Thursday 29 March 2018

Amuua mkewe na kuzika mwili wake

Na Gurian Adolf
Katavi.
Jeshi  la  Polisi mkoani Katavi  linamshikilia mkazi  wa  Kijiji  cha  Songambele  Kata ya  Sibwesa  Tarafa ya  Karema Wilaya ya  Tanganyika  jina  lake  limehifadhiwa(45) kwa  tuhuma za kumuua mke  wake(31) kwa sababu ya wivu wa kimapenzi na  kisha mzika huku  mtoto wake mwenye  umri wa miaka tisa akishuhudia tukio.
Kamanda wa  Jeshi la  Polisi wa  mkoa  wa  Katavi   Damas   Nyanda    alisema tukio  la kupatikana  kwa  mwili  wa  marehemu  huyo lilitokea juzi majira ya saa 6;00 mchana  katika Kijiji  hicho.
Alisema  kuwa  marehemu aliuawa  na  mumewe huyo siku ya  hapo  januari 15  kwa  kupigwa na  mumewe  kwa  kutumia silaha  zajadi ambazo ni fimbo na  mpini  wa   jembe baada ya  kumtuhumu kuwa  anamahusiano wa  kimapenzi na wanaume  wengine  Kijijini  hapo.
Kamanda   Nyanda alisema kuwa wakati mtuhumiwa  huyo akitenda kosa hilo   ambalo  lilishuhudiwa  na  mtoto  wake wa kiume hadi   baba  yake  alivyo muuawa  mama  yake  na  kisha  kushimba shimo na  kumfukia ardhini.
  Baada ya kufanya mauaji  hayo  na kuzika mwili huo mtuhumiwa alirejea  nyumbani  kwake na  kuendendelea  na  shughuli  zake  kama kawaida na  alimtishia  mtoto wake  huyo  mdogo na  kumwambia   asimwambie  mtu  yeyote.
Majirani  waliokuwa  wakimfahamu  marehemu  baada ya  kuona  haonekani  Kijijini  hapo walianza kumuuliza  mtuhumiwa  mahali  alipo  mkewe  naye   alikuwa  akiwajibu kuwa  mkewe  amesafiri kwenda kwao kusalimia.
 Kamanda huyo wa polisi  alisema kuwa Jeshi la  polisi  lilipata  taarifa   ya mauaji ya  mama  huyo  hapo  machi 15 na  ndipo  lilipoanza  uchunguzi wa  tukio  hilo.
Alileza  baada ya  kufanya  uchunguzi wa kina ndipo juzi   waliweza  kumtia  mbaroni  mtuhumiwa  na   baada ya  mahojiano  alikiri  kufanya  mauaji  hayo kwa  kile alichodai kuwa  alikasirishwa na  tabia ya  mke  wake ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine kijijini  hapo  na  aliwaeleza  polisi kuwa  yuko  tayari  kwenda kuwaonyesha alipofukia mwili wa  mke  wake  baada  ya  kufanya mauaji.
Baada ya   mahojiano  hayo  hapo juzi  majira ya saa  6;00 mchana   polisi walifika  kwenye  eneo   ambalo  mtuhumiwa alikuwa  amemfukia  marehemu   mkewe na  baada ya kufukua  eneo  hilo walikuta  mwili na kuutambua kuwa ni mwili wa  mwanamke huyo na kisha kuutoa katika eneo hilo.
Kamanda   Nyanda  alisema kuwa  mwili   wa  marehemu baada ya kufukuliwa  ulichukuliwa na kupelekwa   katika   chumba  cha  kuhifadhi maiti katika  Manispaa ya  Mpanda.
Mtuhumiwa  anaendelea  kushikiliwa  na  jeshi la  polisi na  mara baada ya  upelelezi kukamilika  anatarajiwa kufikishwa  mahakamani  ili  akajibu  tuhuma zinazo  mkabili.
Mwisho

Thursday 22 March 2018

Wafanyabiashara warejeshewa fedha zao

Na Gurian Adolf
Katavi

BAADA ya serikali mkoani Katavi kutoa siku saba kwa makampuni yaliyochukua fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwaajili ya kuwauzia mashine za kulipia kodi za kielektroniki EFDs na hayakufanya hivyo,hatimaye makampuni hayo yamerudisha fedha hizo.

Akizungumza na gazeti hili katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania,mkoani Katavi Robison Bumela alisema kuwa fedha hizo zimerejeshwa kwa wafanyabiashara waliopewa risiti kwakuwa walikuwa na vidhibiti.


Alisema kuwa wafanyabiashara wachache ambao hawajarejeshewa fedha zao ni wale waliokuwa wanalipia bila kupewa risiti na hivyo kuwa vigumu katika ushahidi ili kuwabana mawakala wa makampuni ambao walichuku fedha hizo.
Aidha katibu huyo alisema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo katika matumizi ya mashine za EFDs ni mashine hizo kutotunza kumbukumbu kwa muda mrefu hali inayosababisha kumbukumbu kupotea baada ya kufutika.
Kupitia mikutano mbalimbali ya wafanyabiashara,mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga aliiagiza mamlaka ya ya mapato TRA Mkoani Katavi kuhakikisha wafanyabiashara wanarudishiwa fedha zao au wanakabidhiwa mashine EFDs ambazo walikuwa wamelipa fedha kwa mawakala kwakuwa walikuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na ofisi za TRA mkoa.
Mpaka mkuu wa mkoa huyo alipokuwa akitoa agizo hilo wafanyabiashara zaidi ya kumi walikuwa wakilalamikia kutapeliwa fedha na makampuni waliyoyalipa kwa madai kuwa yanauza mashine za EFDs lakini ilichukua miaka miwili bila kupatiwa mashine hizo.
Kwa mjibu wa wafanyabiashara Peter Mashinje mfanyabiashara wa mkoani humo alisema kuwa walikuwa wakilipia shilingi 800,000 lakini walipofanya malipo hayo na baadhi yao kupatiwa stakabadhi kimya kikawa kimetanda na hawakuelewa hatma ya fedha zao mpaka walipoamua kuieleza serikali ya mkoa huo kupitia vikao baina ya wafanyabishara na uongozi wa serikali ya mkoa.

Mwisho

Wanafunzi waugua ugonjwa wa ajabu

Na Gurian Adolf
Nkasi
WANAFUNZI wa kike wanaosoma katika Shule ya Msingi Kabwe  mwambao mwa Ziwa Tanganyika  wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanaugua ugonjwa wa ajabu ambao unawasababisha kupiga kelele hovyo kutetemeka na kisha kuanguka.

Akizungumza na gazeti hili mkuu wa Shule hiyo , Amon Kawana alisema kuwa ugonjwa huo ulianza kutokea shuleni hapo tangu mwishoni mwa mwaka jana ambapo mpaka sasa ni wanafunzi wapatao 20 wa kike pekee ndio wanaougua ugonjwa huo na kusababisha taharuki  shuleni hapo.
“Tatizo hilo  lilianza mwezi Novemba mwaka jana ambapo watoto wa kike sita waliugua ugonjwa huo wa ajabu na ukaendelea na ilipofika mwezi Februari mwaka  huu  idadi imeongezeka kufikia 20… awali wakiugua tulikuwa tunawakimbiza  katika zahanati ya kijiji kwaajili ya matibabu ambapo ilibainika kuwa ni malaria kali lakini wakitibiwa baada ya muda mfupi wanaugua tena ugonjwa huo'' alisema
''hata hivyo  sasa ikitokea mwanafunzi kuugua ugonjwa huo tunawaita wazazi au walezi wao wanakuja  na  kuwachukua,nadhani wanawapeleka kwa waganga wa jadi kwakuwa wanaamini kuwa ni mapepo'' alisema mkuu huyo wa shule.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kabwe , Richard Madeni alisema  kuwa wachungaji  na waganga wa jadi wamekuwa wakiwashughulikia  tatizo hilo  bila mafanikio yoyote.
“Hivi Serikali ya Kijiji , walimu  na diwani  tumekutana na wazee maarufu baadhi yao ni waganga wa jadi waemdai tuwapatie siku mbili wajipange watatupatia jibu kesho pia tuandae ujira wao kabisa ili wamalize tatizo hili'' alisema.
Diwani wa Viti Maalumu , Christina Simbakavu alisema kuwa  tatizo hilo  limedumu kwa  muda mrefu na sasa limekuwa kero kwa  wazazi , walimu pia wakazi  wa kijiji hicho .
Kaimu afisa elimu msingi wilayani Nkasi Mnyuke Msumeno amekiri kuwapo kwa tatizo hilo na kuwa wamemuagiza mwalimu mkuu wa shule hiyo atoe taarifa ya maandishi itakayomfikia mkurugenzi mtendaji ili waone uwezekano wa kupeleka wataalamu wa afya katika eneo hilo.
Alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa hasa kwa kuwa hutokea mara kwa mara hivyo wanaisubiri taarifa hiyo ili wataalamu wa afya waweze kwenda eneo la tukio ili waweze kuja na majibu ya tatizo lenyewe ikiwa ni pamoja na namna ya kulitatua.
Akizungumza na gazeti hili  kwa njia ya simu , Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa , Dkt Emanuel Mtika alisema kwa kuwa shule hiyo ni ya kutwa  na wasichana wanasumbuliwa  ni wenye umri chini ya miaka 16 na tayari  jitihada  kadhaa  ikiwemo wachungaji  kufanya maombezi  bila mafanikio  kuna uwezekano mkubwa  kuna mlipuko  wa ugonjwa wa malaria .
“Kijiji cha Kabwe (Nkasi ) hadi Kasanga (Kalambo ) ambavyo vipo katika ukanda  wa a mwambao mwa Ziwa Tanganyika  vimekuwa vikikumbwa na milipuko ya ugonjwa wa malaria ……wakazi wa maeneo hayo kutokana na hali ya joto  kali wamekuwa hawatumiii  vyandarua  usiku  hivyo kunauwezekano  mkubwa  kukawa na  mlipukjo wa ugonjwa wa malaria  katika kijiji cha Kabwe “ alisema Dkt Mtika .
Mwisho

Zambia yaondoa marufuku

Na Gurian Adolf
Kalambo

WAVUVI wa samaki katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameishukuru serikali ya Zambia kwa kuondoa marufuku ya biashara ya samaki katika nchi hiyo ambayo ilikuwa imewekwa kwa takribani wiki mbili kutokata na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindu pindu nchini humo.
Shukrani hizo wamezitoa jana wakati wakizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili ambapo walisema kuwa marufuku hiyo ilikuwa imewaathiri kiuchumi kutokana na kuwa soko kubwa la samaki wanaovuliwa katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa nchini Tanzania ilikuwa ikitegemea soko katika nchi hiyo jirani.
Mmoja wa wavuvi hao ambaye ni mkazi wa Kasanga wilayani humo  aliyejitambulisha kwa jina la Richard Sichone alisema kuwa serikali ya nchi hiyo imeondoa marufuku hiyo baada ya jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo kuonesha mafanikio ambapo hivi sasa wavuvi hao wameanza kuuza samaki wao nchini Zambia.
Alisema kuwa katika kipindi ambacho serikali ya nchi hiyo ilikuwa imezuia uvuvi katika nchi hiyo pamoja na biashara ya samaki kutoka nchi za Tanzania na Congo DRC kutokana na kipindu pindu walikabiliwa na ugumu wa maisha kwakuwa walikuwa wakiuza samaki kwa bei ya hasara tofauti na walipokuwa wakiuza nchini Zambia.

Sichone alisema kuwa katika nchi hiyo kuna makampuni 12 ambayo yamekuwa yakinunua samaki tani 1,200 kila siku ambapo kilo moja wavuvi wamekuwa wakiuza kwa shilingi 5,000 za kitanzania lakini katika kipindi ambacho nchi hiyo ilipiga marufuki ya biashara ya samaki soko lilishuka ambapo walikuwa wakiuza kilo moja kwa shilingi 1,500 na kulikuwa kuna kampuni moja tu ya Premji iliyopo Kasanga ambayo ilikuwa inauwezo wa kununua tani nane za samaki.
Naye Michael Sichilima mvuvi wa kijiji cha Kapele katika mwambao wa ziwa Tanganyika wilayani kalambo alisema kuwa kitendo ilichokifanya serikali ya Zambia ni chakupongezwa kwani kimetoa fursa ya biashara si tu kwa wavuvi wa nchini humo lakini pia wavuvi kutoka nchi jirani watanufaika.
Aliwasihi wavuvi kutoka mkoani wilayani humo kuheshimu sheria za nchi hiyo pindi wanapokwenda kufanya biashara ya samaki ili wasije kugeuka kero na kusababisha kuharibu uhusiano wa kibiashara na u dugu baina ya wanachi wa nchi hizo mbili kwakua mahusiano yao ni ya kihistoria na yanafaa kulindwa kwa maslahi ya waafrika wote.
Mwisho

Monday 19 March 2018

Mbunge atoa vitendea kazi

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

MBUNGE wa viti maalumu mkoani Rukwa(CCM) Silafu Maufi ametoa msaada wa vitendea kazi vya ofisi kwaajili ya jumuia ya Umoja wa wanawake mkoani Rukwa(UWT) ili viweze kuwasaidia katika kurahisisha kazi zinazo wakabili watendaji wa jumuia hiyo.

Akikabidhi vitendea kazi hivyo jana ambavyo  ni ngamizi (Computer) aina ya DELL pamoja na  kichapishi (printer) mbunge huyo alisema kuwa kabla ya kustaafu kazi na kuchaguliwa kuwa mbunge wa viti maalum alikuwa akifanya kazi ya Katibu wa CCM katika wilaya mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa katika utendaji wake wa kazi alikuwa akikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa kitendo kilichosababisha kutekeleza majukumu yake kwa shida na wakati mwingine kutokwenda sambamba na muda. 

Maufi aliwaeambia wanachama wa UWT kutoka wilaya za Kalambo, Nkasi, Sumbawanga mjini na Vijijini kuwa kumekuwa na tatizo la uvujaji wa siri za ofisi na za chama pia hasa katika kipindi cha chaguzi mbalimbali na sababu moja wapo ni kutumia ngamizi za nje ya ofisi kuchapa kazi za chama na jumuiya yenyewe.

Kutokana na changamoto hiyo ametumia kiasi cha shilingi milioni 10 kununua ngamizi nne pamoja na vichapishi aina ya HP vinne kila kimoja na ngamizi yake kwa ajili ya ofisi za UWT katika ofisi za wilaya zote katika mkoa wa Rukwa.


Kwaupande wake Beata Weller ambaye  ni katibu wa UWT wilaya ya Kalambo alitoa shukrani kwa niaba ya makatibu wengine ambapo alisema kuwa walikuwa wanalazimika kusafiri kilometa 50 kutoka Matai Kalambo kwenda mjini Sumbawanga kwaajili ya kuchapa kazi za jumuiya na kutumia gharama kubwa na wakati mwingine walilazimika kulala huko kutokana na kuwa ofisi yao ilikuwa haina vifaa hivyo muhimu vya kutendea kazi.

Alisema kuwa  licha ya kutoa shukrani za dhati kwa mbunge Maufi pia wanatoa pongezi kwa mbunge huyo kukumbuka alikotoka na kujaribu kutatua changamoto za kiofisi maana wabunge wengi wanawafikiria wananchi peke yao na kusahau chama na jumuia zake.

Chama cha Mapinduzi mkoani Rukwa kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya ofisi, ukosefu wa ofisi ambapo wilaya za Sumbawanga vijijini na Kalambo hazina ofisi kabisa.

Mwisho

Watoto wa kwenye mazingira magumu wawakera madiwani

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
BARAZA la madiwani la halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa limeviomba vyombo vya usalama vishirikiane na idaya ya uhamiaji  kuwakamata na kuwarudisha nchini kwao watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao wametoka katika nchi jirani za Zambia na  Congo DRC.
Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa alisema hayo hivi karibuni wakati akiongoza kikao cha baraza hilo baada ya wajumbe kulalamikia kuongezeka kwa watoto ambao ambao wamekuwa kero na wanajihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo uporaji.
Alisema kuwa hivi sasa mji wa Sumbawanga unakabiliwa na ongezeko la watoto wanaishi katika mazingira magumu ambao baadhi yao wanatoka katika nchi jirani ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu pamoja na ubakaji.
Malisawa alisema kuwa baada ya kubaini ongezeko la watoto hao halmashauri yake ilianza kuchukua hatua ambapo ilibaini baadhi ya watoto hao wanatoka katika nchi za Zambia na Congo DRC lakini baadhi yao wanatoka katika mikoa jirani na mkoa wa Rukwa.
‘’Ndugu zangu madiwani,hata mimi nakili kuwa watoto hawa ni bomu linalosubili kulipuka, baada ya jitihada za kuwafuatilia kujua tatizo ninini mpaka wanaongezeka kwa kasi kubwa tulibaini wengine wanatoka nchi jirani za Zambia na Congo DRC hivyo tunaomba vyombo vya usalama vishirikiane na idara ya uhamiaji warudishwe kwao’’ alisema.
Mmoja wa madiwani hao Vitalis Ulaya alisema kuwa watoto hao wanazidi kuongezeka kila kukicha katika mji wa Sumbawanga hali ambayo ni hatari kwakuwa hakuna jitihada za kutosha za kuweza kukabiliana na wimbi la ongezeko hilo.
Alisema kuwa wengi wa watoto hao wanazurula nyakati za mchana  wakiokota vitu majalalani na kuomba hela kwa wapiti njia na nyakati za usiku wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu hali inayosababisha amani kutoweka.
Naye Ester Mpelele mjumbe wa baraza hilo alisema kuwa watoto hao wamekuwa ni changamoto kubwa kwa wanawake kwani hivi sasa huwezi kutembea pekeyako nyakati za jioni na usiku hali ambayo aliiomba serikali kuingilia kati jambo hilo.
Aliwaomba wazazi katika Manispaa hiyo ya Sumbawanga kuwajibika katika malezi ya watoto wao kwani kitendo cha kuwaacha bila kuwapa huduma za msingi ikiwemo elimu wanawaandalia maisha mabaya ya baadaye na watakuja kuisumbua jamii kutokana na kushindwa kuwajibika kwao.


Mwisho

Thursday 15 March 2018

Walimu 16 watimuliwa kazi

Na Gurian Adolf
Nkasi

JUMLA ya walimu 16 wamefukuzwa kazi wilayani Nkasi mkoani Rukwa kwa kipindi cha miaka mitatu na wengine 11 wamepewa onyo kali baada ya kubainika wametenda makosa mbalimbali.

Katibu wa tume ya utumishi wa walimu TSC wilayani humo  Richard Katyega aliyasema hayo jana mbele ya kamishina wa tume ya Utumishi wa walimu Taifa, Samwel Koroso ambapo alisema  kuwa katika kipindi hicho  walipokea mashauri 23 na kupelekea walimu 16 kufukuzwa kazi,11 kupewa onyo kali na wengine 5 waliondolewa kazini baada ya kubainika kuwa na vyeti bandia.

Alisema kuwa  katika mwaka wa fedha wa 2016, 2017 na 18  tume hiyo imeweza kusikiliza mashauri hayo na kuyatolea maamuzi ambapo ilifikia maamuzi hayo baada ya kusikiliza mashauri hayo na pasipo kumuonea mwalimu hata mmoja na kutenda haki kwa mujibu wa sheria.

Katyega alisema kuwa tume hiyo sambamba na kuchukua maamuzi hayo pia imekua ikiwahamasisha walimu kufuata maadili ya ualimu kwa uhakika ili wasiweze kukumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake kamishna wa tume ya TSC Samwel Koroso alionyesha kusikitishwa na vitendo vya  uvunjifu wa maadili kwa waalimu hali inaoyopelekea  kufukuzwa kazi na kuwa wao kama tume ya maadili kwa walimu wataendelea kuwachukulia hatua Walimu wote ambao watakwenda kinyume na maadili ya ualimu

 Aliwataka walimu kwenda sambamba na misingi ya sheria ya utumishi kwa walimu kama inavyowataka na kuongeza kuwa walimu wilayani humo hawanabudi kuzipitia sheria za utumishi wa walimu ili waweze kuishi kwa kufuata sheria hizo zinavyo agiza.

Maofisa  kutoka ofisi ya ya kamishina wa tume hiyo nao waliweza kutoa mada mbalimbali zilizolenga kuwapatia elimu Walimu na kuwakumbusha sheria za utumishi wa walimu,huku walimu kwa upande wao walipata fursa ya kueleza changamoto zinazo wakabili  na zilipatiwa majibu kutokana na maswali waliyokuwa nayo.

Mwisho

Wednesday 14 March 2018

Auawa kwa rungu kwasababu ya mashamba yake

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

JESHI la Polisi mkoani  Rukwa, linawashikilia watu sita akiwemo mjukuu aliyekubalichukua hongo Shilingi milioni moja na kukubali babu yake auawe kwa kupigwa rungu kichwani kutokana na ugomvi wa ardhi.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema jana kuwa tukio la kuuawa kwa mzee huyo aliyefahamika kwa jina la Paul Kisiwa (72) mkazi wa kijiji cha Ng'ongo lilitokea machi 3 nyakati za jioni kwenye kijiji cha Kifinga Kata ya Mtowisa wilaya Sumbawanga.
Taarifa kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na Diwani wa Kata ya Mtowisa, Edger Malinyi, zilieleza kuwa baada ya kuuawa kwa mzee huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM ngazi ya kata alizikwa kinyemela shambani kwake.

Inaelezwa kuwa taarifa za kupotea mzee huyo zilianza kuzagaa ndipo ndugu wa marehemu, pamoja na majirani  wakishirikiana na polisi walianza kuchunguza tukio hilo, ambapo ilipofika machi 8 mwaka huu, watu hao walimbana mjukuu wa mzee huyo aitwaye John Kisiwa (22) ambaye alikiri kushiriki kupanga njama za kumuua babu yake kwa ujira wa Shilingi 1,000,000.

Diwani huyo, alisema kijana huyo alipanga njama ya mauaji hayo na wenzake ambao walikuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na mzee huyo ambaye awali aliwakodisha watu hao shamba la ekari zaidi 15 kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Alisema baadaye aliwanyang'anya shamba hilo na kuamua kulilima  yeye mwenyewe kitendo kilichowauzi watuhumiwa  hao ambao walijikuta wakiingia katika mgogoro wa kugombea eneo hilo, hali ilisababisha waandae mipango ya kumuua mzee huyo.

Inadaiwa kuwa  siku ya tukio la mauaji hayo, watu hao walimvamia mzee huyo akiwa katika  shambani lake hilo, na kisha kumpiga na rungu kichwani ambapo alianguka na kufariki dunia papo hapo.

Diwani Malinyi alisema baada ya kumuua mzee huyo walichimba shimo shambani humo na kumfukia ili kupoteza ushahidi hali iliyobainika baada ya mjukuu wake kubanwa na kueleza ukweli hivyo polisi walifukua eneo hilo na kukuta mwili wa mzee huyo.

Kamanda Kyando aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa kuwa ni Kela Lubinza (15), Chani Lubinza (29), Simba Lubinza (16)  wote wakiwa ni ndugu wa familia moja pia Deshi Mihambo (40) na Muli Sabini (21) ambao ni majirani wa wanafamilia hao.

Alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa mara baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.

Mwisho

Madarasa bado ni changamoto Rukwa

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MKOA wa Rukwa bado unakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo jumla ya vyumba 4,226 vinakitajika ili  kumaliza tatizo hilo.
Akizungumza hivi karibuni afisa elimu mkoa huo Nestory Mroka alisema kuwa mahitaji hayo yamekuwa yakisababisha mkoa huo kutopiga hatua katika mafanikio ya elimu.
Alisema kuwa ili wanafunzi waweze kufanya vizuri katika masomo yao ni lazima kuwe na miundombinu mizuri walimu wakutosha,vitabu pamoja na walimu lakini kama kuna mapungufu kati ya hayo mambo hata ufaulu hauwezi kuwa mzuri.
Mroka alisema kuwa kutokana na changamoto hizo jitihada za makusudi zinahitajika katika kulimaliza tatizo hilo pamoja na mengine ili kuweza kuinua ufaulu wa wanufunzi katika shule za msingi pamoja na sekondari ambapo mpaka sasa ufaulu katika kidato cha nne ni wastani wa daraja la nne.
Afisa elimu huyo alisema kuwa yeye binafsi amejitahidi kuhakikisha anawasimamia walimu ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo ikiwamo ni pamoja na kuwepo kazini kwa muda muafaka sambamba na kufundisha kwa juhudi zote ili idara ya elimu iweze kuwa ya mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri mkoani humo.
Kwaupande wake mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo aliziagiza halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha zikuja na  mikakati ya kumaliza tatizo hilo pamoja na kwamba limeongezeka baada ya serikali ya awamu ya tano kuja na sera ya elimu bure.
Alisema kuwa mafanikio yanakuja na changamoto zake lakini sio sababu ya kulalamikia mafanio kilichopo ni kuzikabiri changamoto hizo kwani hivi sasa kila mtoto mkoani humo awe wa tajiri ama masikini anauhakika wa kupata elimu tofauti na miaka ya nyuma.
‘’ninakila sababu ya kumpongeza muheshimiwa raisi John Magufuli kuamua serikali yake kutoa elimu bure kwani hivi sasa kila mtoto wa mkoa huu anauhakika wa kupata elimu kwakuwa inatolewa bila malipo hivyo ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anakwenda shule hata kama hana sare’’ alisema
Wangabo alisema kuwa huu ni wakati wa serikali,wazazi,wadau wa elimu na wadau wengine wa maendeleo  kushirikiana katika kumaliza changamoto hiyo kwani wakisubiri serikali peke yake ifanye kazi hiyo mkoa utachelewa kupiga hatua katika elimu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa hivi sasa serikali inajikita katika uchumi wa viwanda lazima pia kuhakikisha kuwa elimu haibaki nyuma na mzizi wa kufikia mafanikio hayo ni kuwekeza vizuri katika elimu kwani huko ndiko watapatikana wataalamu watakao fanya kazi katika viwanda hivyo.
Mwisho

Wavuvi Rukwa walilia viwanda

Na Gurian Adolf
Kalambo

BAADHI ya wavuvi mkoani Rukwa wameiomba serikali kuiokoa sekta hiyo kwa kualika wawekezaji wakubwa ili wawekeze viwanda vya kusindika samaki hali itakayo saidia kuwa na soko la uhakika la samaki mkoani sambamba na kuifikisha nchi katika uchumi wa viwanda.
Wakizungumza na gazeti hili walisema kuwa hivi sasa sekta ya uvuvi mkoani humo inakabiliwa na hali ngumu baada ya serikali ya Zambia kupiga marufuku uvuvi katika ziwa Tanganyika sambamba na kuingiza samaki kutoka katika nchi jirani za Tanzania na Kongo kutokana na kipindupindu kwasababu mkoani humo hakuna viwanda vya kusindika mazao ya ziwani.
Mmoja wavuvi aliyepo katika kijiji cha Kasanga wilayani Kalambo mkoani Rukwa Skeva Sinyangwe alisema kuwa hivi sasa sekta ya uvuvi imekabiliwa na changamoto kutokana na kukosa soko la samaki ambapo kilogramu moja ya samaki wamekuwa wakiuza chini ya shilingi 1,000 kutoka shilingi 5,000 waliyokuwa wakiuza hapo awali.
Alisema kuwa wavuvi wa mkoani Rukwa walikuwa wakitegemea kuuza samaki wao nchini Zambia ambako kuna makampuni yapatayo 12 ambapo yalikuwa yakinunua mpaka tani 1,200 ambao walikuwa wakiuza katika makasha ya mbao yenye uzito wa kilogramu 30 kwa shilingi 125,000 lakini tangu nchi hiyo ikabiliwe na kipindupindu na kuzuia ununuaji wa samaki wababich bei imeporomoka.
Naye Frances Simzosha mkazi wa Kasanga alisema kuwa kwakuwa hivi sasa serikalin ya awamu ya tano imejikita katika uchumi wa viwanda ni vizuri sasa ikafungua milango na kuwaalika wawekezaji wakubwa waweze kufika mkoani Rukwa na kuwekeza katika viwanda vya kusindika samaki ambao wanaonekana kukosa soka hivi sasa.
Alisema kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuona nchi inakwenda katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda sambamba na kupatikana kwa ajira hali ambayo fursa ipo kupitia sekta ya uvuvi katika ziwa hilo.
Simzosha alisema kuwa sambamba na hayo pia nchi itapata fedha nyingi kutokana na malipo ya kodi kitu ambacho raisi wa awamu ya tano John Magufuli anataka kukiona na inawezekana iwapo yakiandaliwa mazingira mazuri.
Aliiomba serikali kuitumia fursa hiyo vizuri  ya kuanzisha viwanda ambayo itawakwamua wavuvi katika lindi la umasikini,wananchi wanaohitaji ajira sambamba na kuongeza pato la serikali litakalo iwezesha kupata fedha za kuwahudumia wanchi wake.
Mwisho

Tuesday 13 March 2018

Serikali kuanzisha mpango wa kulipia kidogo kidogo bima ya afya

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

SERIKALI imesema ina andaa mpango kwaajili ya wananchi kulipia fedha kidogo kidogo  ili kwa atakaye kamilisha atapata fursa ya kujiunga na mfuko wa bima ya afya (NHIF) wa Taifa.

Waziri wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia na watoto Ummy Mwalimu aliyasema hayo hivi karibuni mjini Sumbawanga wakati akikabidhi mabati 100 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha afya Tambaruka kilichopo wilayani Nkasi yaliyotolewa na mfuko wa bima ya afya NHIF mkoani Rukwa.
Alisema kuwa serikali imebaini wananchi wengi wanashindwa kulipia gharama ya matibabu ya kwa mara moja hali ambayo serikali inaandaa mpango ili wananchi walipie kiasi kidogo kidogo atakapo kamilisha kiwango kinachitakiwa anapewa kadi ya uanachama ya mfuko wa NHIF ambapo atapata fursa ya matibabu.
Waziri huyo wa afya alisema kuwa kwa mtu ambaye si mtumishi wa umma anapaswa kulipia shilingi milioni 1.5 ili ajiunge na mfuko huo fedha ambazo ni nyingi kwani baadhi ya wananchi hususani wa vijijini wamekuwa wakishindwa na hivyo kukosa fursa ya kuwa wanachama wa NHIF na kupata haki ya kutibiwa katika vituo zaidi ya 7,000 ambazo vinatoa huduma za bima ya afya nchi nzima.
Hata hivyo waziri Ummy aliwasisitiza wananchi wa mkoa huo kujiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF ambayo inagharimu kiasi cha shilingi 10,000 ambapo watapata fursa ya matibabu kwa watu watano katika kaya na kujihakikishia matibabu katika maeneo yao kuliko kukosa kabisa huduma za afya kwakuwa magonjwa huwafika binadamu bila taarifa na wakati mwingine wanakuwa katika hali mbaya ya kiuchumi.
Naye meneja wa bima ya afya mkoani Rukwa Simon Mbaga aliwasihi wazazi kuwalipia watoto wao shilingi 50,400 ambapo watasajiliwa na huduma za Toto  Afya kadi ambapo watapata fursa ya kutibiwa katika vituo vinavyotoa huduma za bima ya afya ya Taifa ndani na nje ya mkoa huo.
Kwaupande Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini Ally Kessy aliushukuru mfuko huo wa bima ya afya kwa kutoa mabati hayo ambapo alisema kuwa yatasaidia katika ujenzi wa kituo cha afya cha Tambaruka.
Pia mbunge huyo alimuomba waziri wa afya kuona namna ya kuusaidia mkoa wa Rukwa ili uweze kujenga vituo vya kutosha vya afya kwani unakabiliwa na uhaba mkubwa na hivyo kushindwa kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi inayotaka kila kata kuwa na kituo cha afya.
Mwisho

Wavuvi walia samaki soko la samaki kudoda

Na Gurian Adolf
Kalambo

WAVUVI wanaofanya shughuli katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi baada ya serikali ya nchini Zambia kupiga marufuku shuguli za uvuvi nchini humo pamoja na kuingiza samaki wabichi kutoka nchi za Tanzania na Kongo kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa kipindu pindu.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wavuvi hao walisema kuwa wanakabiliwa na hali ngumu kwakuwa zaidi ya asilimia 85 ya mauzo yao ya Samaki wabichi wanategemea soko la Mpulungu nchini Zambia.
Mmoja wa wavuvi hao Kennedy Sinyangwe alisema kuwa katika nchi hiyo kuna makampuni 12 ambayo yanauwezo wa kununua tani 1,200 za samaki kila siku ambapo kilo moja wavuvi wamekuwa wakiuza kwa shilingi 5,000 za kitanzania lakini tangu nchi hiyo ipige marufuki hiyo wamejikuta wanahali ngumu kwakuwa hawana soko la samaki.
Alisema kuwa changamoto iliyopo katika nchi ya Tanzania hakuna makampuni makubwa ya kununua samaki ambapo mpaka hivi sasa kuna kampuni moja ya Premji iliyopo eneo la Kasanga ambayo inauwezo wa kununua samaki kiasi kidogo ambacho ni tani 8 kitendo kilichosababisha wakose soko.
Sinyangwe alisema kuwa katika mji wa kasanga serikali ya Tanzania imejenga soko kubwa la samaki na lakisasa kwa gharama kubwa ya shilingi milioni 800 lakini inachumba kimoja tu cha baridi cha kuhifadhia samaki chenye uwezo wa kuhifadhi tani 20 ambazo ni kidogo ukilinganisha na zinazo vuliwa kwa siku katika ziwa hilo.
Alisema kuwa tangu nchi hiyo imepiga marufuku shughuli za uvuvi katika nchi yao na kuingiza samaki wabichi kutoka katika mataifa jirani soko la samaki limeshuka ambapo hivi sasa wavuvi wanalazimika kuuza kilo moja ya samaki chini ya shilingi 1,000 kitendo kinacho wafanya wakabiliwe na hali ngumu.
Naye Peter Sichilima mvuvi wa samaki katika ziwa Tanganyika eneo la Samazi mkoani Rukwa aliiomba serikali ya Tanzania kuhakikisha inakamilisha miundombinu katika soko la kuuzia samaki ili waache kutegemea soko la nchini Zambia kwani limekuwa na changamoto nyingi.
Alisema kuwa serikali inakosa mapato iwapo biashara ya samaki ingefanyika nchini mwetu kwakuwa wageni wangekuwa wanalazimika kuja kununua samaki na wanapoingia wangekuwa wanalipa tozo mbalimbali tofauti na hivi sasa ambapo wao wanalazimika kulipa tozo hizo nchini Zambia kwakuwa ndiko soko liliko.
Naye Philipo Siulapwa mkazi wa Kasangana alisema kuwa iwapo kwakuwa hivi sasa serikali imejikita katika uchumi wa viwanda ni vizuri sasa vikaanzishwa viwanda vya kusindika samaki ili iwe rahisi kuwahifadhi na kuwatafutia soko la kimataifa ambalo halina changamoto kama kutegemea kuuza samaki wabichi.
Mwisho

Kanisa lataka serikali irudishe majengo yake

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

CHUO cha ualimu cha Sumbawanga kilichopo mkoani Rukwa huenda kikasitisha kupokea wanafunzi kwaajili ya kujiunga na chuo hicho baada ya Kanisa katoliki jimbo la Sumbawanga kudai majengo yake ambayo yanayotumiwa na serikali kwaajili ya kusomea wanafunzi wa chuo hicho kutokana na kutopewa majengo mengine kama walivyo ahidiwa miaka ya nyuma.
Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa RCC hivi karibuni alisema kuwa majengo yanayotumiwa na chuo hicho ni mali ya kanisa katoliki ambalo liliyatoa kwa serikali mwaka 1974 ili yatumike kama ofisi za mkoa kutokana na mkoa huo ulikuwa mpya na ulikuwa hauna ofisi.
Alisema kuwa kipindi hicho alikuwepo Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Sumbawanga marehemu Karolo Msakila ambaye aliombwa majengo hayo ili yatumike kama ofisi za mkoa huo ambapo alikubari na kuiazima serikali na ofisi za mkoa huo zilikuwa hapo.
Ilipofika mwaka 1989 serikali ya mkoa huo ukawa umejenga ofisi zake lakini haukuyarudisha majengo hayo kwa mmiliki wake ambaye alikuwa anataka kufungua chuo cha kilimo badala yake serikali ilianzisha chuo cha ualimu bila makubaliano yoyote.
Baada ya muda mrefu kanisa katoliki liliyahitaji majengo yake ambapo serikali ya mkoa uliahidi kulipatia majengo yalikuwa yakitumika na kampuni ya ujenzi ya barabarakwa kiwango cha lami  kati ya Sumbawanga-Tunduma, lakini hata hivyo serikali ya mkoa huo haikulipa kanisa majengo hayo badala yake yakatumika kuanzisha tawi la chuo cha Sayansi cha Mbeya(MUST).
Kutokana na hali  hiyo kanisa katoliki lilihoji kuhusu hatma ya majengo yao ambapo serikali ya mkoa iliahidi tena kulipa majengo ya kambi ya ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Mpanda yaliyopo katika eneo la Makutano mjini Sumbawanga,lakini napo haikuwa hivyo baada ya serikali kuweka ofisi za Tanroad mkoa na hivyo kanisa kukosa majengo hayo.
Baada ya kushindikana mara mbili zote kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga lilikutana na uongozi wa serikali ya mkoa ambapo lilisema halitaki tena kupewa majengo mengine bali wanataka majengo yao kwakuwa kanisa hilo limevumilia na kufikia mwisho.
Kutokana na kujuwa kuwa majengo hayo si mali ya serikali kwa muda mrefu yalikuwa hayafanyiwi ukarabati mpaka hapo NACTE ilipotishia kukifunga chuo hicho kutokana na kuwa kimechakaa ndipo serikali ya mkoa ilipoliomba tena kanisa katoliki liwape muda ambapo lilitoa miaka mitano wanafunzi hao wawe wameondoka katika majengo yao na serikali ya mkoa iwe imejenga chuo chake na wakabidhi majengo kwa kanisa hilo liendelee na matumizi waliyokusudia wakati yakijengwa.
Mkuu wa Mkoa wangabo aliwaambia wajumbe wa kikao cha RCC serikali ya mkoa imewasiliana na tasisi ya Jumuiya ya Maendeleo mkoani Rukwa (JUMARU) ambapo imetoa ardhi katika kijiji cha Pito nje kidogo ya mji wa Sumbawanga ambapo yalikuwa mashamba ya bega kwa bega yanayomilikiwa na kijiji hicho ambapo serikali ya mkoa imeanza mchakato wa kutafuta fedha kwaajili ya ujenzi wa chuo cha ualimu Sumbawanga.
Alisema kuwa lengo la serikali ya mkoa ni kujenga chuo hicho na kwakuwa eneo ni kubwa kijengwe pia chuo kikuu ambacho kitamilikiwa na serikali ambacho kitakuwa makao yake makuu mkoani Rukwa.
Baada ya taarifa hiyo kutoka kwa mwenyekiti huyo wa RCC mkoa wa Rukwa wajumbe wa kikao hicho walishauri kuwa nivizuri pia ukarabati ukaendelea kufanyika katika chuo hicho kinacho tumika hivi sasa kilichopo eneo la Kantalamba ili NACTE wasisitishe kuwapangia wanafunzi kwakua miaka mitano waliyo azimwa na kanisa hilo bado ni kipindi kirefu.
Mwisho

Bavicha wanena

Na Gurian Adolf
Sumbawanga.

