Monday 19 March 2018

Watoto wa kwenye mazingira magumu wawakera madiwani

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
BARAZA la madiwani la halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa limeviomba vyombo vya usalama vishirikiane na idaya ya uhamiaji  kuwakamata na kuwarudisha nchini kwao watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao wametoka katika nchi jirani za Zambia na  Congo DRC.
Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Justine Malisawa alisema hayo hivi karibuni wakati akiongoza kikao cha baraza hilo baada ya wajumbe kulalamikia kuongezeka kwa watoto ambao ambao wamekuwa kero na wanajihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo uporaji.
Alisema kuwa hivi sasa mji wa Sumbawanga unakabiliwa na ongezeko la watoto wanaishi katika mazingira magumu ambao baadhi yao wanatoka katika nchi jirani ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu pamoja na ubakaji.
Malisawa alisema kuwa baada ya kubaini ongezeko la watoto hao halmashauri yake ilianza kuchukua hatua ambapo ilibaini baadhi ya watoto hao wanatoka katika nchi za Zambia na Congo DRC lakini baadhi yao wanatoka katika mikoa jirani na mkoa wa Rukwa.
‘’Ndugu zangu madiwani,hata mimi nakili kuwa watoto hawa ni bomu linalosubili kulipuka, baada ya jitihada za kuwafuatilia kujua tatizo ninini mpaka wanaongezeka kwa kasi kubwa tulibaini wengine wanatoka nchi jirani za Zambia na Congo DRC hivyo tunaomba vyombo vya usalama vishirikiane na idara ya uhamiaji warudishwe kwao’’ alisema.
Mmoja wa madiwani hao Vitalis Ulaya alisema kuwa watoto hao wanazidi kuongezeka kila kukicha katika mji wa Sumbawanga hali ambayo ni hatari kwakuwa hakuna jitihada za kutosha za kuweza kukabiliana na wimbi la ongezeko hilo.
Alisema kuwa wengi wa watoto hao wanazurula nyakati za mchana  wakiokota vitu majalalani na kuomba hela kwa wapiti njia na nyakati za usiku wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu hali inayosababisha amani kutoweka.
Naye Ester Mpelele mjumbe wa baraza hilo alisema kuwa watoto hao wamekuwa ni changamoto kubwa kwa wanawake kwani hivi sasa huwezi kutembea pekeyako nyakati za jioni na usiku hali ambayo aliiomba serikali kuingilia kati jambo hilo.
Aliwaomba wazazi katika Manispaa hiyo ya Sumbawanga kuwajibika katika malezi ya watoto wao kwani kitendo cha kuwaacha bila kuwapa huduma za msingi ikiwemo elimu wanawaandalia maisha mabaya ya baadaye na watakuja kuisumbua jamii kutokana na kushindwa kuwajibika kwao.


Mwisho

No comments:

Post a Comment