Wednesday 18 April 2018

CCM Rukwa yataka miradi ya maendeleo itekelezwe kwa kiwango

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

CHAMA cha Mapinduzi CCM mkoani Rukwa kimeitaka serikali kuhakikisha inashimamia miradi ya maendeleo ili itekelezwe ipasavyo kwani baadhi ya miradi hiyo imebainika kuwa chini ya kiwango.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho Clemence Bakuli alitoa agizo hilo jana alipokuwa katika ziara katika vijiji vya Kisumba,Kasanga pamoja na Kilewani baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa kata ya Kasanga wilayani Kalambo kuwa mradi wa maji uliojengwa katika kata hiyo ulioghalimu shilingi bilioni moja umeshindwa kuwatatulia tatizo la ukosefu wa maji.
Awali wakazi wa vijiji hivyo walimlalamikia katibu huyo wa itikadi na uenezi kuwa katika kata hiyo mwaka 2015 ulitekelezezwa mradi wa maji lakini katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja uliofuata matanki yalianza kuvuja na mabomba kuacha kupitisha maji hali ambayo hawakunufaika na mradi huo.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kasanga Paulo Sichilima alisema kuwa kutokana na wakazi hao kutopata maji inaonekana kuwa mradi huo ulitekelezwa chini ya kiwango ambapo pia kuna kila dalili ya ubadhirifu wa fedha katika mradi huo.
Alisema kuwa wakazi wa kata hiyo walifurahishwa na kitendo cha serikali kuwaondolea kero ya ukosefu wa maji ambao licha ya kuwasababishia adha ya kufuata maji katika umbali mrefu lakini pia walijua wataepukana na kuugua na magonjwa yatokanayo na kutumia maji yasiyo safi na salama kama kipindu pindu.
Naye Maria Sichone mkazi wa kiji cha kilewani kata ya Kasanga alisema kuwa lengo la serikali ya chama cha mapinduzi lilikuwa zuri ambalo ni kumtua ndoo kichwani mwanamke lakini changamoto iliyojitokeza ni baadhi ya watendaji wa serikali pamoja na makandarasi wasiokuwa waaminifu ndiyo wamekuwa wakihujumu jitihada hizo za serikali.
Aliiomba serikali ya mkoa huo kuunda timu ya wataalamu ili wakaukague mradi huo na watakaaobainika kuwa kikwazo katika ufanisi wa mradi huo wasifumbiwe macho wachukuliwe hatua za kisheria kwani zama za kuleana zimepitwa na wakati.
Kwaupande wake Katibu mwenezi wa CCM, Bakuli aliwataka watendaji wa serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inayo tekelezwa mkoani humo ifanyike kwa weledi mkubwa ili wananchi waweze kupata manufaa yaliyo kusudiwa.
Mwisho

No comments:

Post a Comment