Tuesday 31 July 2018

Washushwa vyeo kwa kutochukua hatua

Na Gurian Adolf
Nkasi

MKUU wa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Said Mtanda  ameagiza kushushwa cheo afisa elimu wa kata ya Kala pamoja na mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya msingi ya Kilambo cha Mkolechi  huku afisa mtendaji wa kijiji na afisa mtendaji wa kata wakitakiwa kukamatwa kufuatia tukio la Mwalimu mkuu wa shule hiyo Erad Kapyela kumpa mimba mwanafunzi na wao kutochukua hatua za haraka kumkamata kitendo kilicho sababisha mwalimu huyo kutoroka.

 Agizo hilo alilitoa jana katika baraza la madiwani  la halmashauri ya wilaya ya Nkasi baada ya kumebaini kuwa viongozi hao walikua wanalifahamu tukio hilo na wakakaa kimya bila kuchukua hatua yoyote  kutokana na uzembe huo wanatakiwa kuchukuliwa hatua.

Alisema kuwa wao wamefanya uchunguzi na kubaini kuwa mwalimu mkuu huyo amekuwa na tabia hiyo ya kuwapa mimba Wanafunzi ambapo mpaka sasa wanafunzi watatu wamezalishwa na  mwalimu huyo  huku wao wakikaa kimya pasipo  kuchukua hatua zozote na kuwa na wao wanaingia moja kwa moja katika adhabu.

 Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa inashangaza kuona jambo kama hilo linafanywa na mwalimu mkuu wakati wao wanafahamu vita vilivyopo sasa katika wilaya Nkasi ya kupambana na mimba kwa Wanafunzi  na viongozi  wa maeneo hayo wanakaa kimya  na kuwa sasa ni lazima Watendaji hao wawe mfano ili na waweze kujifunza namna ya kuchukua hatua za haraka pale wanapoona mambo hayaendi sawa

“kama viongozi hao wa vijiji na kata wangechukua hatua za haraka mwalimu mkuu huyo angekamatwa na asingepata nafasi ya kutoroka na watendaji wa namna hiyo hawatakiwi katika serikali ya awamu hii ya tano.

Sambamba na hilo aliwataka madiwani kuendelea kuisimamia halmashauri yao vizuri na kuwa mpaka sasa wilaya ipo vizuri hasa kwa kufanya vizuri katika makusanyo na kuongoza katika halmshauri zote nne za mkoa wa Rukwa ambapo  makusanyoi ya ndani yamefikia asilimia 89.97 kiwango ambacho ni kikubwa.

Aliwataka madiwani kuyasimamia mapato hayo vizuri  ili kuona kuwa zinarudi kwa wananchi  kwa kusaidia nguvu za Wananchi katika miradi mbalimbali ya maendeleo waliyoianzisha ili waone kuwa makusanyo yao yanawasaidia ili waweze kutoa mchango zaidi wa kuhakikisha kuwa halmashauri inakusanya zaidi na kuwa walinzi kwa wale wanaotorosha mapato.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Zeno Mwanakulya aliahidi kuendelea kuisimamia halmashashauri vizuri na kuwa maagizo yote ya serikali watayatekeleza.

Naye mkurugenzi wa wilaya  hiyo Missana Kwangula alisema  kuwa  wao kama halmashasuri wataendelea kusimamia misingi ya kiutumishi na kusimamiana ili kila mmoja aweze kutimiza wajibu wake kwa kutoa huduma bora kwa Wananchi

Mwisho

No comments:

Post a Comment