Thursday 15 March 2018

Walimu 16 watimuliwa kazi

Na Gurian Adolf
Nkasi

JUMLA ya walimu 16 wamefukuzwa kazi wilayani Nkasi mkoani Rukwa kwa kipindi cha miaka mitatu na wengine 11 wamepewa onyo kali baada ya kubainika wametenda makosa mbalimbali.

Katibu wa tume ya utumishi wa walimu TSC wilayani humo  Richard Katyega aliyasema hayo jana mbele ya kamishina wa tume ya Utumishi wa walimu Taifa, Samwel Koroso ambapo alisema  kuwa katika kipindi hicho  walipokea mashauri 23 na kupelekea walimu 16 kufukuzwa kazi,11 kupewa onyo kali na wengine 5 waliondolewa kazini baada ya kubainika kuwa na vyeti bandia.

Alisema kuwa  katika mwaka wa fedha wa 2016, 2017 na 18  tume hiyo imeweza kusikiliza mashauri hayo na kuyatolea maamuzi ambapo ilifikia maamuzi hayo baada ya kusikiliza mashauri hayo na pasipo kumuonea mwalimu hata mmoja na kutenda haki kwa mujibu wa sheria.

Katyega alisema kuwa tume hiyo sambamba na kuchukua maamuzi hayo pia imekua ikiwahamasisha walimu kufuata maadili ya ualimu kwa uhakika ili wasiweze kukumbana na adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake kamishna wa tume ya TSC Samwel Koroso alionyesha kusikitishwa na vitendo vya  uvunjifu wa maadili kwa waalimu hali inaoyopelekea  kufukuzwa kazi na kuwa wao kama tume ya maadili kwa walimu wataendelea kuwachukulia hatua Walimu wote ambao watakwenda kinyume na maadili ya ualimu

 Aliwataka walimu kwenda sambamba na misingi ya sheria ya utumishi kwa walimu kama inavyowataka na kuongeza kuwa walimu wilayani humo hawanabudi kuzipitia sheria za utumishi wa walimu ili waweze kuishi kwa kufuata sheria hizo zinavyo agiza.

Maofisa  kutoka ofisi ya ya kamishina wa tume hiyo nao waliweza kutoa mada mbalimbali zilizolenga kuwapatia elimu Walimu na kuwakumbusha sheria za utumishi wa walimu,huku walimu kwa upande wao walipata fursa ya kueleza changamoto zinazo wakabili  na zilipatiwa majibu kutokana na maswali waliyokuwa nayo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment