Monday 23 April 2018

Aachiwa mke kwa laki 8

Na Gurian Adolf
Katavi
MKAZIwa kijiji cha Ntumba kilichpo wilayani Tanganyika katika mkoa wa Katavi, Charles Sabuni (37)  amepwa  viboko 30 hadharani baada ya kushikwa ugoni na mke wa jirani yake Ntema Mwiwela, juzi usiku wa manane kijijini hapo.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa adhabu hiyo  alipewa mgoni huyo ili iwefundisho kwake na  kwa wanaume wengine wenye tabia kama hiyo.
Akisimulia tukio hilo mwenyekiti wa Kitongoji cha Ntumba Samwel Mbuya alisema lilitokea saa tisa usiku, juzi nyumbani kwa Mwiwela ambaye anaishi jirani na Sabuni.
Akifafanua alisema kuwa mchana wa siku hiyo ya tukio hilo Mwiwela alimuaga mkewe kuwa ana safiri ambapo alirejea nyumbani kwake ghfla usiku wa manane na kumkuta Sabuni akiwa amelala chumbani kwake.
“Mwenye mke alimthibiti mgoni wake huyo asitoroke huku akimwamuru apige mayowe huku akisema anaomba msaada kwani amefumaniwa na mke wa mtu ….. kele hizo ziliwaamsha wanakijiji wenzake ambao walikimbilia eneo la tukio na  walipigwa na kutwaa kumkuta Sabuni akiwa chumbani chini ya ulinzi wa Mwiwela “ alieleza.
Alieleza kuwa wananchi hao walielezwa na Mwiwela  kitendo alichofanyiwa na jirani yake Sabuni ambapo walipandwa na hasira na kuamuru aendelee kuwa chini ya ulinzi hadi kutakapopambazuka .
Inadaiwa kulipokucha wananchi hao wenye hasira walimuaru mwenzao huyo apewe adhabu kali ya kucharazwa viboko hadharani ili iwe fundisho kwake na kwa wanaume wengine wenye tabia kama hiyo
Hata hivyo Sabuni alinusurika baada ya viongozi wa kitongoji wakiongozwa na mwenyekiti Mbuya na kuwazuia wasimcharaze viboko hadharani  kwa kuwa watakuwa wamekiuka haki za binadamu .
Ndipo kilipoitishwa kikao cha dharura kikiwajumuisha viongozi wa serikali wa kitongoji hicho, wazee  pamoja na Mwiwela na ‘mgoni wake ambapo baada ya majadiliano marefu Sabuni alikubali kumlipa faini faini ya  kiasi  cha Shilingi 800,000/- ikiwa ni fedha alizotoa mahali wakati muoa mke wake .
Kwa mujibu wa Mbuya mara tu Mwiwela alipokabidhiwa kiasi hicho cha fedha hapo hapo alimkabidhi mke wake kwa Sabuni akidai kuwa hawezi kuendelea  kuishi naye kwa sababu sio muaminifu.


Mwisho

Radi yaua mwanafunzi

Na Gurian Adolf
Nkasi
MWANAFUNZI wa darasa la pili shule ya msingi Kipundu James Kandege (8) amefariki dunia baada ya kupigwa radi juzi jioni akiwa nyumbani  kwao na wenzake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisa mtendaji  wa kijiji cha  Mabatini kata ya Namanyere  Ibrahimu Adriano alisema kuwa  tukio hilo lilitokea juzi jioni majira ya saa 10 alipokuwa ameketi nyumbani na wenzie walipokuwa wakila chakula cha mchana.
Alisema kuwa marehemu akiwa na wenzie sambamba na wazazi wake wakila chakula  katika kitongoji cha Katowa kijiji cha Mabatini walipigwa na radi wakiwa ndani ya nyumba yao na mwanafunzi huyo alifariki dunia papo hapo huku wengine wakisalimika.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kipundu Josephat Laban athibitisha kutokea kwa kifo cha  mwanafunzi huyo ambapo alisema kuwa shule hiyo iliwaruhusu Wanafunzi wote walishiriki katika msiba huo sambamba  na mazishi huku akidai kuwa shule imempoteza mtu muhimu.
Diwani wa kata ya Namanyere Evarist Mwanisawa alisema  kuwa Mwanafunzi huyo alikua ni mkazi wa kitongoiji cha Katowa na ndiko alikokutwa na mauti na kuwa mazishi ya mtoto huyo yamefanyika katika kijiji cha Lunyala.
Mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda amekiri kutokea kwa  kifo hicho na kuwa na kuwa wakati radi hiyo ikipiga Mwanafunzi huyo alikua pamoja na watoto wenzie na wazazi wake wote wawili wakila chakula ambapo katika hao hakuna mwingine aliyepata madhara yoyote .
Alisema kuwa serikali kupitia idara ya elimu msingi wilayani humo imeshiriki  katika mazishi ya mwanafunzi huyo licha ya kudai kuwa watu wengi walishikwa na simanzi kutokana na tukio hilo.
Katika siku za hivi karibuni wilaya Nkasi kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya watu kupiga radi na kusababisha vifo au mifugo kufa kiasi cha wananchi kuishi kwa hofu huku wakiwa hawajui nini cha kufanya.


mwisho

Saturday 21 April 2018

Tibiweni upesi,muishi maisha marefu


Na Gurian Adolf
Sumbawanga

WAKAZI mkoani Rukwa wameshauria kuacha tabia ya kupuuza kutibiwa  magonjwa wanayougua kwa wakati kwani vifo vingi vinatokana na kutofanya maamuzi ya haraka ya kupata matibabu.

Ushauri huo umetolewa jana katika ukumbi wa mikutano wa hospital ya mkoa ya Sumbawanga na katibu tawala wa mkoa huo Benard Makali alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa ambapo walikuwa wakipewa elimu kuhusiana na kufanyika kwa chanjo ya kitaifa ya kuzuia saratani ya kizazi kwa watoto wa kike.

Alisema kuwa moja kati ya changamoto kubwa inayosababisha vifo vingi ni watu kutokuwa na utaratibu wa kupata matibabu haraka pindi wanapougua au kuhisi dalili za kuugua kitendo kinacho changia ongezeko la vifo.

Katibu tawala huyo wa mkoa wa Rukwa alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakitembea na magonjwa kwa muda mrefu mpaka wakifikia maamuzi ya kwenda kupata matibabu,ugonjwa unakuwa umefikia katika hatua mbaya zaidi.

Makali alisema kuwa hivi sasa sayansi ya afya imepiga hatua kubwa kila tatizo linaufumbuzi wake kinachotakiwa ni wananchi kujenga utamaduni wa kutibiwa haraka pindi anapohisi dalili za kuugua hali itakayo saidia watu kuishi maisha marefu hata kama wanamatatizo ya kiafya kwani wataalamu watawapa mbinu za kukabilia na tatizo husika.

''nichukue fursa hii kuwasihi wanahabari wa mkoa wa Rukwa waelimisheni wananchi umuhimu wa kupata huduma za matibabu kwa wakati kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia wananchi kuishi maisha marefu hata kama magonjwa waliyonayo hayana tiba, lakini wataalamu wa afya watawaelekeza namna ya kuishi maisha marefu'' alisema.

Aalisema kuwa katika mkoa huo serikali imeboresha huduma za afya na matibabu yanapatikana kila sehemu kinachotakiwa ni wao kutumia huduma hizo kwa wakati na baadhi yao waachane na dhana ya kuamini waganga wa jadi kwani baadhi yao wamekuwa si waaminifu na wanachangia vifo kwa kuwachelewesha wagonjwa kupata tiba sahihi.

Awali akimkabribisha katibu tawala huyo, mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Bonifas Kasululu alisema kuwa chanjo hiyo ya saratani ya shingo ya kizazi iataanza kutolewa katika mwezi huu wa April na itawalenga watoto wa kike wenye umri wa miaka 14.

Alisema kuwa chanjo hiyo imehakikiwa na shirika la afya duniani (WHO) pia na kuidhinishwa na malaka ya chakula na dawa hapa nchini (TFDA) hivyo ni salama na haina madhara na aliisihi jamii kuhakikisha inawaruhusu watoto wakike wakapate chanjo hiyo.

Kasululu alisema kuwa chanjo hiyo itakuwa ikitolewa daima kama chanjo nyingine  hivyo watoto wa kike wanaofikia umri huo wanapaswa kupata chanjo hiyo ili kuwakinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwani ni miongoni mwa salatani zinazo changia vifo kwa wanawake sambamba na saratani ya matiti.

mwisho

Thursday 19 April 2018

TASAF Katavi kulipa kaya masikini Benk

Na Walter Mguluchuma
Katavi
Mfuko wa  hifadhi ya  Jamii  TASAF  katika   Halmashauri ya  Manispaa ya  Mpanda Mkoani  Katavi umefanikiwa kuzilipa kaya masikini zaidi ya shilingi milioni 67  imeanzisha  utaratibu  mpya kwa  njia ya  mtandao  sambamba  na kuwafungulia  akaunti   Benki  bure.
Afisa  ufuatiliaji  wa  TASAF  katika  Manispaa ya   Mpanda   Twambulile   Solomon alisema  hayo hivi karibuni ambapo  alisema kuwa utaratibu huo   mpya kwa walengwa wa  mfuko huo ulianza  mwezi julai  mwaka  jana   katika   Manispaa hiyo.
Alisema kuwa mpaka sasa utaratibu  huo hapa  nchini  umefanyika   katika   halmashauri 16 kwa  ajiri ya  majaribio  na   kwa  mkoa  wa   Katavi unafanyika  katika Manispaa ya  Mpanda   huku  lengo  likiwa  ni    kutaka  malipo  kwa  njia ya  mtandao  yafanyike  katika  halmashauri zote za  Mkoa wa  Katavi kwa njia hiyo .
Twambulile  alisema   kuwa  katika kipindi cha  kuanzia  Julai  mwaka  jana  hadi  sasa  wamelipa  walengwa malipo yao  kwa  njia ya  mtandao  kiasi cha  shilingi milioni 67,459,500.
 Alifafanua  kuwa    hadi  kufikia  mwezi wa  pili  mwaka  huu   dirisha  lilikuwa  linawalipa  walengwa 344  kwa  njia ya  mtandao  ambapo  kwa  kipindi cha  mwezi  Machi  na April  walengwa  wengine 300  wamejiunga  na  utaratibu huo wa kulipwa  kwa  njia ya  mtandao.
Afisa   ufuatiliaji   huyo wa  Tasaf   alisema kwa  kipindi cha  mwezi  Aprili  wameweza  kuwafungulia  walengwa  71   akaunti  katika Benki ya  CRDB  Tawi  la   Mpanda   bila   malipo  yoyote  na   akaunti zao   hazitakuwa  na   makato yoyote.
 Aliitaja  mitaa  ambayo   walengwa  wamefunguliwa    akauti   Benki  kuwa ni    Kawajense   walengwa  30   Kamakuka  walengwa  14,  Mbugani  Kakese walengwa  walengwa  24 na  Kijiji  cha  Mwamkulu  walengwa  4.
 Mmoja  wa  walengwa  hao  Salome   John   alisema  kuwa    utaratibu huo utawazidi  kuwahakikishia  usalama wa  fedha  zao kuliko ilivyokuwa  awali na  utawapunguzia  usumbufu wa kupanga  foleni   kwenye  malipo.
Mwenyekiti wa  Mtaa wa   Kawajense   Simon  Jumapili   alisema  utaratibu  huo wa malipo kwa  njia ya  mtandao   utawasaidia walengwa  kwenda  kuchukua   fedha  zao  kwa  muda  wanaotaka  wao  tofauti na  hapo  awali  walipokuwa wakipangiwa muda wa  kwenda kuchukua  fedha.
Pia alisema utawafanya  walengwa wa mfuko  kwenda  kuchukua  fedha zao  pindi   wanapokuwa  wamemaliza   shughuli  zao  za  nyumbani  na hivyo kuto athiri muda wa uzalishaji mali.

Mwisho


Wednesday 18 April 2018

Tabibu jela miaka 30 kwa kubaka

Na Walter Mguluchuma
Katavi
MHAKAMA ya  Wilaya ya  Mpanda  Mkoani  Katavi   imemuhukumu mganga mkuu wa  Zahanati ya  Kasekese  Wilaya ya  Tanganyika  Martin  Mwashamba  (27)kifungo cha  miaka  30 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mbaka na kumpa  mimba  wanafunzi wa  dasasa la  sita  wa  shule ya  Msingi  Kasekese mwenye  umri wa miaka 15  jina  lake limehifadhiwa.
Hukumu  hiyo ilitolewa  jana   na   Hakimu  mkazi wa  Mahakama ya  Wilaya hiyo  Odira  Amwol   baada ya  Mahakama  kuridhika  na  ushahidi  uliotolewa  Mahakamani  hapo  na   upande wa  mashitaka.
Awali katika  kesi  hiyo  mwendesha  mashtaka   Mwanasheria wa   Serikali wa  Mkoa wa   Katavi  Gregoli  Mhagwa  alidai   Mahakamani  hapo  kuwa   mshitakiwa  alitenda  kosa  hilo  siku ya  Julai  2  mwaka  jana   Kijijini  hapo.
Alieleza  Mahakamani  hapo siku  hiyo ya  tukio  mshitakiwa  alimbaka   mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa    darasa la  sita wa shule   ya   Msingi  Kasekese mwenye  umri wa  miaka   15 huku  akijua  kufanya  hivyo ni  kosa.
Upande wa  mashitaka   katika  kaesi  hiyo  uliongozwa  na  mwanasheria   Mhagwa ulikuwa na  mashahidi  watano na  miuongoni  mwao  alikuw ni  mwanafunzi   aliyetendewa kitendo hicho na  mshitakiwa   kwa  upande  wake wa utetezi   alikuwa na  mashahidi  watatu .
Hakimu  Amwol kabla ya  kusoma  hukumu  hiyo aliiambia   Mahakama  kuwa  kutokana  na  ushahidi  uliotolewa  Mahakamani  hapo na upande wa  mashitaka   Mahakama  pasipo  kuacha shaka  lolote   imemtia   mshitakiwa  hatiani kwa  mujibu wa kifungu  cha  sheria  130 kifungu  kidogo cha kwanza na chapili  na kifungu  cha  sheria   namba 131 kidogo cha kwanza  cha  kanuni ya  adhabu  sura ya 16  marejeo  ya  mwaka 2002.
Baada ya  kutoa  maelezo  hayo   Hakimu   alitaka  mshitakiwa  kama   anayosababu  yoyote ya  msingi ya   kuishawishi mahakama ili impunguzie   adhabu   basi   anapewa   nasafi hiyo kabla ya kusomewa  hukumu.
Mshitakiwa   Mwashamba Katika  utetezi  wake   aliiomba   Mahakama   impunguzie   adhabu   kwa  kile  alichodai   kuwa   yeye    anafamilia  inayomtegemea   na  pia   ana wadogo  zake  watatu   ambao   anawasomesha  yeye .
  Hata  hivyo  utetezi  huo  ulipingwa  vikali na     mwendesha  mashitaka    mwanasheria wa  Serikali   Gregoli  Mhagwa  ambae   aliiomba  Mahakama  itoe  adhabu  kali  ili  iwefundisho kwa  watu  wengine  wenye  tabia   kama  hiyo .
Hakimu Amwol  baada ya  kusiliza  pande  hizo  mbili za   mashitaka  na  utetezi   aliiambia   Mahakama  kuwa   mahakama  imetowa   adhabu ya  kumuhukumu  mshitakiwa    Tabibu wa  Zahanati ya  Kasekese  Martin   Mwashamba  kutumikia  jela  kifungo cha  miaka  30 kwa  kosa  la  kumbaka    msichana  mwenye  umri wa miaka  16.
  MWISHO

CCM Rukwa yataka miradi ya maendeleo itekelezwe kwa kiwango

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

CHAMA cha Mapinduzi CCM mkoani Rukwa kimeitaka serikali kuhakikisha inashimamia miradi ya maendeleo ili itekelezwe ipasavyo kwani baadhi ya miradi hiyo imebainika kuwa chini ya kiwango.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho Clemence Bakuli alitoa agizo hilo jana alipokuwa katika ziara katika vijiji vya Kisumba,Kasanga pamoja na Kilewani baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa kata ya Kasanga wilayani Kalambo kuwa mradi wa maji uliojengwa katika kata hiyo ulioghalimu shilingi bilioni moja umeshindwa kuwatatulia tatizo la ukosefu wa maji.
Awali wakazi wa vijiji hivyo walimlalamikia katibu huyo wa itikadi na uenezi kuwa katika kata hiyo mwaka 2015 ulitekelezezwa mradi wa maji lakini katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja uliofuata matanki yalianza kuvuja na mabomba kuacha kupitisha maji hali ambayo hawakunufaika na mradi huo.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kasanga Paulo Sichilima alisema kuwa kutokana na wakazi hao kutopata maji inaonekana kuwa mradi huo ulitekelezwa chini ya kiwango ambapo pia kuna kila dalili ya ubadhirifu wa fedha katika mradi huo.
Alisema kuwa wakazi wa kata hiyo walifurahishwa na kitendo cha serikali kuwaondolea kero ya ukosefu wa maji ambao licha ya kuwasababishia adha ya kufuata maji katika umbali mrefu lakini pia walijua wataepukana na kuugua na magonjwa yatokanayo na kutumia maji yasiyo safi na salama kama kipindu pindu.
Naye Maria Sichone mkazi wa kiji cha kilewani kata ya Kasanga alisema kuwa lengo la serikali ya chama cha mapinduzi lilikuwa zuri ambalo ni kumtua ndoo kichwani mwanamke lakini changamoto iliyojitokeza ni baadhi ya watendaji wa serikali pamoja na makandarasi wasiokuwa waaminifu ndiyo wamekuwa wakihujumu jitihada hizo za serikali.
Aliiomba serikali ya mkoa huo kuunda timu ya wataalamu ili wakaukague mradi huo na watakaaobainika kuwa kikwazo katika ufanisi wa mradi huo wasifumbiwe macho wachukuliwe hatua za kisheria kwani zama za kuleana zimepitwa na wakati.
Kwaupande wake Katibu mwenezi wa CCM, Bakuli aliwataka watendaji wa serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inayo tekelezwa mkoani humo ifanyike kwa weledi mkubwa ili wananchi waweze kupata manufaa yaliyo kusudiwa.
Mwisho

Monday 9 April 2018

Mtowisa hawana Chumba cha maiti

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAKAZI wa kata ya mtowisa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamelalamikia kitendo cha kituo cha afya Mtowisa ambacho ni kikongwe kwa zaidi ya miaka 20 kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti kitendo kinachosababisha wagonjwa kukaa na maiti muda mrefu wodini baada ya mtu kufariki.
Wakizungumza mbele ya mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hicho. 
Wakazi hao walimweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa wagonjwa wanalazimika  kulala na miili ya marehumu wardini  huku wakisubiri ndugu wa marehamu kufika na kuchukua miiili hiyo kwa maziko na wakati mwingine maziko ya baadhi ya watu yamekuwa yakifanyika haraka bila kusubiri ndugu wa karibu na marehemu hao kutokana na kuzikwa mapema kwa kuhofia kuharibika kutokana na  kukosekana chumba cha kuhifadhia maiti.
Mmoja wa wakazi hao  Christina Mponji alisema kuwa iwapo kifo kikimfika mgonjwa aliyekuwa amelazwa jirani na kitanda chako hali inayosababisha kupatwa na hofu jambo linalosababisha kutoroka hospitali kabla huduma za matibabu hazijakamilika.
 Naye Msafiri Malema alisema  kuwa kukosekana kwa chumba cha kuhifadhia maiti jambo hilo limetokana na uongozi wa kata kutokuwa na hamasa ya kuwahamasiasha wananchi kujitokeza katika nguvukazi ya ujenzi wa chumba hicho  kitendo ambacho kingeondowa changamoto hiyo.
 Kwa upande wake mkuu wa mkoa huo  Wangabo aliwataka wakazi wa kata hiyo kuanza mara moja  nguvu kazi kwaajili ya ujenzi wa huku akiwaahidi kutoa bati  wa watakapokuwa wamekamilisha ujenzi wa chumba hicho cha akuhifadhia maiti

Mwisho