Thursday 22 March 2018

Zambia yaondoa marufuku

Na Gurian Adolf
Kalambo

WAVUVI wa samaki katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameishukuru serikali ya Zambia kwa kuondoa marufuku ya biashara ya samaki katika nchi hiyo ambayo ilikuwa imewekwa kwa takribani wiki mbili kutokata na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindu pindu nchini humo.
Shukrani hizo wamezitoa jana wakati wakizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili ambapo walisema kuwa marufuku hiyo ilikuwa imewaathiri kiuchumi kutokana na kuwa soko kubwa la samaki wanaovuliwa katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa nchini Tanzania ilikuwa ikitegemea soko katika nchi hiyo jirani.
Mmoja wa wavuvi hao ambaye ni mkazi wa Kasanga wilayani humo  aliyejitambulisha kwa jina la Richard Sichone alisema kuwa serikali ya nchi hiyo imeondoa marufuku hiyo baada ya jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo kuonesha mafanikio ambapo hivi sasa wavuvi hao wameanza kuuza samaki wao nchini Zambia.
Alisema kuwa katika kipindi ambacho serikali ya nchi hiyo ilikuwa imezuia uvuvi katika nchi hiyo pamoja na biashara ya samaki kutoka nchi za Tanzania na Congo DRC kutokana na kipindu pindu walikabiliwa na ugumu wa maisha kwakuwa walikuwa wakiuza samaki kwa bei ya hasara tofauti na walipokuwa wakiuza nchini Zambia.

Sichone alisema kuwa katika nchi hiyo kuna makampuni 12 ambayo yamekuwa yakinunua samaki tani 1,200 kila siku ambapo kilo moja wavuvi wamekuwa wakiuza kwa shilingi 5,000 za kitanzania lakini katika kipindi ambacho nchi hiyo ilipiga marufuki ya biashara ya samaki soko lilishuka ambapo walikuwa wakiuza kilo moja kwa shilingi 1,500 na kulikuwa kuna kampuni moja tu ya Premji iliyopo Kasanga ambayo ilikuwa inauwezo wa kununua tani nane za samaki.
Naye Michael Sichilima mvuvi wa kijiji cha Kapele katika mwambao wa ziwa Tanganyika wilayani kalambo alisema kuwa kitendo ilichokifanya serikali ya Zambia ni chakupongezwa kwani kimetoa fursa ya biashara si tu kwa wavuvi wa nchini humo lakini pia wavuvi kutoka nchi jirani watanufaika.
Aliwasihi wavuvi kutoka mkoani wilayani humo kuheshimu sheria za nchi hiyo pindi wanapokwenda kufanya biashara ya samaki ili wasije kugeuka kero na kusababisha kuharibu uhusiano wa kibiashara na u dugu baina ya wanachi wa nchi hizo mbili kwakua mahusiano yao ni ya kihistoria na yanafaa kulindwa kwa maslahi ya waafrika wote.
Mwisho

No comments:

Post a Comment