Na Gurian Adolf
Sumbawanga
MKUU wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amewaijia juu
watendaji wa serikali mkoani humo kutokana na kuwa na tabia ya kuwasilisha
takwimu zisizo na mabadiriko katika vikao mbalimbali kwani kitendo hicho
kinaonekasha ni wavivu wa kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza
katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo hivi karibuni, Wangabo
alisema kuwa tangu amefika amekuwa akipewa taarifa ambazo takwimu
zake hazibadiriki kwa kuonekana kupungua ama kuongezeka kwa jambo
wanalowasilisha.
Alisema kuwa alipopangiwa teuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo na
kupangiwa kazi aliongoza kikao cha kwanza cha RCC na alielezwa kuwa katika mkoa
huo kunachangamoto kubwa ya mimba kwa wanafunzi ambapo taarifa hiyo ilieleza
katika kipindi cha Januari mpaka Juni mwaka jana kuna wanafunzi 325 waliopata
ujauzito na hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyehukumiwa kwa kosa hilo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa taarifa hiyo ilieleza kuwa
katika kipindi cha juni mpaka desemba mwaka jana takwimu zilionesha kuwa bado
idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito iko vilevile hakuna ongezeko wala
kupungua.
Wangabo alisema kuwa hivi sasa taarifa iliyotolewa katika
kipindi cha januari mpaka mwezi machi mwaka huu inaonesha kuwa kunamimba kwa
wanafunzi wa shule za msingi 37 na sekondari 288 ambapo jumla yake ni 325
ambapo hakuna tofauti yoyote tangu alipoanza kupewa taarifa ya suala hilo.
Alisema kuwa kinacho onekana watendaji wa mkoa huo wamekuwa
wakinakiri taarifa ileile na kuiwasilisha katika vikao bila kufanyia
marekebisho hali inayoonesha ni uvivu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwenyekiti huyo wa RCC alisema kuwa yeye binafsi amefanya
jitihada za kutosha kutoa elimu kuhusiana na suala la mimba lakini takwimu
hazibadiriki hali inayosababisha agundue kuwa kunauzembe katika kuwajibika kwa
watendaji hao.
Katika kikao hicho baadhi ya wajumbe walishangazwa mkoa huo
kuwa na viwanda 901 lakini bado wananchi wake ni masikini kitu ambacho walisema
kuwa nilazima wajitafakari kwakuwa haiwezekani mkoa kama warukwa kuwa na
viwanda vyote hivyo lakini wananchi ni masikini.
Mwanasiasa mkongwa Chrisant Mzindakaya alisema kuwa lengo la
serikali kujikita katika uchumi wa viwanda ni zuri na lina nia ya kuwakomboa
wananchi kutoka katika umasikini lakini changamoto ni watendaji wa serikali
ambao wamekuwa ni mabingwa wa kuzungumza bila vitendo.
Alisema kuwa mkoa huo umekuwa na mikakati mingi mizuri kwa miaka
mingi lakini tatizo ni namna ya kuitafsiri mikakati hiyo katika vitendo ili
iweze kufanikiwa na wanachi wa mkoa huo waweze kupiga hatua na kuwa na maisha
bora.
Pia alisema kuwa jitihada zifanyike za kushawishi wawekezaji
wawekeze viwanda vikubwa ambavyo vitatoa ajira nyingi kwa wakazi wa mkoa huo
tofauti na hivi sasa viwanda vilivyo vingi ni vyerehani ambavyo vinaajiri mtu
mmoja ndiyo maana pamoja na kusema kuwa mkoa wa Rukwa unaidadi kubwa ya viwanda
lakini bado wananchi wake ni masikini na wanakabiliwa na tatizo la ajira.
Mwisho
No comments:
Post a Comment