Wednesday 21 February 2018

Milioni 700 kujenga kituo cha afya

Na Gurian Adolf
Kalambo
WAKAZI wa kata ya Legezamwedo wilayani Kalambo mkoani Rukwa wanatarajia kuondokana na adha  ya kufuata huduma za afya umbali wa zaidi ya kilomita 50 baada ya serikali kutoa shilingi milioni 700 kwaajili ya kujenga kituo cha afya  katika kata hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura aliwaambia jana wakazi hao wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kata hiyo kuwa halmashauri ya wilaya ya Kalambo tayari imekwisha pokea fedha hizo na ujenzi wa kituo hicho cha afya utaanza ndani ya muda mfupi baada ya kukamilika taratibu zote.
Alisema kuwa fedha hizo zipo kinacho subiriwa ni kukamilisha taratibu ndogo ndogo na ujenzi utaanza baada ya muda si mrefu nay eye amekwisha agiza ukamilike ndani ya siku 90 ili wananchi waanze kupata huduma za afya katika kituo hicho cha afya.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kinachotakiwa ni wananchi wa kata hiyo kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano kwa kujitolea nguvu kazi pindi zinapo hitajika kwani zipo kazi kama za kuchima mitaro,kubeba zege na kusogeza tofali zinaweza kufanya na wananchi hao kwa kadiri ya maelekezo ya mafundi ujenzi.
‘’ndugu wanachi serikali imekwisha toa shilingi milioni 700,kinachotakiwa ni nyinyi kuunga mkono katika mchakato mzima wa ujenzi,sitaku kusikia kuna watu wanahujumu jitihada za serikali kwa kuiba vitendea kazi ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati’’ alisema
Alisema kuwa serikali imetambua shida wanayopata wananchi hao ndiyo maana imetoa fedha hizo ambazo zinapaswa kutumika kama zilivyo kusudiwa ambapo kata hiyo itapata kituo cha afya na wananchi watatibiwa katika kata hiyo bila usumbufu.
Awali kabla ya kumbalibisha mkuu huyo wa wilaya diwani wa kata hiyo Mwakyusa Larmeck aliishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo ambapo alisema wananchi wa kata hiyo walikuwa wakipata matibabu katika kituo cha afya cha Mwimbi kilicho umbali wa kilomita 50.
Alisema kuwa kituo hicho cha afya kitasaidia kupunguza idadi ya vifo vya wakina mama wajawazito na watoto ambao wangekufa kutokana na kuchelewa kupata huduma kwa wakati kutokana na umbali mkubwa uliopo mpaka kufikia kituo cha afya.
Naye Maria Namzosha mkazi wa kata hiyo aliiomba halmashauri hiyo kuwapangia watumishi katika kituo hicho mara baada ya ujenzi kukamilika ili waondokane na kero ya kutembea umbali mkubwa kufuata matibabu kwani wameteseka kwa muda mrefu.
Mwisho

No comments:

Post a Comment