Tuesday, 16 May 2017

Swala ampeleka jela mwaka mmoja mtuhumiwa

Na Israel Mwaisaka
Nkasi

MKAZI wa kijiji cha Lyapinda tarafa ya Wampembe wilayani Nkasi mkoani Rukwa Derick simfukwe (25) amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Tshs,500,000 na mahakamama ya wilaya Nkasi kwa kosa la kukutwa na Nyara za serikali.

Mtuhumiwa alifikishwa katika mahakama ya wilaya Nkasi alipokutwa na nyama ya Insha kilo 6,huko kijijini kwao katika kijiji cha Lyapinda na kwenda kinyume na sheria ya uhifadhi Wanyama Pori na uhujumu uchumi.

Mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo mbele ya Mahakama, huku akiiomba mahakama hiyo isimpatie adhabu yoyote kwa maana hakujua kuwa mnyama huyo aina ya Insha ni nyara ya serikali.

Baada ya mtuhumiwa kukiri kutenda kosa hilo mahakama haikuhitaji kuita mashahidi zaidi na mtuhumiwa kukutwa na hatia chini ya kifungu cha sheria Na,86(1) (2) kifungu cha 57 (1) (2) na kifungu namba 57(1) 60 (2) sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na mwendesha mashitaka wa jeshi la Polisi Hamimu Gwelo uliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe ni fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutaka kutenda kosa kama hilo.

Upande wa utetezi mtuhumiwa aliiomba Mahakama isimpatie adhabu kali licha ya kuwa hakujua kuwa ile ni nyara ya serikali lakini yeye anafamilia kubwa inayomtegemea.

Mahakama ilitoa adhabu hiyo ya kifungo jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Tshs,500,000 na alishindwa kutoa faini na amekwenda jela kutumikia adhabu hiyo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment