Friday 25 July 2014

Wazazi Sumbawanga mkoani Rukwa waomba kucharazwa mboko na walimu

Na Gurian  Adolf
Sumbawanga.

Baadhi ya wazazi katika kata ya Lusaka wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamemuomba kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Chrispine Mrwanda kupeleka ombi lao kwenye baraza la madiwani ili lipitishe kuwa sheria ambayo itawapa uwezo walimu wa kuwacharaza viboko baadhi ya wazazi wasiowatimizia mahitaji ya elimu watoto wao.

Ombi hilo walilitoa jana katika viwanja vya serikali ya kijiji hicho ambapo Idara ya elimu halmashauri hiyo ilikuwa ikifanya ziara yenye lengo kuboresha ufaulu katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni utekelezaji wa sera ya matokeo makubwa sasa (BRN) katika halmashauri hiyo.

Mmoja wa wazazi hao Datus Seleman alimuomba kaimu mkurugenzi huyo kupokea ombi kutoka kwa wazazi wa kata hiyo kuliomba baraza la madiwani kuanziasha sheria ndogo itakayo waruhusu walimu kuanza kuwachapa viboko wazazi wote ambao hawawatimizii watoto wao mahitaji ya elimu.

Alisema kuwa wapo baadhi ya wazazi wamekuwa hawajali kuhusu watoto wao kama wanakwenda hata shuleni ikiwa ni pamoja na kuwanunulia sare za shule, madaftari na michango mbalimbali kitu ambacho kinapaswa kuwa ni kosa la kisheria.

Naye bi Maria Maivune alisema kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakitumia pesa zao kwa kunywa pombe na kuoa wanawake wengi na hivyo kushindwa kuwahudumia watoto wao.

"nadhani kama wazazi hao wangekuwa wanacharazwa viboko na walimu labda wanaweza kubadirika kutokana na aibu ya kuchapwa huenda wakaanza kuwajali watoto wao".....alisema.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi Mlwanda alisema kuwa halmashauri itakachopaswa kufanya ni kuwabana wazazi hao ili waweze kutimiza wajibu wao wakuwapa mahitaji wanafunzui hao ili malengo ya BRN yaweze kutekelezeka katika Halmashauri hiyo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment