Monday 12 February 2018

Waonywa kutotelekeza wagonjwa hospitalini

Na Gurian Adolf
Sumbawanga

Wakazi wa mkoani Rukwa wametakiwa kuacha tabia ya kutelekeza wagonjwa wao hospitalini kwa kisingizio cha kukwepa gharama za matibabu kwani kufanya hivyo kunazipa mzigo mkubwa hospitali wa kuwahudumia wagonjwa hao.

Katibu wa afya wa hospitali ya Kristu Mfalme, Sista Yasinta Rugabagi alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya hospitali hiyo wakati wa maadhimisho ya kikanisa ya siku ya wauguzi duniani yaliyoambatana na ibada ya kuwaombea wagonjwa waliolazwa hospitalini yaliyofanyika Katika hospitali hiyo iliyopo mjini hapa.

Sista Yasinta alisema kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wananchi kutelekeza wagonjwa wao waliougua kwa muda mrefu na kulazwa Katika hospitali hiyo, kitu ambacho kinailazimu hospitali kuwahudumia kila kitu kuanzia gharama za matibabu yao na chakula kwa siku zote wanazokuwa wakipata matibabu kwenye hospitali hiyo.

Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha hospitali kuelemewa na mzigo mkubwa wa kuwahudumia wagonjwa wao kwa kuwa inakabiliwa na changamoto ya fedha hivyo ifike wakati jamii ibadilike na kuachana tabia hiyo kwani kuendelea kufanya hivyo ni kutokuwa na upendo kwa wagonjwa hao. 

Pia alitaka jamii kujenga utamaduni  kutembelea wagonjwa na kutoka misaada mbalimbali kwa wagonjwa si tu wanaolazwa Katika hospitali hiyo lakini na maeneo mengine kwa kuwa wagonjwa wanahitaji kufarijiwa nyakati zote.

Awali, meneja wa mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Simon Mbaga alizitaka taasisi zilizo chini ya Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga kujiunga na mfuko wa Bima ya afya ili watumishi wao wawe na uhakika wa kupata matibabu pindi wanapougua maradhi mbalimbali.

Alisema kuwa baadhi ya watumishi wa taasisi hizo wamekuwa wakitumia gharama kubwa kupata matibabu kutokana na kutojiunga na bima ya afya hivyo wana fursa ya kujiunga na mfuko huo kupitia mpango wa uanzishwaji wa vikundi.

Aisha,  Kaimu mganga mkuu wa mkoa, Emmanuel Mtika aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kijitolea damu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwasaidia wagonjwa wenye mahitaji ya kuongezewa damu ili kuokoa maisha yao.

Alisema mahitaji ya damu bado ni makubwa Katika mkoa wa Rukwa, ambapo kwa mwezi huitajika lita 200 hadi 300 ambazo husaidia sana kuokoa maisha ya wakinamama wajawazito pindi wanapopungukiwa na damu baada ya kufanyiwa upasuaji. 

Mwisho

No comments:

Post a Comment