Gurian Adolf
Kalambo
SERIKALI
mkoani Rukwa imewataka waandishi wa habari mkoani humo kuyaandika na
kuyatangaza mambo mazuri na changamoto zilizopo bila kuhofia mtu yeyote
kwani maendeleo ya mkoa huo yatapatikana kwa kuyatangaza mambo yaliyomo
katika mkoa huo bila hofu.
Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo
aliwaambia waandishi wa habari wa mkoa huo jana wakati akizindua zoezi
la upandaji miti milioni sita lililofanyika juzi katika mji wa Matai
wilayani Kalambo.
Alisema kuwa waandishi wa habari ni wadau
wakubwa wa maendeleo ya mkoa huo hiyo wanawajibu wa kuandika mambo
mazuri na mabaya yaliyopo katika mkoa wa Rukwa kwani kushindwa na
kufanikiwa kwa mkoa huo nao kunawahusu.
Wangabo alisema
kuwa waandishi wa habari wanatumia kalamu katika kuchangia maendeleo
hivyo wajue wanajukumu la kuandika mazuri na changamoto ili mkoa upige
hatua kwani wakikaa kimya mkoa ukikosa maendeleo nao itawagharimu.
''waandishi
wa habari wa mkoa wa Rukwa nawaagizeni andikine vitu vyote
vinavyoendelea katika mkoa wa Rukwa,pigeni picha na tangazeni yote bila
kumuogopa mtu na asiwepo mtendaji ambaye anakataa kuwapa ushirikiano" alisema.
Alisema
kuwa yeye binafsi yupo tayari kuona mkoa wake ukitangazwa kwa mazuri
pamoja na changamoto zake kwani ndiyo fursa ya kupiga hatua,na kazi hiyo
waandishi wanapaswa kuifanya kwa kuzingatia misingi ya taaluma yao.
Mkuu
huyo wa mkoa aliwataka waandishi wa habari kutembea vijijini kuandika
habari za uharibifu wa mazingira pamoja na kuhamasisha wananchi wajitume
katika kilimo cha kisasa na ufugaji wenye tija kwani mkoa huo unahitaji
maendeleo.
Awali akimkaribisha mkuu huyo wa mkoa, mkuu wa
wilaya ya Kalambo Juliath Binyura alisema kuwa wananchi wa wilaya ya
Kalambo wamejipanga katika kutekeleza zoezi la upandaji miti kwani
wanatambua kuwa miti ni uhai.
Alisema kuwa halmashauri ya
wilaya hiyo ipo tayari kuwadhibiti watu watakao baininika kuharibu
mazingira kwakuwa serikali inatumia fedha nyingi na muda hivyo ni lazima
waone thamani ya miti.
Binyura alisema kuwa kwakuwa mkuu
wa mkoa amekwisha zindua kampeni ya upandaji miti wananchi wameipokea na
wanahakikisha watafikia lengo kwa asilimia mia moja kwani wao ni
wakulima na wanahitaji mvua ambayo haiwezi kupatikana bila kuwepo
misitu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment