Thursday 8 March 2018

Waziri Ummy Mwalimu atoa siku saba kwa wanawake kurejesha mikopo



Na Gurian Adolf
Sumbawanga

WAZIRI wa afya,maendeleo ya jamii,jinsia na watoto Ummy Mwalimu ametoa siku saba kwa wanawae wote waliochukua mikopo katika benki ya wanawake wawe wamerudisha vinginevyo waanze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa mgeni rasmi akihutubia katika sherehe za wanawake zilizofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
Alisema kuwa benki ya wanawake imekuwa ikitoa mikopo lakini kitu cha kusikitisha baadhi yao wamekuwa na tabia ya kurudisha mikopo hiyo kitendo kinachowanyima fursa wanawake wengine ya kunufaika na mikopo hiyo.
Waziri Ummy alisema kuwa anatoa siku saba wanawake wote wanaodaiwa mikopo na walipaswa kuwa wamesharudisha wahakikishe wamerudisha katika kipindi cha siku saba tofauti na hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia waziri huyo alitumia fursa hiyo kumuomba waziri wa utawala bora George Mkuchika kuwafikisha mahakamani wanawake wote waliokuwa watumishi wa benki hiyo ambao walifanya ufisadi kwani wamekuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya wanawake wenzao.
Alisema kuwa benki hiyo iliajiri wanawake ikiamini kuwa watakuwa na uchungu na benki yao ambapo wataisimamia vizuri ili iweze kuendelea zaidi na kuwa msaada lakini kinyume na matarajio wanawake hao ndio wamefanya ufisadi na kuendelea kuwakwamisha wanawake wenzao.
‘’nitumie fursa hii kumuomba kaka yangu waziri wa utawala bora Geore Mkuchika kuwafikisha mahakamani wanawake wote ambao walikuwa watumishi wa benki ya wanawake na kisha kufanya ufisadi kwani hawa ni adui wa wanawake wenzao’’ alisema.
Waziri huyo alitumia fursa hiyo kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kufikiria upya katika suala la kutoa mikopo kwa makundi ya wanawake na vijana kwani mikopo inayotolewa haiendani na uhalisia kwakuwa haiwezekani kikundi cha watu 15 wakakopeshwa shilingi 300,000 halafu ukategemea watapiga hatua.
‘’Naagiza wakurugenzi wote nchini kutazama upya suala la mikopo ya wanawake na vijana inayotoka katika asilimia tano ya mapato ya halmashauri kuwakopesha mikopo itakayowasaidia kufanya shughuli na kupata faida kwasababu utakuta kikundi cha watu 15 wanapewa shilingi 300,000 fedha ambazo hazitoshi walau ziwe hata shilingi milioni kumi kwa kikundi walau wanaweza kuzizalisha’’ alisema.

Pia aliitaka jamii kubadili mtazamo wa kufikiria kuwapelekea misaada ya chakula na nguo watoto yatima na wanaoishi katika  mazingira magumu badala yake waanze kuwalipia huduma ya afya kupitia Toto Afya Kadi kwani miongoni mwa changamoto zinazo wakabiri watoto hao ni pamoja na huduma za afya.
Naye mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Aesh Hilary alimuomba waziri huyo magari ya kubebea wagonjwa ambapo wanawake hasa wajawazito ambao wanahitaji huduma za dharula kwakua mkoa huo wa Rukwa unachangamoto ya upungufu wa magari hayo.
Baada ya kulisikia ombi hilo waziri huyo wa afya aliahidi kutoa magari mawili ya kubebea wagonjwa(ambulance) ambapo moja litakuwa kwaajili ya hospitali ya rufaa ya Sumbawanga na jingine aliagiza kuwa kitafutwe kituo kilichopo mbali na mjini ndiyo kipatiwe gari hilo.
Naye mkuu wa Kalambo Julieth Binyura alimshukuru waziri Ummy kwa kukubali kufika mkoani Rukwa na kusherekea na wanawake wa mkoa huo kwani amewapa hamasa na kuwasaidia kutatua changamoto nyingi ambazo zitawafanya kuongeza ari katika utendaji kazi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment