Saturday 26 December 2015

Noah yauwa watatu mtoni

Na Gurian  Adolf

WATU watatu  wamekufa maji  wakiwa wanatoka katika mahemezi ya sikukuu ya Krismasi baada ya gari aina ya NOA walilokuwa wamepanda  kutumbukia katika mto Kilambo wakati likiwa safarini kutoka katika kijiji cha Muze wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa likielekea katika kijiji cha  Majimoto wilayani  Mlele mkoani Katavi.

Kwamujibu wa taarifa kutoka kwa Diwani wa kata ya Muze Kalolo Joseph Ntila alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba  24 majira ya saa 4;20 usiku ambapo gari hilo likiwa na abiria saba lilipoacha njia na kutumbukia katika mto huo.

Alisema kuwa baada ya gari hilo kutumbukia mtoni baadhi ya abiria walifanya jitihada za kujiokoa ambapo walifanikiwa kutoka huku wanawake wawili na mtoto mdogo mmoja walishindwa kutoka ndani ya gari hilo na kufa maji wakiwa ndani ya gari hilo.

Diwani Ntila alisema kuwa baada ya abiria hao kutoka walijitahidi kutoa msaada kwa watu waliokuwa wamebaki ndani ya gari hilo lakini hawakufanikiwa kutokana na maji mengi na walipofanikiwa waliwatoa wakiwa wameshafariki dunia.

Alisema kuwa watu hao bado hawajafahamika majina yao lakini miili ya marehemu hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Muze kwaajili ya kusubiri kutambuliwa ili ndugu zao wakafanye maziko ya watu hao.

Aidha diwani huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga alisema kuwa barabara katika eneo hilo si nzuri hasa nyakati hizi za masika pindi mvua zinaponyesha kumekuwa na utelezi hali iliyosababisha gari hilo kuteleza na kutumbukia mtoni.

Alitoa wito kwa madereva wanaofanya safari kupitia barabara hiyo kuwa waangalifu katika nyakati hizi za masika kwani tahadhari isipochukuliwa huenda watu wakaendelea kupoteza maisha kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment