Wednesday 14 February 2018

Auawa kwa kukanyagwa na tembo

Na Gurian Adolf
Kalambo
MWANAMKE  aliyefahamika kwa jina la Maria Sekaye(60) mkazi wa kijijii cha Ilambila wilayani Kalambo  ameuawa baada ya kukanyagwa na tembo waliokuwa njiani wakitokea katika pori la akiba la Lwafu mkoani Rukwa kuelekea katika nchi jirani ya Zambia.
Akizungumzia tukio hilo diwani wa kata ya Mkowe Alfred Mpandasharo alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 4 za asubuhi wakati mwanamke huyo akiwa ametoka kutembelea shamba lake lililokuwa limevamiwa na mazao kuliwa na tembo hao.
Alisema kuwa Maria akiwa njiani kurejea kijijini ghafla alikutana na kundi kubwa la tembo waliokuwa na hasira wakiwa wamechokozwa na vijana wa kijiji hicho kutokana na kuwafukuza kwa makelele ili waondoke kijijini hapo waache kula mazao katika mashamba yao.
Diwani huyo alisema kuwa baada ya kundi hilo la tembo kumkuta mwanamke huyo lilimvamia na kuanguka chini ambapo alikanyagwa na kufa papo hapo.
Naye mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura aliwaonya wananchi wanao wafukuza hovyo tembo hao waache tabia hiyo kwani ni hatari kwa usalama wao wasubiri watendaji wa maliasili ambao watafika kwaajili ya kuwafukuza kijijini hapo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa  kwa kawaida katika vijiji vya  Sundu,Mkowe Ilambila na Katete huwa ni mapito ya tembo ambapo mara kwa mara wamekuwa wakipita kuelekea nchini Zambia na baadaye kurejea tena nchini katika pori la akiba la Lwafu.
Alisema kuwa nivizuri wananchi wakaacha kufanya kilimo na kujenga makazi katika mapito ya tembo hao kwakuwa kawaida huwa hawaachi kupita hata kama itachukua miaka mingi lakini kunasiku watarejea na kupita tena hivyo ni hatari kwao.
Mwisho

No comments:

Post a Comment