Wednesday 14 March 2018

Madarasa bado ni changamoto Rukwa

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MKOA wa Rukwa bado unakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo jumla ya vyumba 4,226 vinakitajika ili  kumaliza tatizo hilo.
Akizungumza hivi karibuni afisa elimu mkoa huo Nestory Mroka alisema kuwa mahitaji hayo yamekuwa yakisababisha mkoa huo kutopiga hatua katika mafanikio ya elimu.
Alisema kuwa ili wanafunzi waweze kufanya vizuri katika masomo yao ni lazima kuwe na miundombinu mizuri walimu wakutosha,vitabu pamoja na walimu lakini kama kuna mapungufu kati ya hayo mambo hata ufaulu hauwezi kuwa mzuri.
Mroka alisema kuwa kutokana na changamoto hizo jitihada za makusudi zinahitajika katika kulimaliza tatizo hilo pamoja na mengine ili kuweza kuinua ufaulu wa wanufunzi katika shule za msingi pamoja na sekondari ambapo mpaka sasa ufaulu katika kidato cha nne ni wastani wa daraja la nne.
Afisa elimu huyo alisema kuwa yeye binafsi amejitahidi kuhakikisha anawasimamia walimu ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo ikiwamo ni pamoja na kuwepo kazini kwa muda muafaka sambamba na kufundisha kwa juhudi zote ili idara ya elimu iweze kuwa ya mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri mkoani humo.
Kwaupande wake mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo aliziagiza halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha zikuja na  mikakati ya kumaliza tatizo hilo pamoja na kwamba limeongezeka baada ya serikali ya awamu ya tano kuja na sera ya elimu bure.
Alisema kuwa mafanikio yanakuja na changamoto zake lakini sio sababu ya kulalamikia mafanio kilichopo ni kuzikabiri changamoto hizo kwani hivi sasa kila mtoto mkoani humo awe wa tajiri ama masikini anauhakika wa kupata elimu tofauti na miaka ya nyuma.
‘’ninakila sababu ya kumpongeza muheshimiwa raisi John Magufuli kuamua serikali yake kutoa elimu bure kwani hivi sasa kila mtoto wa mkoa huu anauhakika wa kupata elimu kwakuwa inatolewa bila malipo hivyo ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anakwenda shule hata kama hana sare’’ alisema
Wangabo alisema kuwa huu ni wakati wa serikali,wazazi,wadau wa elimu na wadau wengine wa maendeleo  kushirikiana katika kumaliza changamoto hiyo kwani wakisubiri serikali peke yake ifanye kazi hiyo mkoa utachelewa kupiga hatua katika elimu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa hivi sasa serikali inajikita katika uchumi wa viwanda lazima pia kuhakikisha kuwa elimu haibaki nyuma na mzizi wa kufikia mafanikio hayo ni kuwekeza vizuri katika elimu kwani huko ndiko watapatikana wataalamu watakao fanya kazi katika viwanda hivyo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment