Tuesday 15 May 2018

waomba kupimwa tezi dume

Na Gurian Adolf
Sumbawa

WAKATI baadhi ya  wanaume jijini Dar es salaam wakipinga hoja ya mkuu wa mkoa huo Paul Makonda ya kupima saratani ya tezi dume nyumba kwa nyumba ,hali ni tofauti katika kijiji cha Zimba  halmashauri ya wilaya ya
Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo baadhi ya wanaume wameiomba idara ya afya wilayani humo kuwapima
saratani ya tezi dume kutokana na hofu kuwa saratani hiyo imekuwa
ikisababisha vifo vya wanaume wengi.

Ombi hilo walilitoa jana kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na
waandishiwa habari katika siku ya afya kijijini hapo ambapo wilaya ya
Sumbawanga kwa kushirikiana na mradi wa mama na mwana iliandaa siku
maalumu kwaajili ya kupima afya kwa wakazi wa kijiji hicho.

Mmoja wa wanaume walio hudhuria siku hiyo Peter Katyega alisema kuwa
pamoja na vipimo mbalimbali vinavyotolewa lakini angependa pia kupima
saratani ya tezi dume kwani ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha
vifo vya wanaume wengi na hakuna mkakati wa kuwahimiza wanaume wa
wilaya hiyo kwaajili ya kupima ili kubaini kama wanaugua saratani ya
tezi dume.

Alisema kuwa mara kwa mara wanawake wamekuwa wakihimizwa kupimwa
saratani ya matiti na hivi sasa wilaya hiyo imezindua chanjo kwaajili
ya saratani ya mlango wa kizazi kwaajili ya watoto wa kike wenye umri
wa miaka 14 lakini hakuna jitihada za makusudi za kuhamasasha sambamba
na upimaji wa saratani ya tezi dume kwa wanaume.

Naye Majaliwa Ntobo mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa inawezekana
baadhi ya vifo vya wanaume vinavyotokea katika kijiji hicho vingine
vinasababishwa na saratani ya tezi dume lakini kwakuwa hakuna
wataalamu wa kupima saratani hiyo na hawahamasishwi kufanyiwa
uchunguzi inaonekana kuwa wanakufa na magonjwa mengine,ambapo
wangeweza kutibiwa na wakaendelea kuishi.

Alisema kuwa imefika wakati sasa kwa watendaji wa idara ya afya
kubadili fikra kuacha kufikiria saratani ya matiti tu na badala yake
waanze kupima na saratani ya tezi dume ili kuokoa maisha ya wanaume
waliopo hatarini ambao wanasumbuliwa na ugonjwa huo.

Kwa upande wake Maria Kela mkazi wa kijiji cha Zimba alisema kuwa
pamoja na changamoto ndogo ndogo kama ukosefu wa mataktari bingwa
kwaajili ya kutibu  baadhi ya magonjwa lakini anaishukuru serikali
wilaya hiyo kwa kutenga walau siku mbili kwa mwaka kupima afya kwa
wakazi wa kijiji hicho kwani imesaidia watu wengi kujua matatizo ya
kiafya yanayo wasumbua.

Akizungumzia siku ya upimaji wa afya katika kijiji hicho mganga mkuu
wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Fani Musa alisema kuwa
halmashauri hiyo imetenga siku mbili katika mwaka kwa kila kijiji cha
wilaya hiyo ambapo wakazi wa kijiji husika wanapata fursa ya kupima
magonjwa mbalimbali pamoja na uchangiaji damu.

Alisema kuwa lengo ni kusaidia wanachi kutambua mapema magonjwa
yanayowasumbua na kuanza taratibu za matibabu mapema kabla hali
haijafikia katika hatua kubwa ambapo alisema kuwa itakuwa ni rahisi
kutibiwa na kuishi maisha marefu kwakuwa mgonjwa anakuwa anafahamu
tatizo lake mapema.

Musa alisema kuwa yeye binafsi anatoa wito kwa wakazi wa vijiji vya
halmashauri hiyo kujitokeza kwa wingi ili kutumia nafasi hiyo kupima
afya zao bila kujali kuwa hakuna madaktari bingwa ama baadhi ya
magonjwa hayafanyiwi vipimo lakini ni afadhali wakapima hata yatakayo
wezekana kuliko kukata tamaa na kuendelea kuishi na magonjwa mengi
zaidi.

Mwisho

No comments:

Post a Comment