Saturday 21 April 2018

Tibiweni upesi,muishi maisha marefu


Na Gurian Adolf
Sumbawanga

WAKAZI mkoani Rukwa wameshauria kuacha tabia ya kupuuza kutibiwa  magonjwa wanayougua kwa wakati kwani vifo vingi vinatokana na kutofanya maamuzi ya haraka ya kupata matibabu.

Ushauri huo umetolewa jana katika ukumbi wa mikutano wa hospital ya mkoa ya Sumbawanga na katibu tawala wa mkoa huo Benard Makali alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa ambapo walikuwa wakipewa elimu kuhusiana na kufanyika kwa chanjo ya kitaifa ya kuzuia saratani ya kizazi kwa watoto wa kike.

Alisema kuwa moja kati ya changamoto kubwa inayosababisha vifo vingi ni watu kutokuwa na utaratibu wa kupata matibabu haraka pindi wanapougua au kuhisi dalili za kuugua kitendo kinacho changia ongezeko la vifo.

Katibu tawala huyo wa mkoa wa Rukwa alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakitembea na magonjwa kwa muda mrefu mpaka wakifikia maamuzi ya kwenda kupata matibabu,ugonjwa unakuwa umefikia katika hatua mbaya zaidi.

Makali alisema kuwa hivi sasa sayansi ya afya imepiga hatua kubwa kila tatizo linaufumbuzi wake kinachotakiwa ni wananchi kujenga utamaduni wa kutibiwa haraka pindi anapohisi dalili za kuugua hali itakayo saidia watu kuishi maisha marefu hata kama wanamatatizo ya kiafya kwani wataalamu watawapa mbinu za kukabilia na tatizo husika.

''nichukue fursa hii kuwasihi wanahabari wa mkoa wa Rukwa waelimisheni wananchi umuhimu wa kupata huduma za matibabu kwa wakati kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia wananchi kuishi maisha marefu hata kama magonjwa waliyonayo hayana tiba, lakini wataalamu wa afya watawaelekeza namna ya kuishi maisha marefu'' alisema.

Aalisema kuwa katika mkoa huo serikali imeboresha huduma za afya na matibabu yanapatikana kila sehemu kinachotakiwa ni wao kutumia huduma hizo kwa wakati na baadhi yao waachane na dhana ya kuamini waganga wa jadi kwani baadhi yao wamekuwa si waaminifu na wanachangia vifo kwa kuwachelewesha wagonjwa kupata tiba sahihi.

Awali akimkabribisha katibu tawala huyo, mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Bonifas Kasululu alisema kuwa chanjo hiyo ya saratani ya shingo ya kizazi iataanza kutolewa katika mwezi huu wa April na itawalenga watoto wa kike wenye umri wa miaka 14.

Alisema kuwa chanjo hiyo imehakikiwa na shirika la afya duniani (WHO) pia na kuidhinishwa na malaka ya chakula na dawa hapa nchini (TFDA) hivyo ni salama na haina madhara na aliisihi jamii kuhakikisha inawaruhusu watoto wakike wakapate chanjo hiyo.

Kasululu alisema kuwa chanjo hiyo itakuwa ikitolewa daima kama chanjo nyingine  hivyo watoto wa kike wanaofikia umri huo wanapaswa kupata chanjo hiyo ili kuwakinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwani ni miongoni mwa salatani zinazo changia vifo kwa wanawake sambamba na saratani ya matiti.

mwisho

No comments:

Post a Comment