi wakiwemo waadhirika wa mimba za utotoni kutofika mahakamani hali inayosababisha baadhi ya kesi kufutwa na watuhumiwa kuachiwa huru kitendo kinachosababisha wananchi kuvitupia lawama vyombo vya sharia kuwa havitendi haki.

Kwaupande wake mratibu wa mradi wa kuzuia mimba za utotoni wilayani Nkasi Frank Nestory alisema kuwa tangu mradi huo ulipoanza kutekeleza wilayani humo kumekuwa na madiliko chanya kitendo kinachoonesha jamii hiyo ilikosa elimu.

Alisema kuwa wapo baadhi ya wazazi walikuwa hawatambui kuwa kumuozesha mtoto  wake  mdogo wa kike ni kosa kisheria kwani mlolo huyo ni wakwake kwahiyo hakuna mtu anayeweza kumzuia kufanya hivyo mradi aamue yeye mwenye mtoto.

Nestory alisema kuwa ni mtumaini yake mpaka mradi huo utakapokuwa umefikia mwisho suala la mimba kwa watoto wilayani Nkasi litabaki historia kutokana na elimu wanayoitoa sambamba na nmwitikio wa wananchi katika kuunga mkono jitihada za kutokomeza ndoa za utotoni pamoja na mimba.

Mwisho