Monday 31 July 2017

Sikaungu bado walilia ardhi kwaajili ya mashamba na kujenga

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
WAKAZI wa kijiji cha Sikaungu wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamelalamikiwa kitendo cha askari magereza wa gereza la Moro wakiwa na wafungwa kuwavamia na kuwatishia kwa kupiga risasi hewani wakidai kuwa wameingia na kuchungia ng'ombe katika eneo la gereza hilo. 

Tukio hilo lilitokea julai 28 majira ya saa 8 mchana baada ya wachunga ng'ombe hao kuwa wanachunga katika maeneo ya kijiji chao ambacho kinapakana na eneo la gereza hilo. 

Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa kijiji hicho William Khamsini alisema kuwa baadhi ya vijana walikuwa wakichunga ng'ombe wa familia ndipo waliposhangaa kuona askari magereza wanne wakiwa na wafungwa wanane wakiwa wamewazunguka na kuanza kuswaga ng'ombe wakidai kuwa wanachungia katika eneo la gereza hilo. 

Baada ya kitendo hicho vijana waliokuwa wamachunga mifugo hiyo walipiga kelele za kuomba msaada ambapo wananchi wengine walikwenda kuwasaidia na kisha kuibuka mzozo mkubwa baina ya wananchi hao na askari magereza pamoja na wafungwa. 

Kutokana na hali hiyo askari magereza hao walilazimika kupiga risasi hewani lakini wananchi hao hawakuogopa mpaka walipofanikiwa kuondoka na ng'ombe wao na askari polisi hao pia wakiwa na wafungwa waliondoka zao. 

Khamsini alisema kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo Kutoelewana baina ya wananchi hao na watumishi wa gareza hilo ambapo wananchi wamekuwa wakituhumiwa kuvamia eneo la gereza hilo na kuchungia mifugo yao kutokana na kijiji hicho kukosa ardhi ya kutosha kwakua eneo kubwa la kijiji hicho lipo katika shamba la Malonje linalomilikiwa na taasisi na gereza hilo pamoja na taasisi ya EFATA Ministry ambapo analimiliki kama mwekezaji. 

Kutokana na hali hiyo wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakikutana na changamoto ya kupigwa na kujeruhiwa pindi wanapoingia kuchunga ama kupita katika upande wa mwekezaji huyo ama upande wa eneo la magereza hali ambayo mwenyekiti wa kijiji hicho aliiomba serikali ya awamu ya tano kushughurikia suala hilo kwani limekuwa likisababisha kero kubwa kwa wananchi hao kwakua hawana eneo maeneo ya kulima, kuchungia mifugo pamoja kujenga nyumba za kuishi. 

Alisema kuwa wameamua kumuandikia barua mkuu wa mkoa wa Rukwa Zelote Steven ili awasaidie na kama suala hilo ataona liko nje ya uwezo wake alifikishe kwa raisi aweze kuwatatulia kero zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ardhi ya kulima na kujenga kwani imekuwa niyamuda mrefu. 

Hata hivyo kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa hawezi kuzungumzia chochote kwakuwa tukio hilo halijaripotiwa polisi,na alitoa wito kwa wananchi kuwa na tabia ya kutoa taarifa ya matukio yoyote yanayotokea. 

Mwisho

No comments:

Post a Comment