Sunday 24 September 2017

Marie Stopes walaani mtoto kuozeshwa kwa nguvu

Na Walter Mguluchuma
Katavi
Mratibu  wa  shirika la Marie Stopes Mkoani Katavi Seif Kajiko  amelaani kitendo cha  wazazi wa   mtoto mwenye ulemavu wa  kuongea  na  kusikia (bubu)  ambae  jina  lake  limehifadhiwa(12 ) kuozeshwa kwa nguvu na mwanaume mwenye umri wa miaka 18 ambaye naye ni bubu na hivyo kuendelea kuongeza kwa tatizo la ubakaji pamoja na mimba za utotoni mkoani humo.
Tukio hilo limetokea katika Kijiji  cha  Masigo wilaya ya Mlele  Mkoani humo ambapo binti huyo ameozeshwa kwa nguvu na wazazi wake ambao walidai Kuwa hawezi kupata mtu mwingine wakumuoa isipokuwa mwanaume huyo kwakua naye ni bubu.
Mratibu  wa  Marie Stopes  Kajiko  alilaani  kitendo cha mtoto  huyo kuolewa  kwa  nguvu kwa  shinikizo la wazazi wake  wakati  alipokuwa  akizungumza na  wandishi wa  habari  kwenye  uwanja wa  shule ya  msingi  Kashaulili  Manispaa ya Mpanda wakati wa maadhimisho ya tamasha la  vijana lililowahusisha  wanafunzi wa  shule  kumi za  Sekondari za  Manispaa ya  Mpanda lililoandaliwa na Marie Stopes kwa kushirikiana  na ofisi ya mganga  mkuu wa  mkoa wa Katavi.
Alitoa rai kwa  jamii ya  wananchi wa mkoa wa huo kuachaa  tabia ya kuwaozesha watoto wao wa kike  wakati wakiwa  na  umri  mdogo kwani huwasababishia  madhara mbali mbali ikiwemo vifo  vitokanavyo na  uzazi.
 Alisema takwimu za  mimba  za  utotoni  zimekuwa  zikiongezeka  siku   hadi  siku  Mkoani Katavi na  kusababisha  baadhi ya  wanafunzi wa  kike kukatisha  masomo yao  kutokana  na  kuwa  wajawazito.
Mratibu  huyo wa  Marie   Stopes alieleza  kuwa tasisi hiyo imejipanga kuendelea kutoa     elimu  kwenye  shule  zote za   Seondari ili  kuwaelimisha  juu ya elimu ya uzazi wa  mpango na  madhara ya mimba za utotoni.
Alisema  pamoja  na  jitihada  zinazofanywa na  Marie  Stopes  katika  kukabiliana  na  tatizo la  mimba za utotoni  wamekuwa  wakikabiliana na  changamoto  mbalimbali ikiwemo ya baadhi ya walimu  wa  shule za  Sekondari kukataa kutoa elimu ya  uzazi wa  mpango isitolewe kwa  wanafunzi wao.
Naya Mratibu  wa vijana  washirika la Marie    Stopes  Tanzania  Daniel   Mjema  Emanuel alieleza  kuwa  lengo  kuu la  kongamano  hilo  lilikuwa ni  kutoa  elimu  ya  afya  ya  msingi  na kuwafanya  vijana watambue afya zao.
 Alisema  elimu  hiyo  ya  afya ya  msingi   imetolewa  na Marie  Stopes  wakati wa kongamano  hilo kwa  wanafunzi wa  Sekondari na  wasio   wanafunzi  ambapo pia  wamefundishwa juu ya uzazi wa  mpango na kujikinga na  maambukizi ya VVU.
Kwa  upande wake  mgeni rasmi wa kongamano hilo  Kaimu katibu  tawala wa  mkoa wa  Katavi  Willbard  Marandu  alitoa  wito  kwa  wanaume  wote wa  mkoa wa huo kuwa  bega kwa  bega  katika kushirikiana na wake zao  katika  swala  la  uzazi wa  mpango.
 Alisema imekuwa  ni  tabia ya  baadhi ya  wanaume  kuwazuia  wake  zao katika  swala  la  uzazi wa  mpango kwa madai kuwa  mwanamke kazi yake ni kuzaa tu.
Naye   Velinancia Godwin  mwanafunzi wa  shule ya  Sekondari ya  Wasichana ya  Mpanda alisema kuwa   mimba za utotoni  zimekuwa zikisababisha   wanafunzi wa  kike  kushindwa kupata elimu waliyoitarajia .
Aliongeza Kuwa mimba  za utotoni pia zimekuwa   zikisababisha  hasara kwa  wazazi  wa  watoto  na  taifa kutopata wataalamu   mbalimbali.
Mwisho

No comments:

Post a Comment