Tuesday 13 March 2018

Bavicha wanena

Na Gurian Adolf
Sumbawanga.

Baraza la vijana la Chadema (Bavicha) limeitaka Serikali kutumia gharama yoyote kulinda amani ya nchi inayo onesha dalili ya kutoweka kutokana na kukithiri kwa vitendo vya mauaji ya kinyama na utekaji unaofanywa watu wasiojulikana.


Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu alisema hayo juzi wakati wa akifungua kongamano la vijana lilolenga kuwapa elimu wanachama wake  kuhusu wajibu wao katika siasa za sasa ambalo liliandaliwa na Bavicha mkoa wa Rukwa.

Alisema hali ya kisiasa hivi sasa hapa nchini ni tete kutokana kushamiri kwa vitendo vya utekaji na mauaji ya kinyama yanayofanywa na watu wanaodaiwa kutojulikana huku serikali ikiwa haijavalia njuga vya kutosha katika kudhibiti vitendo hivyo.

Makamu huyo mwenyekiti alisema imefika wakati sasa serikali kutumia gharama yoyote ili kulinda amani ya taifa hili iliyoasisiwa na Baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere ambaye katika utawala wake na zile zilizopita hawakukubali kuona amani ikitiwa doa.

"Amani ni tunu ya taifa hili....... kwa hiyo sisi kama wanasiasa tulazima tuhakikishe nchi inakuwa na amani asitokee mtu wa kutaka kutia doa amani yetu na sisi tukamwangalia......kwa hiyo serikali ina wajibu wa kukomesha vitendo hivi vya uvunjifu wa amani, utekaji na mauaji ya kinyama ya watu" alisema

Awali, Mwenyekiti wa Bavicha mkoa wa Rukwa, Aida Khenan aliwataka vijana wa Chadema mkoani humo kulitumia kongamano hilo ili kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto za kisiasa ambazo zimekuwa zikiathiri ustawi wa vyama vya upinzani hapa nchini.

Khenan ambaye pia mbunge wa viti maalumu mkoani Rukwa, alisema kuwa,vijana hao wanapaswa kutumia fursa ya kongamano hilo kubaini mbinu mbalimbali za kujiongezea kipato ili waeze kujikwamua kiuchumia na hatimaye kuondokana na umasikini.

Aliongeza kwamba ili vijana waweze kushiriki kikamilifu katika siasa za mageuzi wanapaswa wawe na nguvu ya kiuchumi hivyo makongamano kama hayo yanawapa fursa ya kubaini mbinu mbalimbali za kujiongezea kipato.

Mwisho

No comments:

Post a Comment