Wednesday 28 June 2017

Amuua mdogo wake kwa kumpiga mpini wa jembe

Na Gurian Adolf
Sumbawanga
Jeshi la Polisi mkoa wa Rukwa, linamshikilia mkazi wa kijiji cha Kilida kona wilayani Sumbawanga, Japhet Kigula kwa tuhuma ya kumuua mdogo wake kwa kumpiga mpini wa jembe kichwani wakati
akimuadhibu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juni 26 nyakati za saa 12 jioni katika kijiji hicho, ambapo aliyeuawa ni Makumbi Kigula.
Taarifa zinaeleza kuwa siku mbili kabla tukio mtuhumiwa ambaye alikuwa amesafiri kutoka mkoani Mwanza alimwita mdogo wake nyumbani kwake ili waweze kufanya mazungumzo ambayo hayakuwekwa bayana lakini kijana huyo hakuweza kwenda hali ambayo ilimkera Japhet.
Inasemekana kwamba juzi nyakati za jioni saa 11 kijana huyo alikwenda nyumbani kwa kaka yake na kuanza kuongea nae ambapo mtuhumiwa
alionekana kutofurahisha na kitendo cha mdogo wake kuchelewa kuitika wito wake.
Kutokana na hali hiyo, Japhet akisaidia na mmoja wa watumishi wake wa ndani walimkamata kijana huyo na kumfunga kamba mikono na miguu kisha
kaka mtu kuanza kumuadhibu kwa kutumia mpini wa jembe ambao alimpiga nao sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani huku damu
zikimtoka puani ndipo majirani walipoingilia kati.
Baada ya majirani kuingilia kati walimkimbiza katika zahanati ya kijiji iliyopo kijijini hapo lakini ilipofika jana mchana alifariki dunia.
Polisi walifika kijijini hapo na kumkamata mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye bado anashikiliwa kwa mahojiano kabla ya kufikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Katika hatua nyingine, Polisi inamshikilia dereva Josephat Salya mkazi wa Sumbawanga mjini kwa tuhuma za kumgonga kwa gari mtoto Eliud
Steven(5) mkazi wa kijiji cha Kipundu Kala tarafa ya Namanyere wilayani Nkasi.
Tukio la  kumgonga mtoto huyo lilitokea juni 27 saa 10:05 katika kijiji hicho wakati mtoto huyo akiwa anatembea barabarani.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa George Kyando alisema kuwa dereva huyo alikuwa akiendesha  gari lenye namba za usajili T 790 DEM T aina ya Tata Truck mali ya Assif Ashraf ambapo lilimgonga mtoto huyo na kufa papo hapo.
Alisema kuwa chanzo cha ajalia ni uzembe wa dereva kushindwa kujali watumiaji wengine wa barabara na hivyo kukosa umakini awapo
barabarani.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment