Saturday 2 June 2018

Wanafunzi Nkasi sasa wapeana mimba

Na Gurian Adolf
Nkasi

IMEELEZWA vitendo vya kupeana mimba baina ya wanafunzi kwa wanafunzi vimeshika kasi katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa hali inayochangia kukwamisha jitihada za kukabiliana na mimba za utotoni wilayani humo.

Hayo yalielezwa jana na hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya hiyo Ramadhan Rugemalila wakati akitoa mada katika mkutano wa siku moja wa kupitia utekelezaji wa mpango kazi wa kuanzia mradi wa kuzuia mimba za utotoni unaofadhiriwa na shirika la kimataifa la Plan International  wa mwezi Januari hadi Juni na kuandaa mpango kazi wa mwezi Julai hadi mwezi Desemba mwaka huu.

Alisema kuwa kutokana na elimu inayotolewa kwa wananchi pamoja na adhabu kali za kisheria zinazotolewa hivi sasa vitendo vya watu wazima kuwapa mimba watoto wa kike vimepungua badala yake vimeibuka vitendo vya kupeana mimba wanafunzi kwa wananfunzi.

Rugemalila alisema kuwa hivi sasa mahakani zimejaa kesi za mimba kwa wanafunzi ambazo idadi kubwa ni wanafunzi wamekuwa wakipeana mimba hali ambayo inalazimu sasa mashirika ya kutoa elimu yaelekeze nguvu mashuleni huenda mashirika yaliyopo yalijikita kutoa elimu kwa watu wazima na wakawasahau wanafunzi.

Hakimu huyo mfawidhi alisema kuwa pia changamoto nyingine iliyopo ni sheria inayotoa adhabu kwa mwanafunzi anayempa mwanafunzi wa kike ujauzito kwani haitoi adhabu kali  isipokuwa inaelekeza kupelekwa katika magereza maalumu ya watoto ambako anakwenda kuendelea na masomo hivyo kitendo hicho kinasababisha baadhi yao kuto ogopa wakati mwanafunzi wa kike anapoteza fursa ya masomo.

Alisema kuwa pia ipo chanagamoto kwa baadhi ya kesi kukosa ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani watuhumiwa ama baadhi ya mashahidi wakiwemo waadhirika wa mimba za utotoni kutofika mahakamani hali inayosababisha baadhi ya kesi kufutwa na watuhumiwa kuachiwa huru kitendo kinachosababisha wananchi kuvitupia lawama vyombo vya sharia kuwa havitendi haki.

Kwaupande wake mratibu wa mradi wa kuzuia mimba za utotoni wilayani Nkasi Frank Nestory alisema kuwa tangu mradi huo ulipoanza kutekeleza wilayani humo kumekuwa na madiliko chanya kitendo kinachoonesha jamii hiyo ilikosa elimu.

Alisema kuwa wapo baadhi ya wazazi walikuwa hawatambui kuwa kumuozesha mtoto  wake  mdogo wa kike ni kosa kisheria kwani mlolo huyo ni wakwake kwahiyo hakuna mtu anayeweza kumzuia kufanya hivyo mradi aamue yeye mwenye mtoto.

Nestory alisema kuwa ni mtumaini yake mpaka mradi huo utakapokuwa umefikia mwisho suala la mimba kwa watoto wilayani Nkasi litabaki historia kutokana na elimu wanayoitoa sambamba na nmwitikio wa wananchi katika kuunga mkono jitihada za kutokomeza ndoa za utotoni pamoja na mimba.

Mwisho

No comments:

Post a Comment