Tuesday 29 December 2015

Sangoma anaswa na Nyara za serikali

Na Gurian  Adolf

MGANGA  wa Jadi aliyefahamika kwa jina la Vitus Chomba(42) mkazi wa Sumbawanga mjini mkoani Rukwa anashikiliwa na polisi wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi baada ya kukutwa na nyara za serikali ambazo alieleze kuwa huwa anazitumia wakati wa kutibu na kuroga pindi wateja wake wanapohitaji huduma hizo.

Tukio la kukamatwa kwa tabibu huyo wa tiba mbadala lilitokea Desemba 27 majira ya saa 1;00 za jioni baada ya wakazi wa eneo alilokuwa akiishi kumtilia shaka kutokana na kukutana na watu kwa siri wakati yeye ni mgeni katika eneo hilo.

Akizungumzia tukio hilo afisa mtendaji wa kata ya Nsekwa wilayani Mlele mkoani Katavi Amos Ngozi alisema kuwa alipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa kata hiyo wakieleza kuwa kunamtu ambaye amekuwa akikutana kwa siri kubwa na baadhi ya wakazi wa kata hiyo hali iliyosababisha hofu kwa baadhi ya wananchi.

Alisema baada ya taarifa hizo alitoa taarifa polisi ambapo kwa kushirikiana na polsi hao walivamia katika nyumba anayoishi mganga huyo na kuanza kuifanyia upekuzi na katika beji lake la nguo walikuta kuna Ngozi ya simba, maini ya Swala pamoja na ngozi ya paka pori.

Mtendaji huyo wa kata alisema kuwa vitu vingine walivyomkutanavyo ni nyama ya Sungura, kwato za pundamilia pamoja na mkia wa nyati ambapo alieleza kuwa yeye ni mganga wa jadi na huwa anatumia vitu hivyo wakati wa kutibu ama kuroga kutokana na huduma anayohitaji mteja wake.

Alisema mganga huyo alifika katika kijiji cha Inyonga wilayani humo kwalengo la kufuata wateja wake ambao walikuwa wamemuita awatibu na kuwafanyia zindiko pia kutafuta vitu ambavyo atavitumia katika kutengeneza dawa ambazo anatumia kutibia wateja wake.

Hata hivyo mtendaji Ngozi alisema mganga huyo alichukuliwa na polisi na kushikiliwa katika kituo cha polisi kutokana na kukutwa akiwa na nyara za serikali, kosa la kufanya tiba za jadi wakati hana kibali cha kufanya kazi hiyo.

mwisho.

No comments:

Post a Comment