Friday 9 March 2018

lishe tatizo Rukwa


Na Gurian Adolf
Sumbawanga
PAMOJA na kuwa mkoa wa Rukwa ni mmoja kati ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula hapa nchini lakini watoto mkoani  humo wanaongoza kwa utapiamlo na udumavu hapa nchini ambapo umefikia kiwango cha asilimia 56.3 huku kiwango cha kitaifa ni asilimia 36.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Kaimu katibu tawala wa mkoa huo Albinus Mgonya wakati akizungumzia hali ya lishe katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa RCC kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Alisema kuwa watoto katika mkoa huo wanakabiliwa na hali mbaya ya utapiamlo na udumavu kiasi kwamba imekuwa ikisababisha hata wanafunzi kutofanya vizuri katika masomo yao.
Alisema kuwa pia kuwepo kwa changamoto ya lishe katika mkoa huo kumesababisha kuwepo kwa tatizo la upungufu wa uzito kwa watoto ambapo takwimu zinaonesha kuwa mkoa huo umefikia wastani wa asilimia 23 wakati kiwango cha kitaifa ni asilimia 14.
Mgonya alisema kuwa hali hiyo imesababisha kuwepo kwa ukondefu kwa watoto katika mkoa huo ambao umefikia kiwango cha asilimia5.3 wakati kiwango cha kitaifa kikiwa ni asilimia 5.
Katika kikao hicho afisa elimu wa mkoa wa Rukwa Nestory Mroka alisema kuwa ufaulu wa wanafunzi wa sekondari katika mkoa huo ni wastani wa daraja la nne ambapo katika matokeo ya mtihani uliopita wa taifa wa darasa la nne mkoa huo ulishika nafasi ya 179 kati ya shule 185 ambazo wanafunzi wake walisajiliwa kufanya mtihani huo.
Alisema kuwa iwapo mkoa huo unataka kuongeza ufauru kwa wanafunzi ni lazima elimu ya lishe itolewe kwani ni miongoni mwa sababu zinazochangia mkoa huo kuwa na matokeo mabaya katika mitihani ya sekondari na shule za msingi.
Aidha katika kikao hicho mmoja wa wajumbe kutoka shirika la Plan International  Gasper Materu alisema kuwa nilazima suala ma afisa lishe wajikite katika suala zima la kutoa elimu kwani hata nia ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda inaweza kukwama iwapo wananchi watakuwa na afya mbaya kwasababu ya kutokuwa na lishe ya kutosha.
Alisema kuwa wataalamu wa kufanya kazi katika viwanda hivyo ni lazima wapate elimu na iwapo ufaulu wao utakuwa hafifu kutokana na lishe mbaya basi nia ya serikali inaweza isifikiwe kutokana na tatizo la lishe.
Naye mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao cha RCC aliwaagiza maafisa lishe mkoani humo kuhakikisha kuwa wanakabiliana na hali hiyo kwakuwa mkoa huo unavyakula vya kutosha changamoto iliyopo ni wananchi hawajui wale chakula kwa namna gani ili tatizo hilo liishe.
mwisho

No comments:

Post a Comment