Tuesday 29 December 2015

Apigwa radi akienda shambani

Na Gurian  Adolf

MWANAMKE  aliyefahamika kwa jina la Grace Nobert (36) mkazi wa kijiji cha Kipundukala katika mamlaka ya mji mdogo wa Namanyere  wilayani Nkasi mkoani Rukwa  amekufa papo hapo baada ya kupigwa radi.

Akizungumza na Nipashe  mume wa marehemu Anord Kaunda alisema kuwa mauti hayo yalimkuta mkewe Desemba 27 majira ya saa 9 alasiri akiwa njiani akielekea shambani.


Alisema tukio la kupigwa radi mkewe huyo  kilitokea muda mfupi baada ya kuagana na mke wake huyo aliyemuaga kuwa anakwenda shambani kupalilia maharage naye mumewe alimuaga kuwa alielekea kanisani katika ibada ya jioni.

Kabla hajafika kanisani alipigiwa simu na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho na kupewa taarifa kuwa  mkewe kafariki taarifa ambazo zilimsababishia mstuko mkubwa.

Baada ya taarifa hizo alielekea eneo la tukio na kushirikiana na majirani zake kisha walimkimbiza hospitali na walipofika madaktari waliwaeleza kuwa mwanamke huyo alifariki dunia palepale alipopigwa na radi.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho Kiliani tinga alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwa marehemu huyo alikutwa na majeraha kifuani na katika eneo la chini ya tumbo na nguo zake zilichanwachanwa na mwili wake ulikuwa mweusi kupita kiasi.

Alisema kuwa polisi walifika eneo la tukio kwalengo la  kujiridhisha kuwa kifo hicho kweli kilitokana na kupigwa  radi na si vinginevyo.

Diwani wa kata hiyo Philipo Kapembwa alisema kuwa katika maeneo hayo kumekuwepo na radi za mara kwa mara ambapo katika siku za hivi karibuni mbuzi kadhaa walikufa baada ya kupigwa na radi.

Alisema kumekuwepo na minong’ono kwa majirani  wa familia hiyo ya kuwapo kwa imani za kishirikina kufuatia tukio hilo lakini wana familia wa marehemu huyo walikataa na kuongeza kuwa kifo hicho kimetokana na mapenzi ya Mungu.

mwisho

No comments:

Post a Comment