Tuesday, 16 May 2017

Wazazi kumalizana nje ya mahakama kikwazo cha kumaliza mimba za utotoni

Na Gurian  Adolf
Nkasi
MOJA kati ya changamoto kubwa zinazo kwamisha jitihada za mapambano dhidi ya tatizo la  mimba za utotoni wilayani Nkasi mkoani Rukwa ni tabia  ya baadhi ya wazazi kumalizana nje ya mahakama.

Hayo yamebainishwa na Ramadhan Rugemalira ambaye ni  hakimu mkazi wa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wakati akifungua semina ya siku  mbili iliyoandaliwa na shirika la Plan International ambayo iliwakutanisha wajumbe wa kamati ya wilaya ya ulinzi wa mtoto wa kike na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha afya cha Mtakatifu Bakita kilichopo wilayani humo.
Ramadhan Rugemalira ambaye ni  hakimu mkazi wa wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, akizungumza wakati akifungua semina ya siku  mbili iliyoandaliwa na shirika la Plan International ambayo iliwakutanisha wajumbe wa kamati ya wilaya ya ulinzi wa mtoto wa kike.

Alisema kuwa pamoja na mikakati mingi inayowekwa kupitia serikali, jamii na sekta mbalimbali bado suala la  wazazi kumalizana nje ya mahakama limekuwa ni changamoto kubwa kwani ikitokea mtoto amepata ujauzito wamekuwa wakikutana na kulipana bila kwenda kwenye vyombo vya sheria.

Rugemalira alisema kuwa hata  kesi chache ambazo zimekuwa zikifikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria wazazi wamekuwa hawahudhurii matokeo yake  mahakama imekuwa ikilazimika kuzifuta na hivyo haki ya kukumu inakosekana kutokana na wazazi kumalizana nje ya mahakama.
Nestory Frank ambaye ni mratibu wa ndoa za utotoni kutoka shirika la Plan International akizungumza na wajumbe wa kamati ya wilaya ya ulinzi wa mtoto wa kike wilayani Nkasi.

Naye Nestory Frank mratibu wa ndoa za utotoni kutoka shirika la Plan International alisema kuwa lengo la  mafunzo hayo ni  kuendelea kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hiyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
wajumbe wa kamati ya wilaya ya ulinzi wa mtoto wa kike wakifuatilia kwa umakini mada zinazo wasilishwa katika semina ya siku mbili.

Alisema kuwa mradi huo unatekelezwa katika kata  tatu wilayani humo ambazo ni  kata ya Mtenga, Mkwamba na Nkandasi ambapo umesaidia kuleta uelewa kwa wazazi ambapo ni  matumaini ya shirika hilo  kuwa baada ya muda jamii itabadirika na pengine ndoa za utotoni zikapungua.

Akimshukuru mgani rasmi baada ya kufungua mafunzo hayo, sheikh wa wilaya ya Nkasi Hadhiri Daruesh alisema kuwa niwakati kwa jamii kurejea katika maadili kwanzia watoto mpaka watu wazima.
wajumbe wa kamati ya wilaya ya ulinzi wa mtoto wa kike wakisikiliza kwa umakini mada zinazo wasilishwa katika semina ya  siku mbili.
Alisema changamoto ya mimba za utotoni linatokana na jamii kutokuwa na hofu ya Mungu hivyo kuanza kushiriki vitendo vya ngono katika umri mdogo na hivyo kupelekea kupata mimba.

Kiongozi huyo  wa kiroho alisema kuwa viongozi wa dini na madhehebu wanajukumu kubwa la  kuendelea kuhubiri ili watu warejee katika maadili huenda pia ikachangia kupungua tatizo hilo la  mimba za utotoni wilayani humo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment