Thursday 31 December 2015

Majangili wanaswa, waua tembo wanne


Na Gurian  Adolf

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia watu  watatu kwa tuhuma
za kuwakamata na meno ya Tembo yenye thamani ya shilingi milioni 120
ambayo  ni sawa na Tembo wazima wanne .

Watuhumiwa hao watatu waliokamatwa na meno hayo ya Tembo  wametajwa
kuwa ni  Bathromeo Agustino(26) Geofrey Exavery(40)  na  Elias
Mwelela( 40) wakazi wa Mtaa  wa  Aitel Kata ya Uwanja wa Ndege
Manispaa ya Mpanda.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari aliwaambia
waandishi wa Habari  kuwa watuhumiwa hao walikamatwa  Desemba 29
majira ya saa 4 usiku katika Mtaa huo wa Airtel waliko kuwa wakiishi.

Alisema    Askari Polisi  na Askari wa (TANAPA)  wa  HIFADHI  ya Taifa
ya mbuga ya Katavi walipatataarifa za siri kutoka kwa Raia wema  kuwa
katika Mtaa huo kuna  watu wanamiliki  nyara za Serikali.

Kamanda Kidavashari alieleza   kuwa baada ya taarifa hizo kuwa
zimepokelewa  na ufuatiliaji  ulifanyika   katika makazi waliokuwa
wakiishi watuhumiwa hao watatu.

Alisema ndipo siku hiyo ya tukio upekuzi ulipofanyika kwenye makazi ya
watuhumiwa  na katika upekuzi huo watuhumiwa hao walikutwa na meno ya
Tembo vipande 12 vyenye thamani ya shilingi milioni 120  ambayo ni
sawa na tembo wanne hai yakiwa kwenye makazi yao.

Kidavashari aliendelea kueleza  kuwa watuhumiwa mbali ya kukamatwa na
meno hayo ya Tembo pia walikutwa na   mzani mmoja  na Pikipiki aina ya
  Sanya  yenye  Namba za usajiriT.552 CZE.

 Alisema  watuhumiwa  wanaendelea  kushikiliwa na  Jeshi la Polisi
kwa hatua za  upelelezi na watafikishwa Mahakamani  baada ya upelelezi
 utakapo kuwa umekamilika .

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi ametowa onyo kwa Wananchi kuacha
mara moja kujihusisha na biashara  za nyara za Serikali  na biashara
haramu .

Mwisho

No comments:

Post a Comment