Wednesday 6 June 2018

Rukwa kujikita kwenye Alizeti

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

MKOA wa Rukwa umejipanga kwaajili ya kuzalisha zao la alizeti ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula unaotokea mara kwa mara hapa nchini.

Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alisema hayo hivi karibuni wakati anazungumza na balozi wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock ofisini kwake  wakati akiwasilisha ombi la ushirikiano baina ya mkoa wa Rukwa na nchi yake hali itakayo ongeza uzalishaji wa zao la alizeti mkoani humo na kupelekea kuinua kipato cha wakazi wa mkoa wa huo.

alisema kuwa Kwa mwaka 2016/2017 zililimwa hekta 47,862 za alizeti na kupatikana tani 53,470 ambayo ni chini ya kiwango kilichotakiwa kuzalishwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa kwa hekta 47,862 zikilimwa vizuri zinaweza kupatikana tani 119,655 ambayo ni ongezeko la asilimia 55.

Wangabo alisema kuwa nia ya kujikita katika kuzalisha alizeti kwa wingi ni kuzalisha mafuta ya alizeti kwa wingi, kutengeneza ajira na kuongeza viwanda ili kufikia nia ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda.

Alisema kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji Tanzania inatumia Shilingi bilioni 189.6 kila mwaka kununua mafuta ya kula nje ya nchi huku ikizalisha tani 91,000 ambayo ni sawa na asilimia 40 za mafuta hayo tofauti na makadirio ya tani 200,000 hadi 300,000 ya uhitaji wa bidhaa hiyo kwa mwaka kitu ambacho mkoa wa Rukwa umeiona fursa hiyo na hivyo umejipanga kujikita katika kilimo cha alizeti vizuri.

Mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alisema kuwa mkoa unatarajia kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Faida mali ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kukuza zao la alizeti katika Mkoa wa Singida ili kuhamishia ujuzi huo katika Mkoa wa Rukwa.

Kwa upande wake balozi wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock alisema kuwa amefurahishwa sana na mikakati hiyo ya mkoa wa Rukwa kwa kuona umuhimu wa kutafuta zao mbadala la biashara katika Mkoa wa Rukwa ikiwa ni pamoja na kuinua kilimo cha mkoa na kuinua kipato cha wakulima wadogo na hatimae kuwatafutia namna ya kuongeza viwanda vidogo na kuongeza ajira.

Alisema kuwa serikali ya nchi yake ipo tayari kutoa msaada wa hali na mali ili mkoa huo uweze kufikia malengo hayo kitu cha muhimu ni kuendelea na ushirikiano ili mikakati hiyo iweze kufanikiwa na kuleta tija kwa wakulima pamoja na serikali kwa ujumla.
 
Mwisho

No comments:

Post a Comment