Tuesday 13 March 2018

Wavuvi walia samaki soko la samaki kudoda

Na Gurian Adolf
Kalambo

WAVUVI wanaofanya shughuli katika ziwa Tanganyika wilayani Kalambo mkoani Rukwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi baada ya serikali ya nchini Zambia kupiga marufuku shuguli za uvuvi nchini humo pamoja na kuingiza samaki wabichi kutoka nchi za Tanzania na Kongo kutokana na kuibuka kwa ugonjwa wa kipindu pindu.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wavuvi hao walisema kuwa wanakabiliwa na hali ngumu kwakuwa zaidi ya asilimia 85 ya mauzo yao ya Samaki wabichi wanategemea soko la Mpulungu nchini Zambia.
Mmoja wa wavuvi hao Kennedy Sinyangwe alisema kuwa katika nchi hiyo kuna makampuni 12 ambayo yanauwezo wa kununua tani 1,200 za samaki kila siku ambapo kilo moja wavuvi wamekuwa wakiuza kwa shilingi 5,000 za kitanzania lakini tangu nchi hiyo ipige marufuki hiyo wamejikuta wanahali ngumu kwakuwa hawana soko la samaki.
Alisema kuwa changamoto iliyopo katika nchi ya Tanzania hakuna makampuni makubwa ya kununua samaki ambapo mpaka hivi sasa kuna kampuni moja ya Premji iliyopo eneo la Kasanga ambayo inauwezo wa kununua samaki kiasi kidogo ambacho ni tani 8 kitendo kilichosababisha wakose soko.
Sinyangwe alisema kuwa katika mji wa kasanga serikali ya Tanzania imejenga soko kubwa la samaki na lakisasa kwa gharama kubwa ya shilingi milioni 800 lakini inachumba kimoja tu cha baridi cha kuhifadhia samaki chenye uwezo wa kuhifadhi tani 20 ambazo ni kidogo ukilinganisha na zinazo vuliwa kwa siku katika ziwa hilo.
Alisema kuwa tangu nchi hiyo imepiga marufuku shughuli za uvuvi katika nchi yao na kuingiza samaki wabichi kutoka katika mataifa jirani soko la samaki limeshuka ambapo hivi sasa wavuvi wanalazimika kuuza kilo moja ya samaki chini ya shilingi 1,000 kitendo kinacho wafanya wakabiliwe na hali ngumu.
Naye Peter Sichilima mvuvi wa samaki katika ziwa Tanganyika eneo la Samazi mkoani Rukwa aliiomba serikali ya Tanzania kuhakikisha inakamilisha miundombinu katika soko la kuuzia samaki ili waache kutegemea soko la nchini Zambia kwani limekuwa na changamoto nyingi.
Alisema kuwa serikali inakosa mapato iwapo biashara ya samaki ingefanyika nchini mwetu kwakuwa wageni wangekuwa wanalazimika kuja kununua samaki na wanapoingia wangekuwa wanalipa tozo mbalimbali tofauti na hivi sasa ambapo wao wanalazimika kulipa tozo hizo nchini Zambia kwakuwa ndiko soko liliko.
Naye Philipo Siulapwa mkazi wa Kasangana alisema kuwa iwapo kwakuwa hivi sasa serikali imejikita katika uchumi wa viwanda ni vizuri sasa vikaanzishwa viwanda vya kusindika samaki ili iwe rahisi kuwahifadhi na kuwatafutia soko la kimataifa ambalo halina changamoto kama kutegemea kuuza samaki wabichi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment