Friday 25 May 2018

kipindu pindu chaibuka upya

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

UGONJWA wa kipindu pindu umeibuka tena katika wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa na katika kipindi kifupi cha siku kumi umesababisha vifo vya watu saba huku jumla ya watu 166 wakiwa wamekwisha ugua ugonjwa huo katika kipindi hicho.
Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dkt Halfan Haule alitoa taarifa hiyo jana katika kikao cha kamati ya afya ya mkoa huo ambayo ilikutana kwa lengo la kuweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa ya Ebola pamoja na kipindu pindu mkoani humo.

Alisema kuwa awali ugonjwa huo ulikuwepo katika wilaya hiyo kuanzia mwezi Novemba mwaka jana na jitihata za kuumaliza zilifanyia na ilipofika mwezi Machi mwaka huu ukawa umekwisha na katika kipindi hicho cha miezi mitano uliua watu saba.

Alisema kuwa hivi sasa ugonjwa huo umeibuka upya katika vijiji vya Maenje,Milepa,Kpaenta, Mkusi,Tunko na Laela ambapo uliripotiwa Mei 12 na tayari watu saba walikwisha fariki dunia katika kipindi kifupi cha siku kumina mpaka hivi sasa bado kuna wagonjwa 44 wakiwa wanatibiwa kipindu pindu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa sababu kubwa ya kuibuka upya kwa ugonjwa huo ni kutokana na kuwa hivi sasa wakulima wa mpunga wanavuna mbugani na hawana utamaduni wa kutumia maji yaliyochemshwa hali ambayo imesababisha kuibuka upya ugonjwa huo na kusababisha vifo hivyo.

Dkt Haule alisema kuwa hivi sasa wilaya hiyo inakabiliwa na ukosefu wa dawa za kutibu maji(water guard) ambapo alitumia fursa hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kusaidia upatikanaji wa dawa hizo ili zigawiwe kwa wananchi ambapo zitasaidia kupunguza kasi ya ugonjwa huo.

Katika kikao hicho mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Bonifas Kasululu alisema kuwa katika suala la ugonjwa wa Ebola tayari taratibu zote zimekwisha fuatwa ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya kuwapatia matibabu wagonjwa watakao onesha dalili za ugonjwa huo na vifaa kwaajili ya wahudumu wa afya vipo licha ya kuwa bado hakujaripotiwa mgonjwa wa Ebola katika mkuoa huo.

Kwaupande wake mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho aliagiza madaftari ya wakazi yaanze kutumika katika serikali za vijiji ilikuwatambua watu wanaoingia mkoani humo kwa lengo la kukabiliana na Ebola.

Pia Wangabo alisema kuwa ifike pahala ugonjwa wa kipindu pindu ukomeshwe kabisa katika mkoa huo kwani kunadalili kuwa ugonjwa huo umeanza kuzoeleka kwa wakazi wa mkoa huo kitu ambacho ni hatari.

Alisema kuwa changamoto kubwa kwa wananchi ni ukosefu wa elimu wa namna ya kujikinga na kipindu pindu ni lazima nguvu kubwa iwekezwe upande huo yeye hayupo tayari kuvumilia kuona watu wanakufa kwa ugonjwa huo.



Mwisho

No comments:

Post a Comment