Na Gurian Adolf
Sumbawanga
CHUO
cha ualimu cha Sumbawanga kilichopo mkoani Rukwa huenda kikasitisha
kupokea wanafunzi kwaajili ya kujiunga na chuo hicho baada ya Kanisa
katoliki jimbo la Sumbawanga kudai majengo yake ambayo yanayotumiwa na
serikali kwaajili ya kusomea wanafunzi wa chuo hicho kutokana na
kutopewa majengo mengine kama walivyo ahidiwa miaka ya nyuma.
Mkuu
wa mkoa huo Joachim Wangabo akizungumza katika kikao cha kamati ya
ushauri ya mkoa RCC hivi karibuni alisema kuwa majengo yanayotumiwa na
chuo hicho ni mali ya kanisa katoliki ambalo liliyatoa kwa serikali
mwaka 1974 ili yatumike kama ofisi za mkoa kutokana na mkoa huo ulikuwa
mpya na ulikuwa hauna ofisi.
Alisema kuwa kipindi hicho
alikuwepo Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Sumbawanga marehemu Karolo
Msakila ambaye aliombwa majengo hayo ili yatumike kama ofisi za mkoa huo
ambapo alikubari na kuiazima serikali na ofisi za mkoa huo zilikuwa
hapo.
Ilipofika mwaka 1989 serikali ya mkoa huo ukawa
umejenga ofisi zake lakini haukuyarudisha majengo hayo kwa mmiliki wake
ambaye alikuwa anataka kufungua chuo cha kilimo badala yake serikali
ilianzisha chuo cha ualimu bila makubaliano yoyote.
Baada
ya muda mrefu kanisa katoliki liliyahitaji majengo yake ambapo serikali
ya mkoa uliahidi kulipatia majengo yalikuwa yakitumika na kampuni ya
ujenzi ya barabarakwa kiwango cha lami kati ya Sumbawanga-Tunduma,
lakini hata hivyo serikali ya mkoa huo haikulipa kanisa majengo hayo
badala yake yakatumika kuanzisha tawi la chuo cha Sayansi cha
Mbeya(MUST).
Kutokana na hali hiyo kanisa katoliki
lilihoji kuhusu hatma ya majengo yao ambapo serikali ya mkoa iliahidi
tena kulipa majengo ya kambi ya ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Mpanda
yaliyopo katika eneo la Makutano mjini Sumbawanga,lakini napo haikuwa
hivyo baada ya serikali kuweka ofisi za Tanroad mkoa na hivyo kanisa
kukosa majengo hayo.
Baada ya kushindikana mara mbili zote
kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga lilikutana na uongozi wa serikali ya
mkoa ambapo lilisema halitaki tena kupewa majengo mengine bali wanataka
majengo yao kwakuwa kanisa hilo limevumilia na kufikia mwisho.
Kutokana
na kujuwa kuwa majengo hayo si mali ya serikali kwa muda mrefu yalikuwa
hayafanyiwi ukarabati mpaka hapo NACTE ilipotishia kukifunga chuo hicho
kutokana na kuwa kimechakaa ndipo serikali ya mkoa ilipoliomba tena
kanisa katoliki liwape muda ambapo lilitoa miaka mitano wanafunzi hao
wawe wameondoka katika majengo yao na serikali ya mkoa iwe imejenga chuo
chake na wakabidhi majengo kwa kanisa hilo liendelee na matumizi
waliyokusudia wakati yakijengwa.
Mkuu wa Mkoa wangabo
aliwaambia wajumbe wa kikao cha RCC serikali ya mkoa imewasiliana na
tasisi ya Jumuiya ya Maendeleo mkoani Rukwa (JUMARU) ambapo imetoa ardhi
katika kijiji cha Pito nje kidogo ya mji wa Sumbawanga ambapo yalikuwa
mashamba ya bega kwa bega yanayomilikiwa na kijiji hicho ambapo serikali
ya mkoa imeanza mchakato wa kutafuta fedha kwaajili ya ujenzi wa chuo
cha ualimu Sumbawanga.
Alisema kuwa lengo la serikali ya
mkoa ni kujenga chuo hicho na kwakuwa eneo ni kubwa kijengwe pia chuo
kikuu ambacho kitamilikiwa na serikali ambacho kitakuwa makao yake makuu
mkoani Rukwa.
Baada ya taarifa hiyo kutoka kwa mwenyekiti
huyo wa RCC mkoa wa Rukwa wajumbe wa kikao hicho walishauri kuwa
nivizuri pia ukarabati ukaendelea kufanyika katika chuo hicho kinacho
tumika hivi sasa kilichopo eneo la Kantalamba ili NACTE wasisitishe
kuwapangia wanafunzi kwakua miaka mitano waliyo azimwa na kanisa hilo
bado ni kipindi kirefu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment