Na Gurian Adolf
Nkasi
HALMASHAURI ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imetajwa kuwa ndiyo inayo ongoza kwa wanafunzi wanafunzi kupata ujauzito mkoani Rukwa na katika kipindi cha miezi tisa jumla ya wanafunzi 74 wamekatiza masomo kutokana na kupata ujauzito.
Akizungumza jana kwenye kikao cha baraza la madiwani afisa serikali za mitaa mkoani humo Albinus Mgonya alisema kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi april 30 mwaka huu wanafunzi 36 wanafunzi wa shule za msingi na wanafunzi38 wa sekondari walipata ujauzito.
Alisema kuwa kulingana na takwimu hizo inamaana kuwa wanafunzi wanaopata ujauzito ni sawa na kuwa kila mwezi wanafunzi wanne wa shule za msingi wanapata mimba sambamba na wanne wa sekondari wanapata ujauzito.
Mgonya alisema kuwa kutokana na hali hiyo ameiagiza halmashauri ya wilaya Nkasi kuandaa taarifa itakayoainisha idadi ya Watoto wenye mimba mahali walipo,wazazi wao ikiwa ni pamoja na viongozi wa maeneo yao hasa Watendaji wao wa vijiji na kata ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Katika hatua nyingine afisa huyo wa serikali za mitaa ameipongeza halmashauri ya wilaya Nkasi kwa kufanya vizuri katika makusanyo ya ndani ambapo hadi sasa makusanyo ni asilimia 76 na kuwa wilaya hiyo inaongoza kimkoa katika suala zima la makusanyo ikiwa ni pamoja na wilaya kuendelea kupata hati safi.
Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya hiyo Festo Chonya ameitaka halmashauri hiyo kutowahamisha watendaji wabovu bali washughulikiwe pale pale walipo ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi kwani serikali ya sasa haiwezi kuwahamisha watendaji wabovu kutoka eneo moja kwenda jingine.
Alisema kuwa katika mjadala ulioendelea katika kikao hicho madiwani walisema kuwa yupo afisa mtendaji mmoja wa kijiji ambaye ameonyesha uwezo mdogo wa kiutendaji na kuiomba halmashauri imuhamishe kutoka katika kijiji alipo na kwenda eneo jingine.
Chonya alisema kuwa serikali ya awamu ya tano haimuhamishi mtumishi ambaye ameshindwa katika eneo moja na kwenda eneo jingine na kuwa mawazo hayo ya madiwani si sahihi bali kama mtendaji huyo ameshindwa kuwajibika waanze mchakato mwa kumfukuza kazi na aajiriwe mwingine mwenye uwezo wa kazi.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Zeno Mwanakulya aliwataka watendaji wa halmashauri kuyasimamia yale yote yaliyoagizwa katika kikao hicho ,huku akisisitiza suala la uwajibikaji ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
Kaimu mkurugenzi wa halmahsauri ya wilaya hiyo Missana Kwangula alisema kuwa halmashauri ya wilaya inafanya kazi vizuri na ndiyo maana kila mwaka imekua ikipata hati safi hasa katika eneo la makusanyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment