Sunday 30 July 2017

Waacha vyandarua kuhofia kunguni

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
BAADHI ya wananchi wa naoishi katika bonde la ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wameacha kutumia vyandarua vilivyokuwa vikitolewa na serikali kupitia mradi wa hati punguzo wakidai kuwa vimesababisha kuwepo kwa kunguni katika nyumba zao. 
Wananchi hao walidai kuwa tangu kuanza kugawiwa kwa vyandarua hivyo kumekuwa na kunguni wengi tofauti na miaka ya nyuma hali iliyosababisha kuacha kutumia vyandarua hivyo. 
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Muze wilayani Sumbawanga Francis Kakole akizungumza na gazeti hili alisema kuwa wameacha kabisa kutumia vyandarua hivyo kwani tangu wameanza kuvitumia kumeibuka kunguni wengi na hivyo kusababisha kero kubwa kwa wananchi hao. 
Naye Peter Kalanda mkazi wa kambi ya wavuvi ya Kipa katika mwambao mwa ziwa Rukwa alidai kuwa hivi sasa kumekuwa na kunguni wengi katika maeneo yao na walipofanya utafiti waligundua kuwa chanzo cha kunguni hao kilikuwa baada ya kuanza kutumia vyandarua vilivyokuwa vikigawiwa bure  na serikali kwa wanawake wajawazito. 
"kabla ya kugawiwa vyandarua hivyo bonde letu lilikuwa halina kunguni lakini baada ya kugawiwa na kuanza kutumia vyandarua hivi kumeibuka kunguni hadi wamesababisha kero,ndio maana tumeamua kuacha kuvitumia kabisa."..alisema. 
Hii ilibainika baada ya mwandishi wa habari hizi kufika katika kambi ya uvuvi ya Kipa na kukuta wananchi wakiwa wanaishi bila kutumia vyandarua na wakati bonde hilo la ziwa rukwa lina mbu hali ambayo ni hatari kwa kupata ugonjwa wa malaria. 
Wananchi hao walimueleza sababu hiyo ambayo imesababisha wao waache kutumia vyandarua licha ya kuwa wapo wachache ambao wanatumia vyandarua ambavyo wamekuwa wakinunua madukani na si vile vya hati punguzo ambavyo vikigawiwa na serikali. 
Hata hivyo gazeti hili lilizungumza na Dkt Emmauel Mtika wa  hospitali ya mkoa wa Sumbawanga alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na kuongeza kuwa vyandarua hivyo vimewekewa dawa ambayo inafukuza kunguni na mbu na hivyo wanapo waona kunguni wanajua wamesababishwa na dawa hiyo. 
Alisema kuwa pia baadhi yao wamekuwa hawaumwi na mbu pindi wanapotumia vyandarua hivyo kwakua vinadawa ya kufukuza mbu na wanajikuta wamelala usingizi fofofo bila kushiriki tendo la ndoa na hivyo kusingizia kuwa vyandarua hivyo vinasababisha upungufu wa nguvu za kiume hali ambayo si kweli ni wao wanapitiwa na usingizi na wala si suala la vyandarua. 
Mwisho

No comments:

Post a Comment