Baraza la vijana la Chadema (Bavicha) limeitaka Serikali kutumia gharama yoyote kulinda amani ya nchi inayo onesha dalili ya kutoweka kutokana na kukithiri kwa vitendo vya mauaji ya kinyama na utekaji unaofanywa watu wasiojulikana.


Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu alisema hayo juzi wakati wa akifungua kongamano la vijana lilolenga kuwapa elimu wanachama wake  kuhusu wajibu wao katika siasa za sasa ambalo liliandaliwa na Bavicha mkoa wa Rukwa.

Alisema hali ya kisiasa hivi sasa hapa nchini ni tete kutokana kushamiri kwa vitendo vya utekaji na mauaji ya kinyama yanayofanywa na watu wanaodaiwa kutojulikana huku serikali ikiwa haijavalia njuga vya kutosha katika kudhibiti vitendo hivyo.

Makamu huyo mwenyekiti alisema imefika wakati sasa serikali kutumia gharama yoyote ili kulinda amani ya taifa hili iliyoasisiwa na Baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere ambaye katika utawala wake na zile zilizopita hawakukubali kuona amani ikitiwa doa.

"Amani ni tunu ya taifa hili....... kwa hiyo sisi kama wanasiasa tulazima tuhakikishe nchi inakuwa na amani asitokee mtu wa kutaka kutia doa amani yetu na sisi tukamwangalia......kwa hiyo serikali ina wajibu wa kukomesha vitendo hivi vya uvunjifu wa amani, utekaji na mauaji ya kinyama ya watu" alisema

Awali, Mwenyekiti wa Bavicha mkoa wa Rukwa, Aida Khenan aliwataka vijana wa Chadema mkoani humo kulitumia kongamano hilo ili kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto za kisiasa ambazo zimekuwa zikiathiri ustawi wa vyama vya upinzani hapa nchini.

Khenan ambaye pia mbunge wa viti maalumu mkoani Rukwa, alisema kuwa,vijana hao wanapaswa kutumia fursa ya kongamano hilo kubaini mbinu mbalimbali za kujiongezea kipato ili waeze kujikwamua kiuchumia na hatimaye kuondokana na umasikini.

Aliongeza kwamba ili vijana waweze kushiriki kikamilifu katika siasa za mageuzi wanapaswa wawe na nguvu ya kiuchumi hivyo makongamano kama hayo yanawapa fursa ya kubaini mbinu mbalimbali za kujiongezea kipato.

Mwisho

Saturday 10 March 2018

RC awaijia juu watendaji


Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MKUU wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amewaijia juu watendaji wa serikali mkoani humo kutokana na kuwa na tabia ya kuwasilisha takwimu zisizo na mabadiriko katika vikao mbalimbali kwani kitendo hicho kinaonekasha ni wavivu wa kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo hivi karibuni, Wangabo alisema kuwa tangu amefika amekuwa akipewa taarifa ambazo takwimu zake hazibadiriki kwa kuonekana kupungua ama kuongezeka kwa jambo wanalowasilisha.
Alisema kuwa alipopangiwa teuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo na kupangiwa kazi aliongoza kikao cha kwanza cha RCC na alielezwa kuwa katika mkoa huo kunachangamoto kubwa ya mimba kwa wanafunzi ambapo taarifa hiyo ilieleza katika kipindi cha Januari mpaka Juni mwaka jana kuna wanafunzi 325 waliopata ujauzito na hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyehukumiwa kwa kosa hilo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa taarifa hiyo ilieleza kuwa katika kipindi cha juni mpaka desemba mwaka jana takwimu zilionesha kuwa bado idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito iko vilevile hakuna ongezeko wala kupungua.
Wangabo alisema kuwa hivi sasa taarifa iliyotolewa katika kipindi cha januari mpaka mwezi machi mwaka huu inaonesha kuwa kunamimba kwa wanafunzi wa shule za msingi 37 na sekondari 288 ambapo jumla yake ni 325 ambapo hakuna tofauti yoyote tangu alipoanza kupewa taarifa ya suala hilo.
Alisema kuwa kinacho onekana watendaji wa mkoa huo wamekuwa wakinakiri taarifa ileile na kuiwasilisha katika vikao bila kufanyia marekebisho hali inayoonesha ni uvivu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwenyekiti huyo wa RCC alisema kuwa yeye binafsi amefanya jitihada za kutosha kutoa elimu kuhusiana na suala la mimba lakini takwimu hazibadiriki hali inayosababisha agundue kuwa kunauzembe katika kuwajibika kwa watendaji hao.
Katika kikao hicho baadhi ya wajumbe walishangazwa mkoa huo kuwa na viwanda 901 lakini bado wananchi wake ni masikini kitu ambacho walisema kuwa nilazima wajitafakari kwakuwa haiwezekani mkoa kama warukwa kuwa na viwanda vyote hivyo lakini wananchi ni masikini.
Mwanasiasa mkongwa Chrisant Mzindakaya alisema kuwa lengo la serikali kujikita katika uchumi wa viwanda ni zuri na lina nia ya kuwakomboa wananchi kutoka katika umasikini lakini changamoto ni watendaji wa serikali ambao wamekuwa ni mabingwa wa kuzungumza bila vitendo.
Alisema kuwa mkoa huo umekuwa na mikakati mingi mizuri kwa miaka mingi lakini tatizo ni namna ya kuitafsiri mikakati hiyo katika vitendo ili iweze kufanikiwa na wanachi wa mkoa huo waweze kupiga hatua na kuwa na maisha bora.
Pia alisema kuwa jitihada zifanyike za kushawishi wawekezaji wawekeze viwanda vikubwa ambavyo vitatoa ajira nyingi kwa wakazi wa mkoa huo tofauti na hivi sasa viwanda vilivyo vingi ni vyerehani ambavyo vinaajiri mtu mmoja ndiyo maana pamoja na kusema kuwa mkoa wa Rukwa unaidadi kubwa ya viwanda lakini bado wananchi wake ni masikini na wanakabiliwa na tatizo la ajira.
Mwisho

Friday 9 March 2018

lishe tatizo Rukwa


Na Gurian Adolf
Sumbawanga
PAMOJA na kuwa mkoa wa Rukwa ni mmoja kati ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula hapa nchini lakini watoto mkoani  humo wanaongoza kwa utapiamlo na udumavu hapa nchini ambapo umefikia kiwango cha asilimia 56.3 huku kiwango cha kitaifa ni asilimia 36.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Kaimu katibu tawala wa mkoa huo Albinus Mgonya wakati akizungumzia hali ya lishe katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa RCC kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Alisema kuwa watoto katika mkoa huo wanakabiliwa na hali mbaya ya utapiamlo na udumavu kiasi kwamba imekuwa ikisababisha hata wanafunzi kutofanya vizuri katika masomo yao.
Alisema kuwa pia kuwepo kwa changamoto ya lishe katika mkoa huo kumesababisha kuwepo kwa tatizo la upungufu wa uzito kwa watoto ambapo takwimu zinaonesha kuwa mkoa huo umefikia wastani wa asilimia 23 wakati kiwango cha kitaifa ni asilimia 14.
Mgonya alisema kuwa hali hiyo imesababisha kuwepo kwa ukondefu kwa watoto katika mkoa huo ambao umefikia kiwango cha asilimia5.3 wakati kiwango cha kitaifa kikiwa ni asilimia 5.
Katika kikao hicho afisa elimu wa mkoa wa Rukwa Nestory Mroka alisema kuwa ufaulu wa wanafunzi wa sekondari katika mkoa huo ni wastani wa daraja la nne ambapo katika matokeo ya mtihani uliopita wa taifa wa darasa la nne mkoa huo ulishika nafasi ya 179 kati ya shule 185 ambazo wanafunzi wake walisajiliwa kufanya mtihani huo.
Alisema kuwa iwapo mkoa huo unataka kuongeza ufauru kwa wanafunzi ni lazima elimu ya lishe itolewe kwani ni miongoni mwa sababu zinazochangia mkoa huo kuwa na matokeo mabaya katika mitihani ya sekondari na shule za msingi.
Aidha katika kikao hicho mmoja wa wajumbe kutoka shirika la Plan International  Gasper Materu alisema kuwa nilazima suala ma afisa lishe wajikite katika suala zima la kutoa elimu kwani hata nia ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda inaweza kukwama iwapo wananchi watakuwa na afya mbaya kwasababu ya kutokuwa na lishe ya kutosha.
Alisema kuwa wataalamu wa kufanya kazi katika viwanda hivyo ni lazima wapate elimu na iwapo ufaulu wao utakuwa hafifu kutokana na lishe mbaya basi nia ya serikali inaweza isifikiwe kutokana na tatizo la lishe.
Naye mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao cha RCC aliwaagiza maafisa lishe mkoani humo kuhakikisha kuwa wanakabiliana na hali hiyo kwakuwa mkoa huo unavyakula vya kutosha changamoto iliyopo ni wananchi hawajui wale chakula kwa namna gani ili tatizo hilo liishe.
mwisho

Thursday 8 March 2018

Waziri Ummy Mwalimu atoa siku saba kwa wanawake kurejesha mikopo



Na Gurian Adolf
Sumbawanga

WAZIRI wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia na watoto Ummy Mwalimu ametoa siku saba kwa wanawae wote waliochukua mikopo katika benki ya wanawake wawe wamerudisha vinginevyo waanze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa mgeni rasmi akihutubia katika sherehe za wanawake zilizofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
Alisema kuwa benki ya wanawake imekuwa ikitoa mikopo lakini kitu cha kusikitisha baadhi yao wamekuwa na tabia ya kurudisha mikopo hiyo kitendo kinachowanyima fursa wanawake wengine ya kunufaika na mikopo hiyo.
Waziri Ummy alisema kuwa anatoa siku saba wanawake wote wanaodaiwa mikopo na walipaswa kuwa wamesharudisha wahakikishe wamerudisha katika kipindi cha siku saba tofauti na hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia waziri huyo alitumia fursa hiyo kumuomba waziri wa utawala bora George Mkuchika kuwafikisha mahakamani wanawake wote waliokuwa watumishi wa benki hiyo ambao walifanya ufisadi kwani wamekuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya wanawake wenzao.
Alisema kuwa benki hiyo iliajiri wanawake ikiamini kuwa watakuwa na uchungu na benki yao ambapo wataisimamia vizuri ili iweze kuendelea zaidi na kuwa msaada lakini kinyume na matarajio wanawake hao ndio wamefanya ufisadi na kuendelea kuwakwamisha wanawake wenzao.
‘’nitumie fursa hii kumuomba kaka yangu waziri wa utawala bora Geore Mkuchika kuwafikisha mahakamani wanawake wote ambao walikuwa watumishi wa benki ya wanawake na kisha kufanya ufisadi kwani hawa ni adui wa wanawake wenzao’’ alisema.
Waziri huyo alitumia fursa hiyo kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kufikiria upya katika suala la kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake na vijana kwani mikopo inayotolewa haiendani na uhalisia kwakuwa haiwezekani kikundi cha watu 15 wakakopeshwa shilingi 300,000 halafu ukategemea watapiga hatua.
‘’Naagiza wakurugenzi wote nchini kutazama upya suala la mikopo ya wanawake na vijana inayotoka katika asilimia tano ya mapato ya halmashauri kuwakopesha mikopo itakayowasaidia kufanya shughuli na kupata faida kwasababu utakuta kikundi cha watu 15 wanapewa shilingi 300,000 fedha ambazo hazitoshi walau ziwe hata shilingi milioni kumi kwa kikundi walau wanaweza kuzizalisha’’ alisema.

Pia aliitaka jamii kubadili mtazamo wa kufikiria kuwapelekea misaada ya chakula na nguo watoto yatima na wanaoishi katika  mazingira magumu badala yake waanze kuwalipia huduma ya afya kupitia Toto Afya Kadi kwani miongoni mwa changamoto zinazo wakabiri watoto hao ni pamoja na huduma za afya.
Naye mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Aesh Hilary alimuomba waziri huyo magari ya kubebea wagonjwa ambapo wanawake hasa wajawazito ambao wanahitaji huduma za dharula kwakua mkoa huo wa Rukwa unachangamoto ya upungufu wa magari hayo.
Baada ya kulisikia ombi hilo waziri huyo wa afya aliahidi kutoa magari mawili ya kubebea wagonjwa(ambulance) ambapo moja litakuwa kwaajili ya hospitali ya rufaa ya Sumbawanga na jingine aliagiza kuwa kitafutwe kituo kilichopo mbali na mjini ndiyo kipatiwe gari hilo.
Naye mkuu wa Kalambo Julieth Binyura alimshukuru waziri Ummy kwa kukubali kufika mkoani Rukwa na kusherekea na wanawake wa mkoa huo kwani amewapa hamasa na kuwasaidia kutatua changamoto nyingi ambazo zitawafanya kuongeza ari katika utendaji kazi.
Mwisho