Wednesday 6 June 2018

Kipindu pindu chaua 397

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
HALI ya ugonjwa wa kipindu pindu bado ni tete wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo idadi ya wagonjwa imeendelea kuongezeka ambapo hivi sasa imefikia vifo 15 na wagonjwa 397 waliougua ugonjwa huo tangu ulipolipuka tena  Mei 6 mwaka huu.
Mganga mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Fani Mussa akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema kuwa ugonjwa huo bado haujaisha na watu wamekuwa wakiendelea kuugua.
Alisema kuwa mpaka kufikia jana jumla ya watu 397 wameugua kufa na wengine kupona ambapo mpaka hivi sasa kuna wagonjwa  saba ambao bado wapo wodini wakitibiwa ugonjwa huo.
Mganga mkuu huyo alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni wananchi kutofuata kanuni bora za afya hasa kunywa maji yasiyosalama sambamba na kutojisaidia kwenye vyoo.
Alisema kuwa hivi sasa wakulima wanavuna mpunga na maji wanayotumia kwa kunywa ni ya kwenye majaruba ambayo si salama kiafya kwakuwa hayajachemshwa na baadhi yao wakijisaidia porini.
Dkt Mussa alisema kuwa idara ya afya inajitahidi kutoa elimu lakini bado wananchi hawafuati taratibu za kujikinga na ugonjwa huo licha ya kwamba sheria kali pia zinatumika lakini bado ugonjwa huo unaendelea.
Alisema katika kipindi cha November mwaka jana ugonjwa huo ulilipuka na ulidhibitiwa ilipofika mwezi March mwaka huu lakini bila matarajio ugonjwa huo ulilipuka tena mwezi mei mwaka huu na katika siku si nyingi umeua watu 15 tofauti na mwaka jana ambapo watu 7 ndiyo waliopoteza maisha.
Mwisho

No comments:

Post a Comment